Vikundi vya Wanawake na Vijana wajasiriamali halmashauri ya Arusha
wilayani Arumeru, wameaswa kutumia fedha za mkopo walizopewa kwa malengo
waliyoyakusudia wakati wa kuomba mkopo ili kuwarahisishia urejeshaji wa
fedha walizokopa.
Akizungumza kwa niaba ya wanawake wenzie wakati wa kukabidhiwa mfano
wa hundi mwenyekiti wa kikundi cha JADEKI kilichopo kata ya Kiranyi
kinachojishughulisha na usindikaji mvinyo ndugu Juliana Mamuya amewaasa
wanawake wenzie kuhakikisha fedha walizopewa wanazitumia kwenye biashara
halisi walizozikusudia na kuziandika kwenye mchanganuo waliowasilisha
wakati wa kuomba mkopo.
Mamuya amethibitisha kuwa kuna baadhi ya wanawake ambao baada ya
kukabidhiwa fedha wanabadili mawazo ya biashara walizozikusudia
kuziifanya na kuamua kuanzisha biashara nyingine tofauti jambo ambalo
linasababisha kushindwa kurejesha fedha hizo kutokana na ugeni wa
biashara wanazokurupuka nazo.
"Unakuta mwanamke ni mfugaji wa kuku anaomba mkopo kuongeza mradi wa
kuku lakini akipokea pesa anaingiwa na tamaa na kununua toyo, siku mbili
toyo imeibiwa mara imepata ajali ni dhahiri mtu huyu hawezi kufanya
marejesho kwa wakati na kuingia kwenye mgogoro yeye na familia yake"
amesema Mamuya
Amewaasa wanawake wenzake kuacha tamaa badala yake kusimamia biashara
zao walizozoea kuzifanya kila siku jambo ambalo litawainua kiuchumi na
kuwarahisishia urejeshaji wa fedha walizozikopa .
Akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi ambaye ni Kaimu Mkuu wa Wilaya
ya Arumeru mheshimiwa Idd Kimanta, Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya
Arusha Dkt. Wilson Mahera amewataka wanawake hao kijikita kwenye
shughuli zao za uzalishaji utakaowawezesha kurejesha fedha na kupata
fursa ya kuchukua mikopo mingine na zaidi kutoa nafasi kwa makundi
mengine kupewa mkopo.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha Mheshimiwa Noah Lembris
amewataka wanawake hao kutambua kuwa fedha hizo zinatokana na kodi
mbalimbali wanazolipa na kurudishiwa asilimia kumi ya mapato hayo na
kuwataka kutumia fedha hizo kujikwamua kiuchumi na kurejesha kwa wakati
kwa kuwa mkopo sio zawadi.
Hata hivyo Afisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya Arusha Angela Mvaa
amewataka wanawake na vijana kujikita zaidi kwenye uanzishaji wa
viwanda vidogo na uzalishaji wa malighafi za viwanda ili kuwenda
sambamba na sera ya serikali ya viwanda.
Ameongeza kuwa kwa sasa serikali itajikita zaidi kutoa mikopo kwa
wajasiriamali wenye kujishughulisha na viwanda vidogo pamoja na
uzalishaji wa malighafi za viwanda. Aidha amesisitiza kuwa lengo la
kutoa mikopo hiyo ni kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa kuwawezesha
wananchi kujiajiri kuelekea uchumi wa kati ifikapo 2020.
Halmashauri ya Arusha imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni
220 kwa vikundi 43 vya wajasiriamalii, ikiwemo vikundi 38 vya wanawake
na vikundi 5 vya vijana, fedha hizo ni asilimia 10% ya fedha za mapato
ya ndani ya halmashauri.