Mkurugenzi
Mkuu wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.
Hassan Abbasi (katikati) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari
(hawapo pichani) wakati akitoa onyo kwa magazeti ya Mwananchi na Nipashe
kwa kuandika vichwa vya habari vinavyohukumu, kulia ni Mkurugenzi
Msaidizi kitengo cha Habari, Rodney Thadeus na kushoto ni Mkurugenzi
Msaidizi kitengo cha Usajili, Patrick Kipangula.
Mkurugenzi
Mkuu wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.
Hassan Abbasi (katikati) akionesha waandishi wa habari (hawapo pichani)
gazeti la Mwananchi lenye kichwa cha habari kinachotoa hukumu, kulia
ni Mkurugenzi Msaidizi kitengo cha Habari, Rodney Thadeus na kushoto ni
Mkurugenzi Msaidizi kitengo cha Usajili, Patrick Kipangula.
Mkurugenzi
Mkuu wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.
Hassan Abbasi (katikati) akionesha waandishi wa habari (hawapo pichani)
gazeti la Nipashe lenye kichwa cha habari kinachotoa hukumu, kulia ni
Mkurugenzi Msaidizi kitengo cha Habari, Rodney Thadeus na kushoto ni
Mkurugenzi Msaidizi kitengo cha Usajili, Patrick Kipangula.
Picha na Eliphace Marwa - Maelezo
Na: Neema Mathias-MAELEZO
Serikali
imevionya vyombo vya habari nchini hususan baadhi ya magazeti ambayo
yamekuwa na mtindo wa kuandika habari pasi na kuzingatia maadili na
weledi wa kitaaluma.
Akizungumza
katika mkutano na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa Idara ya
Habari-MAELEZO jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu, Idara ya Habari
–MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi alitahadharisha
kuwa aina hiyo ya uandishi unaweza kuleta madhara kwa jamii.
Katika
onyo hilo, Dkt. Abbasi ametolea mfano vichwa vya habari katika kurasa
za kwanza za magazeti ya Nipashe na Mwananchi matoleo ya leo Jumatano
Agosti 30, 2017 ambavyo alisema vimelenga katika kuwatia hofu wananchi,
kuleta taharuki na kuashiria sintofahamu kati ya wananchi na Serikali.
Katika
matoleo hayo ya leo Gazeti la Nipashe liliongozwa katika taarifa yenye
kichwa cha habari “NI MATESO” na Gazeti la Mwananchi liliongozwa na
habari yenye kichwa cha habari “Bomoabomoa Nyingine ya Kufa Mtu yaja
Dar”.
Mkurugenzi
Mkuu huyo na Msemaji Mkuu wa Serikali alifafanua kuwa wakati kichwa cha
habari cha gazeti la Nipashe kililenga kuwatia hofu wananchi na
kusababisha taharuki katika zoezi linalofanyika kisheria kichwa cha
habari cha Mwananchi kinatoa taswira kama kwamba watakaobomolea nyumba
zao kisheria wajiandae kwa vita na taharuki.
“Zoezi
linaloendelea linafuata sheria na taratibu kulingana na aina ya zoezi.
Ziko nyumba ambazo zina amri za mahakama, wako waliopewa onyo la
kuondoka katika maeneo ambayo ni hatarishi kama bonde la Msimbazi”
alieleza Dk. Abbasi na kueleza kuwa katika kutekeleza zoezi hilo kama
zimejitokeza karsoro hazina budi kurekebishwa.
Dk.
Abbasi aliwaeleza waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo kuwa
Serikali haina nia ya kuyachukulia hatua magazeti hayo lakini alitumia
fursa hiyo kuyatahadharisha magazeti hayo na magazeti mengine pia yenye
mtindo wa kuandika vichwa vya habari vinavyohukumu kuacha mtindo huo
vinginevyo sheria itachukua mkondo wake.
“Waandishi
wa habari tuna misingi yetu ya uandishi hivyo hatupaswi kuandika kichwa
cha habari kinachohukumu ama kutia hofu kwa jamii, hivyo navipa onyo
vyombo vinavyoandika vichwa vya habari vyenye maudhui kama hayo” Dkt.
Abbasi alisisitiza.
Mkurugenzi
Mkuu huyo na Msemaji Mkuu wa Serikali alivitaka vyombo vya habari
kusimamia ukweli na kufanya uchambuzi ili kusaidia jamii badala ya
kuandika mambo kwa sababu tu yametokea.
Alitolea
mfano kuwa inashangaza kuona baaadhi ya vyombo vya habari vinashindwa
kuona ukweli kuhusu hatari za watu wanaoishi maeneo hatarishi kama bonde
la Msimbazi na kusubiri kuandika habari za misaada kwa watu hao wakati
wa majanga.
Kwa
hivyo, alitumia fursa hiyo kuvikumbusha tena vyombo vya habari kuwa
tasnia ya habari ni taaluma yenye misingi na maadili yanayopaswa
kuzingatiwa na pale misingi na maadili hayo yatakapoendelea kukiukwa
Serikali haitasita kuchukua hatua kali zaidi za kisheria kwa maslahi ya
taaluma na jamii.