Ticker

6/recent/ticker-posts

WATAKIWA KUTOWAACHIA WATOTO WAO MITANDAO

Wanafunzi wa chekechea wa shule ya New Light ya Mji mdogo wa Mireani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakiwa kwenye mahafali
ya kujiunga na darasa la kwanza kwenye shule hiyo
Na Woinde Shizza 
WAZAZI na walezi nchini wametakiwa kutowaachia huru watoto wao kujihusisha na mitandao ya kijamii, kwani baadhi ya mitandao hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa kubadili maadili yao na kusababisha wawe na tabia mbaya.

Meneja wa shule ya msingi New Light ya mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Benson Mboleka aliyasema hayo juzi kwenye mahafali ya wanafunzi wa chekechea watakaojiunga na darasa la kwanza mwakani.


Mboleka alisema watoto wengi huaribika kitabia pindi wanapojiingiza kutazama mitandao ya kijamii ikiwemo televisheni, hivyo wazazi wanapaswa kuwakataza watoto ambao wanajiingiza kwa kasi kutazama mitandao hiyo isiyo na maadili.

“Mitandao ya kijamii ikitumika vizuri siyo mibaya kwani watu wengi hupata habari nyingi kupitia mitandao hiyo, lakini watoto wengi huaribika kwa kutazama mitandao yenye malengo mabaya na televisheni,” alisema Mboleka.

Pia, alisema shule hiyo yenye watoto 417 kati ya shule 75 wilayani humo imeshika nafasi ya saba kwa kufaulisha wanaojiunga na elimu ya sekondari kwani wanafunzi wote 34 wamefaulu mtihani wa kuhitimu darasa la saba.

“Tuna ujasiri na tunajiamini kutamka kuwa tumeshika nafasi ya saba kwa ufaulu kwani kile tulichowekeza kwa wanafunzi hao ndicho walichokipata na mwanafunzi akitoka hapa anapata maendeleo anapoenda,” alisema Mboleka.

Mwalimu mkuu wa New Light, Kanuti Dimoso aliwashukuru wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule hiyo kwa imani waliyonayo hadi kuwapeleka watoto wao wakasomeshwe hapo ila akaomba ushirikiano kwao ili waendelee vyema.

“Tunazidi kupiga hatua kwani wanafunzi wote wa mwaka huu waliokwenda kufanya mtihani wa kuingia kidato cha kwanza kwenye shule za Tengeru Boys, Star High school, Faraja na St Margareth pia walifaulu vizuri,” alisema Dimoso.



Post a Comment

0 Comments