Mkuu wa Polisi Jamii mkoa wa Arusha Mkaguzi wa Polisi Shabani Shabani
akitoa ufafanuzi juu ya sheria ndogo ndogo zinazoweza kumbana mtu
atakayekaidi kulipa michango ya ulinzi shirikishi katika eneo lake
Diwani wa kata ya Moivaro Bw. Rick Moiro akichangia jambo katika mkutano uliokuwa unazungumzia juu ya ulinzi shirikishi katika kata yake
Viongozi wa kata na mitaa wametakiwa kutoumiza vichwa vyao na
kuvutana mashati na wananchi watakaokaidi kutoa michango katika masuala ya
ulinzi na badala yake wanatakiwa wawabane kwa kutumia sheria.
Akizungumza jana katika mkutano uliofanyika mtaa wa Moshono
Kaskazini kata ya Moivaro tarafa ya Suye halmashauri ya jiji la Arusha, Mkuu wa
Polisi Jamii mkoa wa Arusha, Mkaguzi wa Polisi Shabani Shabani aliwaambia viongozi
pamoja na wananchi kuwa wanaweza kutunga sheria ndogo ndogo kupitia sheria ya
serikali za mitaa ya mwaka 2000.
“Hakuna haja ya kuumiza kichwa bali viongozi mnapaswa kutumia
kifungu namba 163 na 164 katika kitabu hicho wamezungumzia namna ya kutunga sheria
ndogo ndogo kulingana na mahitaji ya eneo lenu”
“Lakini pia kifungu namba 167 kinazungumzia adhabu zinazoweza
kutolewa kwa mtu yeyote ambaye hatashiriki au atakayeshawishi kukwamisha
masuala ya ulinzi atatozwa faini ya Shilingi 50,000”. Alifafanua Mkaguzi huyo
wa Polisi Shabani Shabani.
Alisema pia mbali na kitabu hicho cha sheria pia katika ibara
ya 27 na 28 za katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinazungumzia wajibu
wa kila mtanzania juu ya ulinzi wa mali za umma pamoja na kulilinda Taifa hivyo
aliwataka viongozi hao wafanye kazi zao kwa kujiamini na wafahamu kwamba sheria
juu ya hilo zipo wazi.
Alizidi kuhamasisha viongozi hao kufufua kikundi cha ulinzi
shirikishi ambacho kinaonekana kusimama katika uteketezaji wa majukumu yake, na
kutoa mifano ya baadhi ya kata zilizopo halmashauri ya jiji la Arusha ambazo zimepiga
hatua kubwa katika kuimarisha vikundi hivyo vya ulinzi shirikishi ambapo wana
sare pamoja na silaha za moto na kuongeza kwamba hali hiyo inatokana na hamasa
ya wananchi wenyewe.
Alisema vikundi hivyo vina faida kubwa katika suala zima la
kuimarisha ulinzi hasa ikizingatiwa kwamba askari wa Jeshi la Polisi wao pekee
hawatoshelezi kusambaa kila mitaa kwa mara moja kutokana na idadi yao kuwa
ndogo kauli ambayo iliungwa mkono na Mwenyekiti wa mtaa huo Bi. Janeth Jonas.
Akichangia wazo katika mkutano huo Diwani wa kata ya Moivo
Bw. Rick Moiro alisema pamoja na utaratibu wa kuwatambua na kuwabainisha
wahalifu kwa njia za siri kuendelea katika kata hiyo, lakini akasema ni vyema
Jeshi hilo likaanza kuwakamata wahalifu wanaojulikana badala ya kusubiri mpaka orodha
ya wahalifu wengi ipatikane.
Akijibu malalamiko ya wananchi hao waliohudhuria kikao hicho
juu ya baadhi ya askari wa vikundi shirikishi hao kutoonekana mitaani wakati wa
usiku kwa madai kwamba huwa wanakwenda kulala, Mtendaji wa Kata hiyo Bw.
Goodluck Anderson alisema kwamba kwa sasa wananchi waondoe hofu na kuahidi
kulisimamia jambo hilo kwa ukaribu zaidi ili kuweza kubaini ukweli wa
malalamiko hayo.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia