KATIKA
kuongeza ufanisi kwenye utendaji, Waziri wa Maliasili na Utalii,
Profesa Jumanne Maghembe amefanya mabadiliko ya baadhi ya watendaji
kwenye wizara na idara zilizo chini ya wizara hiyo.
Mabadiliko
hayo madogo yamegusa Chuo Cha Taifa cha Utalii, Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori (TAWA) na Idara ya Utalii kwenye makao makuu ya Wizara ya
Maliasili na Utalii.
Akitangaza
mabadiliko hayo mwishoni mwa wiki mjini Dodoma, Waziri Maghembe
alimtaja Deogratius Mdamu kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii
kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Zahoro Kimwaga TAWA kukaimu nafasi ya
Mkuu wa Shughuli za Utalii wa Picha.
Profesa
Maghembe alisema pia amemteua Phillip Chitaunga, kuwa Kaimu Mkurugenzi
Msaidizi wa Sehemu ya Maendeleo ya Utalii kwenye makao makuu ya wizara,
ili kujaza nafasi iliyoachwa na Uzeeli Kiangi aliyestaafu utumishi kwa
mujibu wa sheria.
"Kwenye
Chuo chetu cha Taifa Utalii, ninamteua Dk. Shogo Mlozi kuwa Kaimu Mkuu
wa Chuo ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Utalii
na Ukarimu kwenye Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT)," alisema.
Pamoja
na hao, Waziri huyo alimtaja Stephen Madenge kuwa Kaimu Mkurugenzi wa
Mafunzo wa Chuo cha Taifa cha Utalii ambaye anabadilishana nafasi na
Martina Hagwet, anayekwenda kushika wadhifa wa Kaimu Meneja wa Chuo cha
Taifa cha Utalii, Kampasi ya Temeke.
Aidha,
Waziri Maghembe alisema kwenye Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori,
amemteua Dk. James Wakibara kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu nafasi iliyoachwa
wazi na Martin Loibooki anayerejeshwa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa
(TANAPA), kupangiwa kazi nyingine.
Uteuzi
zaidi kwenye mamlaka hiyo, umefanywa kwa Imani Nkuwi, kuwa Kaimu
Mkurugenzi wa Biashara na Utalii kuchukua nafasi ya Mzamilu Kaita,
anayerejeshwa Wizarani kupangiwa kazi nyingine.
"Wa
mwisho kwenye mabadiliko haya ni Mabula Misungwi, tunayemteua kuwa Kaimu
Mkurugenzi wa Himasheria yaani Protection ili kuchukua nafasi ya
Faustine Masalu atakayepangiwa kazi nyingine hapo baadaye," alisema.
Mabadiliko
hayo alisema ni ya kawaida na kwamba utekelezaji wake unaanza mara moja
ambapo Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi
aliyathibitisha kwa barua rasmi iliyoandikwa Agosti 3, mwaka huu.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia