BODI ya Sukari Tanzania imewataka wafanyabiashara wote nchini
kuheshimu agizo la Serikali na kusambaza bidhaa hiyo kwa wananchi pasipo
kuihodhi.
Kauli hiyo imetolewa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya
Sukari Tanzania, Henry Semwanza, alipoulizwa na gazeti hili kuhusu
baadhi ya wasambazaji wa sukari kuonekana hawatekelezi agizo la Serikali
kwa kufuata bei elekezi ya Sh 1,800 kwa kilo.
MTANZANIA lilitembelea maduka mbalimbali Dar es Salaam na kubaini
kuwa bado wafanyabiashara wanaendelea kuuza sukari kwa bei ya Sh 2,000
hadi 2,400 kwa kilo moja.
Semwanza alisema kila mfanyabiashara anapaswa kufuata bei elekezi
iliyotolewa na Serikali ya Sh 1,800 kwa kilo moja na atakayebainika
kukaidi amri hiyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
“Bodi ya Sukari Tanzania ilipokutana na waandishi wa habari Machi
mwaka huu, ilitoa ufafanuzi kuwa sukari ipo ya kutosha kwa matumizi ya
ndani na tumewataka wasambazaji wote watumie bei hiyo elekezi
iliyotolewa na Serikali.
“Bodi kwa kushirikiana na sekretarieti za mikoa, inaendelea
kufuatilia utekelezaji wa agizo la Serikali la bei elekezi ya Sh 1,800
kwa kilo moja,” alisema Semwanza.
Alisema mahitaji ya sukari kwa mwaka ni karibu tani 420,000 na hadi
sasa viwanda vya ndani vimezalisha tani 293,724.94 kati ya 295,070.00
zilizotarajiwa kuzalishwa katika msimu wa mwaka 2015/16.
Semwanza alisema mamlaka za dola hazitasita kumchukulia hatua stahiki
za kisheria mfanyabiashara yeyote atakayebainika kukiuka agizo hilo la
Serikali kwa kutokuuza sukari kwa bei elekezi.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia