Halmashauri ya Arusha wilaya ya Arumeru, imejipanga kutokomeza
ukatili dhidi ya wanawake na watoto unaotokana na mila na desturi potofu
zinazoendelezwa ndani ya jamii.
Mikakati hiyo imeanza kwa kuunda kamati ya ulinzi na usalama wa
wanawake na mtoto ngazi ya halmashauri, kufuatia mwongozo wa serikali wa
mpango wa kitaifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo, kaimu mkurugenzi
halmashauri ya Arusha, ndugu Paulus Kessy, amesema kuwa halmashauri
imeunda kamati hii kwa lengo la kuhakikisha ulinzi na usalama wa
wanawake na watoto kwa kutokomeza mila na desturi zinazowakandamiza.
Ameongeza kuwa suala la mila na destruri lina changamoto nyingi,
hivyo kamati hii ina kazi kubwa ya kuelemisha jamii juu ya athari ya
mila hizo kandamizi kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria za serikali.
"Kamati inatakiwa kuwa na uhusiano chanya kati ya wazazi, walezi,
watoto na jamii nzima, uhusiano wenye lengo la kuelimishana na kukemea
mila potofu, uhusiano utakaowezesha halmashauri kufikia lengo la
mwanamke na mtoto kupata haki " amesema Kaimu mkurugenzi
Aidha kaimu mkurugenzi Kessy ameweka wazi mikakati itakayotekelezwa
na halmashauri hiyo ni pamoja na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na
watoto kwa asilimia 50% ifikapo mwaka 2025 kwa jamii kujengewa uwezo wa
kusimamia haki za wanawake na watoto.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Arusha Theresia Costantine,
ameainisha majukumu ya kamati hiyo ni pamoja na kuhamasisha na
kuelimisha jamii kuhusu kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto
pamoja na kushiriki katika utoaji huduma kwa makundi yaliyo katika
mazingira hatarishi.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa mpango kazi wa taifa wa kutokomeza
ukatili dhidi ya wanawake na watoto utatekelezeka, endapo kamati
itafanyakazi kwa ushirikiano kwa kumuweke na mtoto kwanza.
Hata hivyo Sumaiya Abdul (12) , mwenyekiti wa Baraza la watoto
halmashauri ya Arusha ameonyesha kufurahishwa na uundaji wa baraza hilo
kuongeza kuwa anaamini kupitia kamati hii watoto watapata haki zao za
msingi.