CCM:NIKWELI LOWASA ALITUTIKISA


Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, makada wa CCM walirusha kila neno baya na la kejeli kwa Edward Lowassa, lakini moyoni walikuwa wanajua kuwa mgombea huyo wa urais kwa tiketi ya Chadema alikuwa akiwasumbua, Mwananchi imeelezwa.

Lowassa, Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, alijiondoa CCM baada ya kumalizika kwa mchakato wa kumpata mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, jina lake likiwa limekatwa kabla ya kufikishwa kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa na Mkutano Mkuu, vyombo ambavyo hufanya uamuzi kwa kupiga kura.

Siku chache baadaye alijiunga na Chadema, ambayo iliingia kwenye Uchaguzi Mkuu chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) uliokuwa pia na vyama vya CYF, NCCR Mageuzi na NLD vilivyokubaliana kusimamisha mgombea mmoja wa urais, ubunge na udiwani. Hakuondoka peke yake. Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye alimfuata pamoja na mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale-Mwiru, mawaziri wa zamani, wenyeviti wa mikoa, wabunge na madiwani na kufanya Uchaguzi Mkuu kuwa na ushindani wa aina yake.

“Ukweli ni kwamba kuondoka kwa Lowassa kulitutikisa (sisi) CCM,” alisema Abdallah Bulembo aliyekuwa meneja wa kampeni wa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli.

Hata hivyo, alidai kuwa athari za mtikisiko huo hazikuonekana kwa sababu chama hicho tawala kilijivunia ubora wa mgombea wake, utekelezaji wa ilani yake na kusimamia ukweli katika majukwaa ya siasa. Bulembo alisema hayo alipofanya mazungumzo maalumu na gazeti hili juzi jijini Dar es Salaam.

“Nasema CCM ilitikisika kwa kuwa mbali na Lowassa tuliondokewa na mwenyeviti watatu wa mikoa; Shinyanga, Singida na Arusha,” alisema Bulembo.

“Katika Idara ya Wazazi, mimi (mwenyekiti) niliondokewa na wajumbe wa baraza la mikoa ya Pwani, Njombe, Kagera na Rukwa. Lakini tukapata replacement (mbadala) na kusonga mbele.”

Kwa mujibu wa Bulembo, pamoja na kuondokewa na viongozi hao ambao alisema ni nguzo muhimu ya chama, bado CCM iliweza kushinda viti tisa vya ubunge kati ya 10 mkoani Singida, viti vyote vya ubunge katika Mkoa wa Shinyanga na kiti kimoja katika Mkoa wa Arusha.

Maneno ya Bulembo yanaweza kuthibitishwa na jinsi kampeni za CCM zilivyojaa hotuba za kumrushia makombora mbunge huyo wa zamani wa Monduli karibu katika kila mkutano wa kampeni.

Wakati fulani akiwa mkoani Kagera, Bulembo aliwahi kuwatuhumu wana-CCM kuwa wamekuwa ndumilakuwili kwa kukiunga mkono chama hicho wakati wa mchana na baadaye kwenda Ukawa.

Bulembo alisema kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Bukoba Vijijini, ziara ya Lowassa mkoani Kagera iliratibiwa na wana-CCM na kwamba anawafahamu.

“Msidhani hatuwafahamu. Mikakati yote na jinsi mnavyowafadhili Ukawa na Lowassa tunafahamu. Tena tunawafahamu kwa majina. nasema ole wenu. Msipoondoka wenyewe, tutawafukuza Dk Magufuli atakaposhinda uchaguzi,” alisema Bulembo wakati huo.

“Tunawajua mnaomng’ang’ania Lowassa. Lakini nawahakikishia kuwa mtalia baada ya uchaguzi wa mwaka huu. Mnajifanya CCM, lakini mnafadhili Ukawa. Mwisho wenu unakuja.”

Kabla ya mkutano huo, Dk Magufuli pia alifichua mipango ya wanachama ambao aliwaita wanakuwa upande wa CCM mchana na usiku wanahamia Ukawa wakati alipohutubia kwenye uwanja wa Zimbiilo wilayani Muleba.

“Kuna baadhi ya wana-CCM wanatujuhumu sana, wengine nawajua hata majina yao bahati nzuri huwa sisemi uongo bali ukweli. Kuna huyu Gasper mchana tunakuwa naye CCM lakini usiku anaungana na wapinzani,” alisema na kuacha mshangao kwenye mkutano huo. Kukiwa bado na mshangao, Bulembo alisimama na kwenda kumnong’oneza kitu Magufuli na baadaye mgombea huyo wa CCM akarekebisha kauli yake.

“Msaliti ni Gasper Anthony wala si Gasper Kileo,” alisema akimzungumzia mwanachama ambaye alijionyesha waziwazi kumuunga mkono Lowassa wakati wa mchakato wa kutafuta mgombea urais ndani ya CCM.

Siri ya ushindi
Pamoja na upinzani huo ambao CCM ilikumbana nao kutoka kwa Lowassa, Bulembo alisema siri ya ushindi wa chama hicho kikongwe kwenye uchaguzi uliopita ni pamoja na kukubalika kwa Dk Magufuli.

“Tulimteua mtu anayekubalika. Magufuli alijiuza mwenyewe na alikuwa mchapakazi. Tulikuwa tunafanya kati ya mikutano saba na kumi isiyo rasmi kila siku,” alisema Bulembo.

Alipoulizwa kingetokea nini endapo CCM isingemteua Dk Magufuli kugombea urais, alijibu “bado tungeshinda, lakini ingetulazimu kufanya kazi ya ziada”.

Katika uchaguzi huo, Dk Magufuli alipata kura milioni 8.8 na Lowassa alipata kura milioni 6.07, idadi ambayo ni zaidi ya mara mbili ambazo wapinzani wamekuwa wakipata kwenye chaguzi zilizopita. Bulembo pia, alieleza kuwa CCM ilijipanga vizuri ikitumia makada na viongozi wake waliotawanyika kuanzia ngazi ya tawi hadi taifa.

“Chama kilikuwa baba na kilitegemea taasisi zake zote. Katika ngazi ya chama kulikuwa na timu ya watu 32 na mimi katika idara yangu ya wazazi niliteua watu 34, vilevile katika idara nyingine, ingawa siwezi kukumbuka idadi ya watu walioteuliwa kuongoza jahazi,” alisema.

Alisema mbali na timu hiyo iliyokuwa ikiandaa mazingira ya kampeni za mgombea urais, chama hicho kilitumia uongozi wake katika idara zote; vijana, wazazi na wanawake pamoja na kamati zake za uchumi na siasa kufanya kazi hiyo usiku na mchana.
 

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post