Jeshi la Polisi Mkoani hapa limefanikiwa kumkamata mtu mmoja
aitwaye Ismail Swalehe Sang’wa (20) ambaye ni mwenyeji wa kijiji cha Sepuka
wilayani Ikungi katika Mkoa wa Singida kwa tuhuma za kumuua Afisa wa Intelijensia wa TANAPA aitwaye Emily Kisamo (52).
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake asubuhi ya
leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Liberatus
Sabas alisema tukio hilo la mauaji ya Afisa huyo wa TANAPA lilitokea tarehe
18.12.2015 muda kati ya saa 2:30 asubuhi hadi saa 4:00 asubuhi mtaa uitwao
Corridor Area Uzunguni jijini hapa.
Kamanda Sabas alisema kwamba, siku ya tukio hilo marehemu
alikuwa nyumbani kwake sebuleni akiwa anakunywa uji ndipo mtuhumiwa ambaye ni
mfanyakazi wake wa ndani na alimvizia na kumkata shingo na kitu kinachoaminika
kuwa ni panga na kisha kuchukua mwili wake na kuuweka kwenye gari la marehemu
aina ya Nissan Mazda lenye namba za usajili T. 435 CSY.
“Baada ya kuuweka mwili wa marehemu kwenye buti alilisafisha
gari hilo kwa nje na kisha kuliendesha mpaka eneo la kikwakwaru “B” kata ya
Lemara ambapo alilitelekeza hapo na kisha yeye kuondoka”. Alifafanua Kamanda
Sabas.
“Mara baada ya gari hilo kukaa mpaka saa 2:00 usiku ndipo
baadhi ya wananchi wa eneo hilo walitoa taarifa kwetu ambapo askari wa doria
walikwenda na kulichukua gari hilo kwa kulivuta mpaka kituoni. Kwa kuwa mke wa
marehemu aitwaye Caroline Lukumay (38) alikuwa anamtafuta mume wake kwa njia ya
simu bila mafanikio ndipo alipoamua kuja kituoni kutoa taarifa ambapo
tulimuonyesha gari lililotelekezwa ambalo alillitambua mara moja”. Alisema
Kamanda Sabas.
Aliongeza kwa kusema kwamba askari walimuomba mke wa marehemu
funguo za akiba za gari hilo ambapo baada ya kulifungua ndipo walipouona mwili
wa marehemu kwenye buti akiwa na vitu mbalimbali kama vile simu mbili aina ya
Sony na Panasonic, pesa taslimu Tsh 300,000, Laptop aina ya Asus na kadi za
benki tofauti tofauti.
Mara baada ya mtuhumiwa huyo kukamatwa alikiri kuhusika na
mauaji hayo na kusema siku hiyo walikuwa wawili tu yaani yeye na mrehemu na
alifanya hivyo kwa kuwa alikuwa na tamaa za fedha alizokuwa nazo marehemu ndani
ya nyumba hiyo kiasi cha Tsh. Mil.5.
Upekuzi zaidi wa Jeshi la Polisi ulibaini kuwepo kwa fedha
taslimu Tsh. 4,294,000, simu tatu aina ya Sumsang na vocha za mtandao wa
vodacom za sh. Elfu tano tano zenye thamani ya Tsh. 70,000 ambapo vyote
vilifukiwa kwenye banda la kuku.
Mbali na vitu hivyo pia mtuhumiwa Ismail Swalehe Sang’wa
aliweza kuonyesha panga lenye damu ambalo alilihifadhi stoo pamoja na taulo nne
kubwa, kitambaa cha mezani na suruali yake ambazo zilikuwa na damu na
alizitumia yeye mwenyewe kupigia deki sebuleni baada ya tukio na kisha
kuzificha kwenye migomba karibu na mabanda ya kuku.
Kamanda Sabas alimalizia kwa kusema kwamba Jeshi hilo
linawashikilia watuhumiwa watatu wengine mbali na Ismail Swalehe Sang’wa
akiwemo mke wa marehemu, rafiki wa mke wa marehemu ambaye ni mwanamke na dereva
wa nyumbani wa marehemu kwa mahojiano
zaidi.
Pichani
chini gari aina ya Nissan Mazda lenye namba za usajili T. 435 CSY
lililokutwa na mwili wa marehemu Emily Kisamo ambaye ni Afisa wa
Intelejensia TANAPA uliohifadhiwa kwenye buti mara baada ya kuuawa na
Mfanyakazi wake wa ndani.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia