Askofu Dkt Mdegella akizungumza na wanahabari
Na MatukiodaimaBlog
KATIKA harakati za kukinusuru chuo kikuu cha Tumaini Makumira tawi la Mbeya kisipigwe mnada na benki ya biashara ya Afrika (CBA) askofu mstaa wa kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT) dayosisi ya Iringa ambae pia ni mwenyekiti wa bodi ya Chuo hicho Dkt Owdenburg Moses Mdegela amesema ameamua kujilipua kunusuru chuo hicho kwa kuanza kutembeza bakuri kwa waumini wote wa KKKT nchini wakiwemo viongozi na wanasiasa ambao ni walutheri kama mke wa Rais wa awamu ya tatu mama Anna Mkapa na wengine
Dkt Mdegella amesema amechukua hatua hiyo ya kujilipua baada ya kuona dalili ya chuo hicho kupigwa mnada akizungumza na wanahabari juu ya hatua hiyo aliyochukua Dkt. Mdegela a alisema chuo hicho ambacho ni sehemu ya kanisa
hilo kipo katika hatari ya kuzama kwa kushitakiwa na kuuziwa
mali zake, na kuitia aibu KKKT kama uvumilivu wa benki hiyo
utafika mwisho kwa kushindwa kulipa deni hilo.
Alisema ameamua kujilipua na kuomba
msaada huo kupitia vyombo vya habari baada ya kuona jitihada
na mikutano mingi ya kulipa deni na malimbikizo yake ya riba
kwa kupitia taratibu za kawaida za kanisa yakipata vikwazo
kila wanapokutana kujadili.
Alisema Desemba, 2013 chuo hicho
kilikopa kutoka katika benki hiyo zaidi ya Sh Bilioni 1.6
kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala na madarasa ya chuo;
mkopo ambao sehemu yake haukutumika kwa kazi iliyokusudiwa.
Bila kutaja majina ya wahusika wa
matumizi mabaya ya fedha za mkopo huo, Dk Mdegela alisema
baadhi ya wajumbe wa bodi na viongozi wa chuo hicho
wanapaswa kubeba lawama na kuchukuliwa hatua za kisheria
kutokana na ubadhirifu uliofanywa.
“Tumefanya ukaguzi wa hesabu za mkopo
huo mara mbili. KKKT ilifanya ukaguzi wake lakini pia
kulikuwa na mkaguzi wa nje. Kwa pamoja wamebaini kuwepo kwa
ubadhirifu mkubwa, rushwa na ufisadi” alisema.
Alisema ukaguzi wa awali unaonesha
asilimia 45 ya mkopo huo ndiyo iliyotumika kwa kazi
iliyokusudiwa huku asilimia 55 iliyobaki ikitumika kwa
malengo tofauti na ujenzi uliokusudiwa.
“Suala hili limeshakabidhiwa Polisi
na kwa wanasheria ili hatua za kisheria kwa wahusika
zichukuliwe. Na kwa taarifa ni kwamba wahusika wanaotuhumiwa
kwa ubadhirifu huo wamekwisha simamishwa kazi,” alisema
bila kuwataja wahusika hao.
Dk Mdegela ambaye pia ni mwenyekiti wa
timu ya maaskofu watatu wa kunusuru chuo hicho (Dk Mdegela,
Dk Alex Malasula na Dk Abednego Mshahara) alisema kwa
makubaliano ya kulimaza suala hilo kiungwana, benki hiyo
imewataka kulipa Sh Milioni 275 ifikapo mwishoni mwa mwezi
huu na kwamba marejesho ya deni hilo yataendelea kufanywa
kila mwezi.
“Mahali lilipofika suala hili sio
mahali pa kunyamaza, tunataka kila mlutheri na sharika
zake zote nchini zijue kinachoendelea na wachangie kunusuru
chuo hicho ili kuliondolea kanisa aibu,” alisema.
Alisema ili kufikia makusanyo hayo
kutakuwa na makundi manne, la kwanza litajumuisha watu
watakaombwa kuchangia Sh 100,000 na kuendelea, la pili
watachangia kati ya Sh 50,000 na Sh 100,000, la tatu kati ya
Sh 20,000 na Sh 50,000 na la nne kiasi chochote chini ya Sh
20,000.
Pamoja na mapendekezo hayo alisema,
watu wataruhusiwa kuchanga zaidi ya kiwango
kinachopendekezwa katika makundi yao kwa kadri
watakavyoguswa na jambo hilo alilosema ni tatizo kwa
kanisa.
“Lakini pia nitalazimika kukutana na
walutheri maarufu ambao ni waajiriwa katika taasisi
mbalimbali, wafanyabishara na wanasiasa na wadau wengine wa
KKKT nchini,” alisema na kuwataja baadhi yao kuwa ni
pamoja na Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi na
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei.
Pamoja na kupitisha kapu hilo, alisema
wanaendelea kuandaa njia nyingine zitakazosaidia kufikia
lengo la makusanyo na marejesho ya deni hilo hadi
litakapokwisha.
Dk Mdegella aliwataka wadau hao
kuchangia chuo hicho kupitia akaunti maalumu No 108433100028
iliyofunguliwa katika benki hiyo ya CBA kwa ajili ya
kukusanya na kulipa deni hilo.
Alisema yote hayo anayafanya kwa niaba
ya Mkuu wa Kanisa, Askofu Dk Frederick Shoo na kwa niaba ya
askofu wa dayosisi ya Iringa, bodi ya wadhamini ya chuo,
baraza la uongozi na maaskofu wenzake na wajumbe waliopewa
kazi ya kunusuru chuo hicho.
Kwa yoyote anayehitaji ufafanuzi
zaidi anaweza kuwasiliana wa jinsi ya kukisaidia chuo hicho
anaweza kuwasiliana name kupitia simu yangu ya mkononi namba
0754313173,” alisema.
|
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia