Jamii imetakiwa kushiriki kwa hali na mali kutunza rasilimali maji
pamoja na kusimamia miundo mbinu ya maji inayojengwa kwenye maeneo yao
ili miradi ya maji inayojengwa iwe endelevu kwa miaka mingi ijayo.
Rai hiyo imetolewa na mkuu wa Idara ya huduma za Jamii Idara ya
Maendeleo ya Kimataifa Uingereza 'DFID', Bi. Getrude Mapunda alipokutana
na viongozi wa jamii kutoka eneo linalotekelezwa mradi wa maji wa
vijiji vitano ndani ya halmashauri ya Arusha maarufu kama mradi wa maji
wa WaterAid unaofadhiliwa na DFID kwa gharama ya shilingi bilioni 4.5.
Mapunda amekutana na viongozi hao ili kuthibitisha ushirikishwaji wa
jamii katika utekelezaji wa mradi huo ambao tayari miundo mbinu yake
imeanza kuchimbwa na unategemea kukamilika mwishoni mwa mwaka huu wa
2018.
Licha ya kuridhishwa na uelewa wa pamoja waliokuwa nao viongozi hao
baada ya kujengewa uwezo juu ya mradi huo wa maji, Mapunda amewataka
viongozi hao kuendelea kuweka mikakati thabiti ya utunzaji wa mazingira
ambayo ndio chanzo kikuu cha upatikanaji wa rasilimali maji.
Aidha amendelea kufafanua kuwa miradi ya maji inatumia gharama kubwa
kujengwa hivyo jukumu kubwa la wananchi ni kuwa na mikakati thabiti ya
kuitunza na kuiendeleza miradi hiyo ili iweze kutumika kwa miaka mingi
ijayo na vizazi vijavyo.
"Ili mradi wa mji uwe endelevu ni jukumu la jamii kutunza miundo
mbinu ya maji ikiwemo kuchangi gharama za maji kwa ajili ya maintainance
pamoja na kutunza mazingira ya uhifadhi wa maji" amesema Mapunda.
Naye mhandisi wa maji mkoa w Arusha Mhandisi Makaidi amethibitisha
hali halisi ya kupungua kwa kiasi cha maji inayotokana na mabadiliko ya
tabia nchi na kusababisha maji kupungua na kupatikana kwenye kina kirefu
kadiri siku zinavyokwenda tofauti na miaka ya nyuma.
Amefafanua kuwa suala la utunzaji wa mazingira linapaswa kupewa
kipaumbele na jamii nzima ili kuepuka madhara makubwa ya ukosefu wa maji
yanayoweza kutokea kwa siku za baadaye.
"Tafiti zinaonesha kwa sasa maji yanapatikana urefu wa mita 100 mpaka
150 kwenda chini, kama tusipochukua hatua madhubuti miaka kumi mpaka
ishirini ijayo maji hayo yatapatikana kina cha mita 200 mpaka 300 jambo
ambalo litaathiri hata miradi hii inayotekelezwa sasa" amesisitiza
Mhandisi Makaidi.
Hata hivyo viongozi wa jamii wa eneo la mradi wamethibitisha kuunga
mkono juhudi za serikali za utunzaji wa mazingira, utunzaji wa miundo
mbinu ya maji pamoja na uchangiaji wa gharama za huduma za maji ili
kuendeleza miradi hiyo ya maji ambayo serikali na wafadhili hutumia
gharama kubwa kuijenga.
Wameongeza kuwa katika maeneo yao kumekuwa na agenda ya kudumu ya
utunzaji wa mazingira kuanzia ngazi za familia na jamii nzima kwa
kuhamasisha wananchi kutunza mazingira.
Diwani wa kata ya Olkokola mheshimiwa Kalanga Laizer amesema kuwa
wananchi wa kata yake wamehamasika kujenga vyoo bora baada ya kuwa na
mkakati wa kutoza faini kwa nyumba isiyokuwa na choo bora na muitikio ni
mkubwa kwa sasa.
"Kwa sasa wananchi wa kwetu wana vyoo bora licha ya kuwa bado kuna
changamoto ya maji katika maeneo hayo lakini tunaamini mradi huu
ukikamilika shida itakwisha. Amesema Mheshimiwa Kalanga.