Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul
Makonda (kulia), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari katika
Ukumbi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
Dar es Salaam leo asubuhi wakati akitoa mwito kwa wananchi hasa wa Wilaya
ya Kinondoni na maeneo mengine ya jiji la Dar es Salaam kujitokeza kwa
wingi kupimwa maradhi ya moyo bure katiza zoezi litakalofanywa na madaktari
kutoka taasisi hiyo litakalofanyika viwanja vya leaders kesho kutwa January
23, 2015. Kushoto ni Meneja wa Taasisi hiyo, Salome Kassanga na Kaimu
Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Profesa Mohamed Janabi.
Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Profesa
Mohamed Janabi (kushoto), akizungumza katika mkutano huo. Kulia ni Mkuu wa
Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.
Meneja wa Taasisi hiyo, Salome Kassanga
(kushoto), akimuelekeza jambo DC Makonda. Katikati ni Mkuu wa Idara ya
Magonjwa ya Moyo wa Taasisi hiyo, Dk.Peter Kisenge.
Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali
wakichukua taarifa hiyo.
Na Dotto Mwaibale
MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda
kesho kutwa anatarajia kuongoza wananchi wa wilaya yake na wakazi wengine
wa jiji la Dar es Salaam katika upimaji wa magonjwa ya moyo utakaofanywa
bure na madaktari kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete
(JKCI), katika viwanja vya Leaders Club.
Upimaji huo utatoa fursa ya kubaini wagonjwa wa wilaya hiyo kwa kuwa wananchi wengi hawajui magonjwa ya moyo yanaweza pia kusababishwa na shinikizo la damu na ni chanzo kikubwa cha magonjwa ya macho,upungufu wa nguvu za kiume, kiharusi, figo na kutokuzaa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo
asubuhi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Profesa Mohamed Janabi
alisema kutokana na umuhimu wa wananchi kujua afya zao na kupatiwa matibabu
mapema kesho wataungana na Makonda katika kuwapatia vipimo wakazi wa
kinondoni.
Alisema ugonjwa wa moyo ni hatari na
asilimia kubwa ya wagonjwa hao wanatembea na kufanya kazi zao kwakuwa
ugonjwa huo hauna dalili hivyo haja ya kila mmoja kupima na kujua afya yake
ni muhimu.
“Pia wengi wanaougua shinikizo la damu
hawajua wanaweza kuwa na magonjwa ya moyo na kujikuta wakisababisha
kuua figo,macho,nguvu za kiume,kuugua kiharusi na kukosa watoto upimaji huu
ni hatua nzuri kwa wananchi wa kinondoni hivyo tumeridhia kuwapima na
kuwapatia matibabu bure,”alisema.
Alisema taasisi hiyo itakuwa kamili katika
kila sekta kesho kutwa viwanja vya Leaders Club ili wananchi wenye magonjwa
yanayoshabihiana na moyo waweze kupewa tiba katika hospitali za wilaya hiyo
ikiwemo Mwananyamala na wale walioathirika na ugonjwa wa moyo waweze
kutibiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Profesa Janabi alisema pia watahakikisha
madaktari wa ushauri wanatoa elimu ipasavyo juu ya kuepuka ugonjwa wa moyo
na shinikizo la damu ambao hauna tiba na jinsi ya kuzingatia lishe.
“Ni muhimu kujua ongezeko la matumizi ya
vyakula vya wanga kwa wingi pia ni hatari katika kuongeza uzito hivyo
kusababisha shinikizo la damu,”alisema
Kwa upande wake Makonda aliwataka wananchi
kuelewa kuwa ugonjwa wa moyo ni hatari na matibabu yake ni gharama hasa kwa
wale wanaosafirishwa nje ya nchi hivyo ni vyema kuitumia fursa hiyo
kesho.
Alisema serikali imeona haja ya kuboresha
afya za wananchi ili kukuza uchumi na hatua hiyo ya kusaidia upimaji wa
bure itapunguza hatari ya ugonjwa huo kwa watu wengi wanaopoteza maisha
kila siku.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia