Uchimbaji wa visima viwili vya maji unaendelea kwa kasi katika
shamba la mbegu Ilkiushini kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji
unaotekelezwa na shirika la WaterAid jambo linaloashiri upatikani wa
maji kwa wakazi wapatoa 50,000.
Mradi huo wa maji unatekelezwa kwenye vijiji vya Olkokola na
Lengijave na vitongoji vya Olmotonyi, Ekenywa na Seuri vya Mamlaka ya
Mji Mdogo Ngaramtoni kwa gharama ya shilingi bilioni 4.5 kwa ufadhili wa
serikali ya Uingereza kupitia Idara ya Maendeleo ya Kimataifa 'DFID'.
Wakati huo huo serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji
imeongeza kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya kuongeza nguvu ya
ujenzi wa mradi huo ili kWakatiuwafikia wananchi wengi zaidi na
kuwezesha kutumia chanzo cha maji cha Emutoto kilichopo kwenye msitu
ndani ya hifadhi ya mlima Meru licha ya mradi huo kutumia vyanzo hivyo
viwili vya kuchimbwa.
Mradi huo unategemea kukamilika mwishoni mwa mwaka huu 2018 na
kuhudumia takribani wakazi 50,000 ambao watapata maji ndani ya mita 400
na kutekeleza mpango wa serikali ya awamu ya tano wa kuhakikisha
asilimia 90% ya wakazi wa vijiji kupata maji safi na salama ifikapo
mwaka 2025.
Hata hivyo mradi huo utaambatana na teknolojia mpya ya kuchangia
gharama za maji kwa kutumia mfumo wa kulipa kabla ya kutumia, mfumo
unaojulikana kama eWaterpay utakaowekwa na shirika la eWater - Tanzania.