Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mhe Miraji J. Mtaturu akifungua mipira aliyoigawa kwa timu zote shiriki za mashindano ya mpira wa miguu maarufu kama "IKUNGI ELIMU CUP 2017"
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mhe Miraji J.
Mtaturu akionyesha moja ya mipira aliyoigawa kwa timu shiriki kwenye mashindano
ya mpira wa miguu maarufu kama "IKUNGI ELIMU CUP 2017"
Baadhi za jezi
zilizotolewa kwa ajili ya timu zote shiriki kwenye
mashindano ya mpira wa miguu maarufu kama "IKUNGI ELIMU CUP 2017"
Na
Mathias canal, Singida
Takribani timu 69
zinazoshiriki mashindano ya mpira wa
miguu maarufu kama “IKUNGI ELIMU CUP
2017” zimekabiziwa jezi pamoja na mipira kwa ajili ya utimilifu wa kuwa na
vifaa vya michezo kwenye mashindano hayo jambo ambalo limeibua hisia chanya kwa
kila timu kutaka kuibuka mshindi.
Akitoa vifaa hivyo vya
michezo kwa ajili ya ushiriki wa timu hizo, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji
Jumanne Mtaturu alisema kuwa Ofisi yake kwa ushirikiano mkubwa na wadau wa
elimu na wananchi kwa ujumla wamechangia vifaa hivyo vya michezo ikiwa ni
sehemu ya kuongeza chachu ya hamasa katika mashindano na kufikisha zaidi ujumbe
wa umuhimu wa waanchi kuchangia mfuko wa elimu.
Mashindano hayo
yanayoshadihishwa na kauli mbiu isemayo CHANGIA,
BORESHA ELIMU IKUNGI yanafanyika katika vijiji vyote 101 ambapo katika
Jimbo la Singida Magharibi lenye kata 15 kila Kata itatoa timu mbili na Jimbo
la Singida Mashariki lenye Kata 13 kila kata itatoa timu tatu hivyo kuwa na
timu 69 zitakazopambana na kupatikana timu tatu bora.
Mhe Mtaturu alisema
kuwa kunzishwa kwa mashindano hayo ni kusudio la kuifanya jamii kujihusisha na
shughuli za maendeleo kwa kushirikiana na serikali, kuibua vipaji vya michezo
katika Wilaya ili kukuza ajira na kufanya vijana waachane na utumiaji wa madawa
ya kulevya.
Sababu zingine ni
Kuunganisha jamii kuwa kitu kimoja hatimaye vijana na wananchi kuimarisha
upendo, ajira na afya sambamba na kudumisha amani na mshikamano.
Mashindano hayo
yanataraji kufika ukomo Septemba 19, 2017 huku zawadi zikitaraji kutolewa kwa
washindi watano ambapo mshindi wa kwanza atapatiwa zawadi ya Kombe, Seti ya
jezi, Mipira miwili na kitita cha shilingi 1,000,000/= , na mshindi wa pili
atapatiwa Seti ya jezi, Mipira miwili na shilingi 750,000/=.
Mshindi wa tatu
atapatiwa Mipira miwili na shilingi 450,000/= , Mshindi wa nne atapatiwa Mpira
mmoja na Shilingi 200,000/= huku mshindi wa tano akipatiwa Mpira mmoja na
Shilingi 100,000/=.
Aidha, kutakuwa na
zawadi zingine kwa timu yenye nidhamu, Zawadi ya mfungaji bora, Zawadi ya Kipa bora,
Zawadi ya mchezaji bora, huku wachezaji wengine 30 wakichaguliwa kuingia
kambini kufundishwa mbinu za uchezaji bora.
Katika taarifa ya Mkuu
wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu wakati wa uzinduzi wa ligi hiyo mbele
ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt Angelina M. Lutambi aliyemuwakilisha
Mkuu wa Mkoa huo Mhe Dkt Rehema Nchimbi, alisema kuwa Idara ya elimu katika Wilaya
hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa nyumba za walimu,
Upungufu wa Walimu, Maabara ya Masomo ya sayansi kwa shule za sekondari, pamoja
na vifaa vya kujifunzia na kufundishia.
Hivyo Halmashauri ya
Wilaya ya Ikungi kwa ushirikiano na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo walianzisha
mfuko wa elimu wilaya kwa mujibu wa sheria ndogo ya Halmashauri Wilaya ya
Ikungi ya mwaka 2014 ambayo ilitolewa katika tangazo la serikali Na. 222 la
tarehe 11 Julai, 2014 ili kuweza kukabiliana na changamoto za elimu ambazo
zinaathiri mafanikio ya elimu katika Wilaya hiyo.
Kuanzishwa kwa mfuko wa
elimu kumepelekea pia kufunguliwa kwa akaunti ya mfuko katika Benki ya NMB tawi
la Ikungi kwa jina la Mfuko wa Elimu wa
Wilaya ya Ikungi (Ikungi District Education Funds) akaunti Namba 52510000554.
Hata hivyo Mhe Mtaturu
alitoa Rai kwa wadau wa elimu kuchangia mfuko wa elimu ili kukuza ufanisi wa
elimu katika Wilaya hiyo ambao kwa kiasi kikubwa unategemea zaidi upatikanaji
wa rasilimali fedha na nguvu kazi kutoka kwa wadau, wananchi, Taasisi,
Mashirika, Makampuni mbalimbali yaliyopo ndani na nje ya nchi.
MWISHO
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia