Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Lucas Mweri
akisoma mapendekezo mbalimbali kwenye kikao cha baraza la madiwani
kilichofanyika juzi (kushoto) ni Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Jackson Sipitieck.
Na Woinde Shizza,Simanjiro
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara Mahmoud Kambona ametoa wiki moja kwa wajumbe 12 wa Serikali ya Kijiji cha Kambi ya Chokaa waliosusa kutumikia nafasi hiyo kurejea ofisini au uchaguzi mwingine ufanyike.
Inadaiwa kuwa wajumbe hao
walisusa kufanya kazi wakipinga kuchaguliwa Mwenyekiti Mbuki Mollel badala ya
Joshua Kuney, hivyo shughuli za utawala kwenye kijiji hicho zinashindwa
kufanyika kutokana na kutokuwepo uongozi.
Kambona alitoa agizo hilo
juzi mbele ya baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo kwani michango na
huduma za kijamii hazifanyiki na kiongozi aliyepo ni mtendaji wa kijiji pekee
tangu mwaka juzi uchaguzi ulipofanyika.
Alisema anawapa muda wa
wiki moja viongozi hao warudi ofisini na endapo hawatakubaliana na hali hiyo
uchaguzi ufanyike upya kujaza nafasi hizo il ishughuli za kiutawala wa kijiji
hicho ziendelee kwa manufaa ya wananchi.
Kwa upande wake, mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Lucas Mweri alibainisha vyanzo vya
mapato vinavyotarajiwa kukusanywa na halmashauri ambavyo awali vilikuwa
vinakusanywa na vijiji.
“Vyanzo vya ushuru wa
mchanga, kuni kavu na samaki wakavu, ambavyo awali vilikuwa vinakusanywa na
vijiji, hivi sasa vitakusanywa na halmashauri kisha itatoa fedha kwa ajili ya
miradi ya maendeleo ya vijiji husika,” alisema Mweri.
Mwenyekiti wa halmashauri
ya wilaya hiyo Jackson Sipitieck, alisema makusanyo na ushuru unapaswa kufanywa
na halmashauri, kisha inarudisha kwa jamii kutokana na kufanikisha miradi
mbalimbali ya maendeleo.
“Huko vijijini ndipo kunaliwa
fedha za ushuru na michango mbalimbali, hivyo halmashauri itakusanya na
kurudisha kwa kujenga shule, barabara, zahanati na kuibua miradi mingine ya
maendeleo kama inavyofanya,” alisema Sipitieck.