Katika kuhakikisha watu wanaoishi na UKIMWI wanaishi kwa furaha bila kunyanyapaliwa na watu wanaowazunguka, jamii imetakiwa kuwa na mtazamo tofauti kwa watu wanaoishi na ugonjwa huo.
Hayo yalisemwa na mke wa mtoto wa mfalme wa Norway, Mette-Marit ambaye pia ni balozi kimataifa wa Shirika la Umoja la kupambana na HIV na UKIMWI (UNAIDS) wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kazi anazozifanya kwa UNAIDS kama balozi ambaye anazunguka maeneo mbalimbali duniani ili kuelimisha jamii kuhusu UKIMWI.
Mette-Marrit alisema kuwa watu wenye UKIMWI ni kama watu wengine hivyo wana haki ya kupata huduma bila kunyanyapaliwa ili waweze kuishi kwa uhuru kama watu wengine na ili kufanikisha hilo ni wajibu wa kila mtu kuwasaidia waathirika.
“Watu kuwa na UKIMWI sio mwisho wa maisha inatakiwa kwanza jami kuwa na mtazamo tofauti na inatakiwa kila mtu kusaidia mapambano ya UKIMWI sio jambo la mtu mmoja mmoja,” alisema Mette-Marit.
Balozi wa Kimataifa wa UNAIDS, Mette-Marit akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kazi anazofanya kama balozi wa UNAIDS kwa kipindi cha miaka 10 tangu aanze kazi hiyo. (Picha zote na Rabi Humeog)
Nae Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Dkt. Fatma Mrisho alisema Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ili kupambana na UKIMWI lakini pia ili kufanikisha mapambano hayo wanahitaji kushirikiana na taasisi ambazo zitawasaidia katika mapambano hayo.
Lakini pia Dkt. Mrisho amezitaka serikali za mitaa kuacha kusubiri mpaka serikali imepeleke pesa ndiyo wawasaidie watu wanaoishi na UKIMWI na hivyo waweke utaratibu wa kutumia sehemu ya mapato yao ili kusaidia mapambano hayo.
“Serikali haijalala katika mapambano tunahitaji kushirikiana na taasisi ambazo zinatusaidia kupunguza maambukizi mapya na tunaona Mette-Marit amekuwa akifanya jambo zuri anazunguka sehemu nyingi ili kusaidia kupunguza maamukizi mapya ya UKIMWI,” alisema Dkt. Mrisho.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Dkt. Fatma Mrisho akizungumzia kuhusu juhudi zinazofanywa na serikali katika mapambano ya UKIMWI.
Mkurugenzi mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na Ukimwi, UNAIDS nchini Tanzania, Warren Naamara akizungumzia ugonjwa wa UKIMWI.