Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameivunja Bodi
ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kumsimamisha kazi
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Ally Yahaya Simba (pichani)
kutokana na kutosimamia ipasavyo Mkataba wa utekelezaji wa mfumo wa
usimamizi wa mawasiliano ya simu (TTMS), na kusababisha nchi kupoteza
mapato ya takriban shilingi bilioni 400 kwa mwaka.
Rais
Magufuli amechukua hatua hiyo leo tarehe 26 Aprili, 2016 Ikulu Jijini
Dar es salaam baada ya kufanya kikao cha kazi kati yake na viongozi na
wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya
fedha na Mipango na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Tarehe 22
Machi, 2013 Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) iliingia mkataba na
kampuni ya SGS juu ya uwekaji, uendeshaji na uhamishaji wa mapato ya
simu ambapo kampuni hiyo ilipaswa kutekeleza vipengele vitano lakini
mpaka sasa kampuni ya SGS haijaanza kutekeleza kipengele kidogo
kinachohusiana na uthibiti wa mapato ya simu za ndani (Offnet), hali
ambayo imesababisha serikali kukosa mapato yanayokadiriwa kuwa shilingi
bilioni 400 kwa mwaka.
Pamoja na
kuivunja bodi ya TCRA inayoongozwa na Profesa Haji Semboja na
Kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Ally Yahaya Simba, Rais
Magufuli pia amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi
Profesa Makame Mbarawa Mnyaa kumteua Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
hiyo mara moja.
Aidha,
Rais Magufuli amewataka Waziri Prof. Mbarawa, Katibu Mkuu na Naibu
Katibu katika wizara hiyo kuchukua hatua mara moja ili mfumo wa
ukusanyaji wa mapato ya simu kwa simu za ndani (Offnet) uanze kufanya
kazi, na nchi ipate mapato yanayostahili kukusanywa.
Waziri
hakikisha unachukua hatua mara moja, nataka tukusanye mapato yote ya
serikali yanayostahili na sitasita kuchukua hatua dhidi ya yoyote
atakayekwamisha jambo hili Amesisitiza Rais Magufuli.