MBUNGE WA JIMBO LA NYAMAGANA KUKOMALIA UJENZI WA MAEGESHO JJINI MWANZA

Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Mkoani Mwanza (CCM) Stanslaus Mabula.
Na:George Binagi-GB Pazzo @BMG
Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Mkoani Mwanza Stanslaus Mabula (CCM, ameahidi kushughulikia suala la ujenzi wa maegesho ya magari makubwa ya mizigo nje ya jiji la Mwanza ili kuzuia magari hayo kuingia katikati ya jiji.

Akizungumza ofisini kwake hii leo, Mabula amebainisha kuwa upo mpango wa kujenga maegesho hayo katika maeneo yaliyo nje ya Jiji la Mwanza, hatua ambayo itasaidia magari hayo kutoingia katikati ya Jiji na hivyo kuondoa malalamiko yaliyopo kutoka kwa madereva wa magari madogo ya mizigo wanaolalamikia uingiaji wa magari makubwa ya mizigo katikati ya jiji.

Ameyataja maeneo yanayotarajiwa kujengwa maegesho hao kuwa ni Buhongwa pamoja na Igoma na kwamba baada ya ujenzi wake kukamilika, magari yote makubwa ya mizigo hayataruhusiwa kuingia katikati ya Jiji.

Mabula ambae alikuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza katika uongozi uliomalizika mwaka jana, amebainisha kuwa utekelezaji wa ujenzi wa maegesho hayo unatarajiwa kufanyika kwa uharaka zaidi ambapo amewahimiza wawekezaji mbalimbali kujitokeza ili kushirikiana na halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa ajili ya kufanikisha ujenzi huo.

Suala la magari makubwa kuingia katikati ya Jiji la Mwanza huku yakiwa na mizigo, linalalamikiwa na madereva wa magari madogo ya mizigo kwa kile wanachoeleza kuwa wanaingiliwa katika shughuli ambazo wao wangezifanya na hivyo kujiingia kipato ambapo wameiomba halmashauri ya Jiji la Mwanza kutoruhusu magari hayo kuingia katikati ya Jiji.

Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Mkoani Mwanza (CCM) Stanslaus Mabula.
Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Mkoani Mwanza (CCM) Stanslaus Mabula akiongea na wanahabari ofisini kwake.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post