MKUU WA WILAYA AIFUNGIA SHULE

 
 mkuu wa wilaya ya Babati Crispin Meela
Na Woinde Shizza,Manyara
Mkuu wa Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, Crispin Meela ameifunga shule
ya msingi Matufa kwa muda usiojulikana baada ya kutitia kwa matundu ya
vyoo vya wanafunzi na walimu kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na
mvua zinazonyesha.
Akizungumza  baada ya kuitembelea shule hiyo, Meela alisema kutokana
na matundu ya 24 ya vyoo vya shule hiyo kuharibika inabidi shule hiyo
ifungwe kwani hakuna vyoo vingine vya kutumiwa kwa wanafunzi na
walimu.
Hata hivyo, kaya 64 zilizokuwa zinaishi kwenye shule hiyo ya Matufa
kwa kukosa makazi baada ya nyumba zao kusombwa na mafuriko
yaliyosababishwa na mvua zilizonyesha siku mbili hivi sasa wamepatiwa
hifadhi kwa kuwekwa kambini.
Alisema  kutokana na maafa hayo hana budi kuifunga shule hiyo kwa muda
usiojulikana na anatarajia watahakikisha tatizo hilo linapatiwa
ufumbuzi kwa muda mfupi kupitia ushirikiano wa viongozi wa wilaya na
mkoa huo.
“Namuagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Babati
vijijini Dominick Kweka, kuhakikisha shule hiyo inajengewa vyoo mara
baada ya wiki moja kupita ili wanafunzi waweze kuendelea na masomo
yao,” alisema Meela.
Kwa upande wake, mbunge wa jimbo la Babati vijijini Vrajlal Jitu Soni
aliwapa pole wakazi wa vijiji vya Magugu na Matufa vilivyopo kwenye
tarafa ya Mbugwe ambao wameathirika kutokana na mafuriko hayo.
Jitu Soni alisema hivi sasa wanafanya tathmini ya mafuriko hayo ili
kamati ya maafa kupitia ofisi ya Waziri Mkuu waweze kuwapatia msaada
wananchi hao ambao nyumba na mazao yao yamechukuliwa na mafuriko hayo.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post