Masikitiko hayo yamekuja baada ya kutembelea ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi ya walimu, vilivyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi kwa lengo la kuanzisha shule mpya ya Msingi Olkujunderet kuwezesha watoto kupata elimu karibu na maeneo wanayoishi.
Akizungumza mbele ya waziri Jafo, Diwani wa kata ya Olkokola, mheshimiwa Kalanga Laiza, amesema kuwa wamelazika kuanza ujenzi wa shule ya msingi katika eneo hilo, baada ya kuona watoto wanateseka kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
Diwani Kalanga amefafanua kuwa, kijiji hicho ni kipya na baada ya kugawanya kikajikuta hakina shule wala ofisi ya kijiji, hivyo wananchi kuamua kununua eneo la kujenga ofisi na shule.
Ameongeza kuwa wananchi wamechanga fedha na kununua eneo la Ekari 10, na kuanza kujenga vyumba viwili vya madarasa ili waanze kwanza kusoma watoto wenye umri mdogo, huku wakiendelea kutafuta nguvu za kumalizia mdarasa mengine na kufikia madarasa nane kama sheria ya kuanzisha shule inayotaka.
" Watoto wanapata shida sana, hasa wakati huu wa mvua ambapo makorongo yanajaa maji, na kusababisha kushindwa kuhudhuria masomo kwa kuepusha madhara yanayoweza kuwapata kutokana na mvua" amesema Kalanga
Hata hivyo Waziri Jafo, amemuagiza mkurugenzi mtendaji halmashauri ya Arusha, kutafuta fedha haraka kumalizia ujenzi huo na kuahidi serikali pia itaweka mikakati ya kuhakikisha miundo mbinu ya shule hiyo inakamilika na ifikapo Januari 2019, watoto waanze kusoma shuleni hapo.
Ameongeza kuwa kutokana na umbali huo na hali ya hewa ya maeneo hayo, ni dhahiri kuna uwezekano wa watoto kutokuandikishwa shule, na kuzorotesha haki ya mtoto kupata elimu na sera ya elimu ya kila mtoto mwenye umri wa kuanza shule aandikishwe.
"Inakatisha tamaa ya kupenda shule kwa mtoto wa miaka sita na saba anayeanza shule kutembea Kilomita kumi na zaidi, mkurugenzi, zinatakiwa hatua za haraka za ukamilishaji wa ujenzi shule hii, ili watoto wetu wasiendelee kuteseka kutembea umbali huo" amesisitiza Waziri .