Mbunge wa jimbo la Arusha mjini,Godbless Lema amekeme
wimbi la utekaji watoto lililoibuka hivi karibuni jijini Arusha na kuitaka serikali pamoja na jeshi la
polisi mkoani hapa kuchukua hatua mara moja ili kudhibiti matukio hayo.
Lema,alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akiongea na waandishi
wa habari ofisini kwake akiwa ameambatana na mwenyekiti wa mtaa wa Olkeryan
kata ya Olasiti jijini hapa ,Daud Safari ambaye katika mtaa wake jumla ya
watoto watano wanadaiwa kutekwa.
Mbunge Lema alisema kwamba katika siku za hivi karibuni kumeibuka
wimbi la utekaji watoto ndani ya jiji la Arusha ambapo kwa taarifa za awali
alizopokea ofisini kwake jumla ya watoto watano tayari wameshatekwa na
hawajulikani walipo huku watekeji wakiacha ujumbe wa kutaka malipo ili
wawarejeshe watoto hao.
Lema,alisema kwamba watekaji hao wanadai malipo ya juu ambayo
ni kati ya sh, milioni 4 mpaka 5 jambo
ambalo linapaswa kukemewa vikali na kulitaka jeshi la polisi mkoani hapa kuchukua
hatua za haraka kukomesha matukio hayo.
Alisema kwamba watekaji hao wamekuwa wakitumia mbinu za
kuteka watoto wadogo kwa kutaka kiasi kikubwa cha fedha huku wakitishia kuwadhulu
watoto hao iwapo hawatapewa kiasi cha fedha wanachohitaji.
“Hili jambo lisipokomeshwa hata wake zetu na sisi wanaume
tutatekwa kwa siku za mbeleni haya mambo yanaaanza kidogo kidogo kama
ilivyokuwa nchini Mexico”alisema Lema
Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Olkeryan,Safari
akizungumza katika mkutano huo alisema kwamba hadi sasa katika mtaa wake jumla
ya watoto watano tayari wameshatekwa na hawajulikani walipo.
Safari,alisema kwamba tukio la kutekwa mtoto wa kwanza
lilitokea mnamo Agosti 21 mwaka huu ambapo mwanafunzi wa shule ya Lucky
Vicent,Maureen David (6) alitekwa majira ya saa 12;30 jioni ikiwa ni muda mfupi
tu tangu alipotoka shuleni na kuwasili nyumbani.
Safari,alifafanua kwamba wazazi wa mtoto huyo mara baada ya
kufuatilia kwa kina kwa watoto aliokuwa anacheza nao waliwaambia ya kwamba
David alichukuliwa na kijana mmoja asiyefahamika na ndipo walipoamua kupeleka
taarifa hizo mbele ya jeshi la polisi.
“Wale watoto waliokuwa wakicheza na Maureen walipewa ujumbe
ulioandikwa kwenye karatasi waupeleke nyumbani kwao unaosomeka kwamba wazazi wanatakiwa watoe sh,4.5 milioni
ndipo watekaji watamwachia mtoto huyo”alisema Safari
Alisema kwamba mnamo Agosti 24 mwaka huu wazazi wa mtoto huyo
walikuta nguo alizovaa David zikiwa zimetupwa nje ya mlango wa nyumba
wanayoishi na ujumbe unaosomeka kwamba leo ndio siku ya mwisho na
wasipotekeleza maagizo hayo watammaliza mtoto wao na ndipo walipofanya
mawasiliano na watekaji hao na kisha kukubali kutoa kiasi cha sh,500,000
ambacho baadaye walikatazwa na polisi wasikitoe.
Mwenyekiti huyo alisema kwamba mnamo Agosti 26 majira ya saa
12.00 jioni kwa mara nyingine alitekwa mtoto mwingine aliyetambulika kwa jina
la Ikram Kassim(3) ambapo watekaji hao waliacha ujumbe wenye masharti ya namna
ya kumpata mtoto huyo.
Alisema kwamba katika ujumbe huo watekaji hao walionya endapo
wazazi watavunja masharti hayo wako tayari kumchinja jambo lililopelekea
kuwaogopesha wazazi wa Kassim na kutoa kiasi cha sh,300,000 lakini
hawakufanikiwa kurejeshewa mtoto huyo.
Aliwataja watoto wengine waliotekwa ni Ayoub Fred(3),Bakari
Ramadhan pamoja na mtoto mmoja mdogo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 3 ambaye
mpaka sasa hajafahamika jina lake anayedaiwa
kutekwa usiku wa kuamkia jana akiwa usingizini nyumbani kwao mtaa wa Olkeryan.
Wakati huo huo mwenyekiti huyo alisema kwamba hofu imetanda kwa wakazi mtaani kwake kwa kuwa
baadhi ya wazazi wanalazimika kuwapeleka shuleni na kuwarejesha majumbani watoto
kutokana na wasiwasi wa kutekwa huku watoto wengine wakipigwa marufuku kutocheza
mitaani na kuwalazimisha kushindwa nyumbani wakiwa wamefungiwa.
Mmoja wa wazazi wa watoto aliyetekwa aliyejitambulisha kwa
jina la Mama Kassim alisema kwamba mtoto wake alichukuliwa wakati akicheza na
wenzake nje ya nyumba mnamo Agosti 26 mwaka huu na mpaka leo hajulikani alipo.
Kamanda
wa polisi mkoa wa Arusha ,Charles Mkumbo amethibitisha
kutokea kwa matukio hayo ya utekeji na kueleza kuwa jeshi lake linaandaa
taarifa lakini mpaka jana alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi
alisema kwamba yuko kikaoni.