Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), kimemwandikia
barua Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, kumwelezea sababu za mgomo
wao na jinsi wanasheria wanavyonyanyaswa na kuuawa.
Mgomo huo wa siku mbili unatokana na shambulio la mabomu katika Ofisi ya Mawakili ya IMMMA.
Barua hiyo ya TLS iliyotiwa saini na Rais Tundu Lissu,
imesema mgomo wao wa siku mbili haumaanishi kupingana na Serikali au
kuwaadhibu wateja ila kuhamasisha umma kuhusu mazingira ya hatari
waliyopo wanasheria nchini.
Lissu alisema tukio hilo halikufanyika kwa bahati mbaya na
matukio kama hayo ya kuwasumbua wanasheria wasifanye kazi zao ipasavyo,
imekuwa sehemu ya maisha yao.
“Kwa mfano, Aprili 7, mwaka jana ofisi za Mwanasheria Said
Omar Shaaban ambaye kwa sasa ni Rais wa Chama Wanasheria wa Zanzibar
(ZLS), zilipigwa bomu na kuharibiwa, lakini hadi leo hakuna ripoti ya
uchunguzi wa polisi.
“Wanasheria pia wamefungwa kizuizini na wengine kukamatwa
wakiwa mahakamani wakitekeleza majukumu yao ya kitaaluma na wengine
wameuawa kikatili.
“Kwa mfano miaka michache iliyopita, wanasheria Profesa
Jwani Mwaikusa na Dk. Sengondo Mvungi, waliuawa baada ya kuvamiwa na
kupigwa na watu wasiojulikana.
“Machi mwaka juzi Wakili Philbert Gwagilo, alipotea katika
mazingira ya kutatanisha na hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kuhusu
kupotea kwake,” alisema Lissu katika barua hiyo.
Akizungumzia kuhusu wanasheria ambao hawatagoma, alisema
wanaotaka kwenda mahakamani waende kama wanaona wenzao kulipuliwa kwa
mabomu ni sawa, ila wakae wakijua hawako salama.
“Tunataka tuhakikishiwe usalama wetu, siku mbili hizi
tunataka wananchi nao wapaze sauti kuomba usalama wa wanasheria, au
wanataka tufe wangapi ili wajue tunahitaji ulinzi?” alihoji Lissu.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia