Matumaini ya kupata nishati ya umeme yawashukia wananchi wa Mbuyuni
kata ya Oljoro baada ya kusubiri nishati hiyo tangu kupatikana kwa
Uhuru wa Tanganyika zaidi ya miaka hamsini iliyopita.
Matumaini hayo yakwenda mbali zaidi, baada ya Waziri mwenye
dhamana kuagiza na kusisitiza nishati hiyo ya umeme uwafikie wananchi
wote kwa kuzingatia kijiji kwa kijiji, kitongoji kwa kitongoji na hadi
nyumba kwa nyumba.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amesema hayo
alipotembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa umeme vijiji
unaotekelezwa na Wakala wa Umeme Vijijini - REA katika eneo la Mbuyuni,
halamshauri ya Arusha wilayani Arumeru.
Waziri Kalemani ameliagiza shirika la umeme TANESCO kupitia
wakaka wa umeme vijijini-REA kuwaunganishia umeme wananchi wote bila
kujali hadhi za nyumba zao wanazoishi.
Amesisitiza kuwa umeme uwekwe kwa mwananchi yoyote anaehitaji
na mwenye uwezo wa kulipia gharama za kuunganisha hata kama nyumba yake
ni ya udongo na kuezekwa kwa nyasi.
"Sitaki kusikia mneacha nyumba ya mtu kwa sababu hali duni ya
nyumba, hali ya nyumba ya mtu haiwahusu" amesisitiza Waziri Kalemani.
Aidha amewataka wananchi hao kulipia gharama za kuunganishiwa umeme
kiasi cha shilingi 27,000 tu na kuongeza kuwa endapo mtu atatozwa zaidi,
atoe taarifa kwa viongozi wa ngazi ya wilaya na mkoa.
Hata hivyo Waziri huyo ameagiza umeme uunganishwe ndani ya siku
saba baada ya mwananchi kukamilisha taratibu za malipo, na kuwataka
wananchi kulinda miundombinu ya umeme katika maeneo yao na kujenga uzio
kwenye transfoma.
Meneja wa TANESCO mkoa wa Arusha Gasper Msigwa amesema kuwa
REA III kwa kipindi cha awamu ya kwanza itawaunganishia nishati ya umeme
wateja wapatao 6,000 katika maeneo 58 ya mkoa wa Arusha, mradi utakao
gharimu shilingi bilioni 9.3. Ameeleza kuwa hadi sasa jumla ya wateja
1,652 wamekamilisha taratibu za malipo na tayari miundombinu ya umeme
imeksmilika kwa aslimia 90%.
Msigwa ameongeza kuwa, licha ya juhudi hizo za serikali ya awamu
ya tano, bado shirika linakabiliwa na changamoto ya wizi wa nyaya za
umeme na baadhi ya watu kukosa uaminifu na kujiunganishia umeme bila
kufuata taratibu.
Loth Sabaya mkazi wa Oljoro amesema kuwa wamefurashwa na neema
nishati ya umeme kijijini kwao, na kuongeza kuwa kukosa umeme
kunawacheleweshea maendeleo,na wanashindwa kufanya shughuli za
uzalishaji zinahitaji nishati ya umeme.