BREAKING NEWS

Saturday, August 19, 2017

THANDA: KISIWA KINACHOPATIKANA TANZANIA AMBAPO KULALA USIKU MMOJ A INAGHARIMU ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 22



Na Jumia Travel Tanzania

Inawezekana usiamini kwamba kuna sehemu zinagharimu zaidi ya shilingi milioni 22 za kitanzania kulala kwa usiku mmoja tu! Amini au usiamini sehemu hizo zipo, tena hapa hapa nchini kwetu Tanzania.

Jumia Travel ingependa kukujulisha kwamba kupitia shughuli za kitalii, hakuna kinachoshindikana. Linapokuja suala la kujionea mazingira adimu na ya kuvutia au wanyama wa aina mbalimbali, gharama au umbali wa kuyafanikisha hayo huwa siyo masuala ya msingi.


Thanda, ni sehemu kwa ajili ya mapumziko iliyotengenezwa na mtu binafsi katika eneo la kisiwa cha Shungimbili kilichomo Wilaya ya Kisiwa cha Mafia. Kisiwa hiki kina ukubwa wa takribani hekari 20 ambamo ndani yake imejengwa nyumba moja. Nyumba hiyo ina vyumba vya kulala vitano na vibanda viwili pembezoni mwa ufukwe wa bahari ya Hindi kusini mwa Tanzania ambapo familia ya watu mpaka 10 inaweza kuishi.
Ili kuweza kuishi kwenye kisiwa hiki, wamiliki hutoza wageni kiasi cha dola za kimarekani 10,000 kwa usiku mmoja ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 22 za kitanzania. Mazingira ya kuvutia, utulivu wa hali ya juu na namna eneo hili lilivyotengenezwa ndivyo vinavyowafanya watalii kulipia gharama hizo lisiwe ni jambo la kushangaza. Ni jambo la kawaida ukiwa mapumzikoni kisiwani humo kuwaona au kuogelea pamoja na viumbe wa baharini kama vile pomboo (dolphin), papa wakubwa (whale sharks) na kobe wa majini.

Wamiliki wa kisiwa hiki binafsi cha mapumziko, wanandoa Bw. Dan na Bi. Christin Olofsson ambao asili yao ni Sweden walipata wazo la kutengeneza sehemu hii ikiwa ni kwa ajili ya kupumzikia pamoja na watoto wao watatu na wajukuu nane. Kikubwa kilichowasukuma kufanya hivyo ni katika jitihada za kubadili mazingira hususani hali ya hewa ukizingatia nchi za Scandinavia wanapotea hukumbwa na baridi kali kwa vipindi virefu vya majira ya mwaka. Walianza kwa kuwekeza Afrika ya Kusini kutokana na kuvutiwa na wanyama na uoto wa asili kabla ya kuja nchini Tanzania.  
Miongoni mwa masuala ambayo yalizingatiwa kabla ya uwekezaji katika kisiwa hiki ni pamoja na kulinda vivutio vya kitalii na kuhifadhi viumbe wa baharini katika eneo hilo. Kwa kushirikiana na Mamlaka ya Uhifadhi wa Baharini ya Kisiwa cha Shungimbili, wamiliki wa Kisiwa cha Thanda wanashirikiana kwa ukaribu kuhakikisha jitihada za kulinda na kuendeleza uhifadhi wa vivutio vyake unazingatiwa.
Mbali na hayo, Kisiwa cha Thanda kinahakikisha kwamba jamii ya wakazi wanaoishi karibu na sehemu hiyo ambapo ni Kisiwa cha Mafia, wanafaidika na uwekezaji huo. Wakazi wake wananufaika kupitia ajira, uchangiaji kwenye shughuli za maendeleo ya elimu pamoja na uhifadhi wa viumbe wa baharini ambalo ndio kipaumbele kubwa.    
Tanzania inazo fursa nyingi za kitalii ambazo watu kutoka mataifa ya nje wanaziona na kuzitumia ipasavyo. Jumia Travel inaamini kwamba kupitia makala haya utakuwa umejifunza mambo mengi kuhusu Kisiwa cha Thanda ambayo hukuyajua hapo awali. Ni fursa kwako kuendelea kutafuta na kujifunza vivutio vinavyopotikana sehemu nyingine za nchi.  

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates