Mbunge
wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye pia ni Naibu waziri wa Madini
Mhe Doto Mashaka Biteko akisisitiza jambo wakati akizungumza na wafugaji
wa Jimbo la bukombe walioshiriki kwenye kikao cha kujadili namna ya
kuwa na ufugaji wenye tija katika jamii, Leo 4 Machi 2018. Picha Zote Na Mathias Canal-Wazo Huru Blog
Mbunge
wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye pia ni Naibu waziri wa Madini
Mhe Doto Mashaka Biteko akiwaeleza bwafugaji namna serikali ilivyo
jipanga kwa ajili ya kutenga maeneo ya malisho wakati akizungumza na
wafugaji Jimboni kwake Bukombe, Leo 4 Machi 2018.
Baadhi
ya wafugaji wakimsikiliza kwa makini Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani
Geita ambaye pia ni Naibu waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko
wakati wa kikao cha pamoja akizungumza na wafugaji Jimboni kwake
Bukombe, Leo 4 Machi 2018.
Na Mathias Canal, Geita
Baadhi
ya wafugaji wamemlilia Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye
pia ni Naibu waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko kwa kumtaka
kuwafikishia kilio chao kwa Waziri wa Wizara ya maliasili na Utalii Mhe.
Dkt Khamis Kigwangala juu ya kuwafichua baadhi ya maofisa wa serikali
wanaojinufaisha na mifugo ya wananchi hifadhini.
Manufaa
ya maofisa hao na askari wa wanyamapori yanajili kipindi wanapowakamata
Ng'ombe wa wafugaji wanaoingia katika maeneo ya hifadhi ya Taifa ambapo
huwakamata na kuwapiga mnada kwa bei yakutupa tofauti na thamani ya
wanyama hao.
Wananchi
hao wametoa malalamiko hayo leo 4 Machi 2018 mbele ya Mbunge huyo
wakati wa kikao na wafugaji wa Jimbo hilo la Bukombe kilichofanyika
katika eneo la shule ya msingi Shibingo katika kata ya Yogelo ikiwa ni
siku ya kwanza ya ziara ya Mbunge huyo katika Jimbo hilo la uchaguzi
tangu ateuliwe kuwa Naibu Waziri wa Madini.
Akizungumza
katika kikao hicho Mbunge Biteko alisema kuwa wananchi wanapaswa kutoa
taarifa Mara kwa Mara kwa uongozi wa vijiji ili kuwabaini maofisa hao
wanaofanya kazi kinyume na matakwa ya taratibu na sheria.
Aidha,
alisema kuwa wananchi wanapaswa kutambua kuwa kumekuwa na athari nyingi
katika jamii kutokana na kukamatwa Ng'ombe wengi kwa ukiukaji wa
taratibu kwa kuwaingiza kuchunga katika maeneo ambayo yametengwa kwa
ajili ya hifadhi.
Aliongeza
kuwa katika kipindi cha muda mrefu wananchi walijisahau na kupeleka
mifugo yao katika maeneo yasiyoruhusiwa kwa ufugaji hivyo kutokana na
usimamizi hafifu wa sheria wananchi wakadhani kuwa wapo sahihi kwa kila
wafanyalo kumbe sivyo.
Mhe
Biteko alisema hakuna kilichobadilika badala yake kumekuwa na usimamizi
madhubuti wa sheria katika kila sekta jambo ambalo linawaumiza kwa
kiasi kikubwa wananchi kwani hawakutegemea jambo hilo katika kipindi
hiki.
Akijibu
kuhusu serikali kuwatengea maeneo ya malisho wafugaji hao Mhe Biteko
alisema kuwa tangu serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli iingie
madarakani imekuwa na kazi kubwa ya kuondoa mifugo holela kutoka nchi
jirani jambo ambalo limeifanya serikali kushindwa kutenga maeneo hayo ya
malisho.
Sambamba
na hayo aliongeza kuwa wakati Tanzania inapata Uhuru 1961 kulikuwa na
Ng'ombe wasiozidi milioni 10 lakini kwa hivi Sasa kumekuwa na Ng'ombe
zaidi ya elfu 40 hivyo serikali inatumia busara kubwa kutenga maeneo
kwani kumekuwa na wingi wa mifugo lakini maeneo hayajaongezeka bado ni
yale yale.
Alisema
serikali imedhamiria kwa kauli moja kuwatoa wananchi katika ufugaji
holela usiokuwa na tija na kuhamia katika ufugaji wenye tija ili kuwa na
faida ya ufugaji huo kwa wananchi wenyewe.