Mkuu wa
Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akisisitiza umakini kwa wananchi waliojitokeza kwenye Kikao cha Mafunzo ya namna bora ya kushiriki katika kilimo chambogamboga na matunda kupitia umwagiliaji
Afisa kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ayub Sengo akiwasihi wananchi kutumia njia za kisasa katika kilimo cha umwagiliaji na kufuata taratibu wanazoelekezwa na wataalamu wa kilimo
Baadhi ya viongozi wa vikundi mbalimbali vya ujasiriamali sawia na wajumbe washiriki kwenye mafunzo hayo wakifatilia kwa makini Muelimishaji
Kutoka Kushoto ni Mkurugenzi wa Asasi isiyo ya
kiserikali ya RIWADE
Mhandisi Ayubu Massau, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Mkuu wa
Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu, Moses Msai Mratibu wa RIWADE
mkoa wa Singida na Afisa kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ayub Sengo
Kulia ni Mkuu wa
Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu na kulia kwake ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Bi Haika Massawe wakifatiliakwa makini mafunzo ya namna bora ya kujishughulisha na kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia Gree House
Kutoka Kushoto ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Hassan Tati, Mkurugenzi wa Asasi isiyo ya
kiserikali ya RIWADE
Mhandisi Ayubu Massau, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Bi Haika Massawe, Mkuu wa
Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu, Moses Msai Mratibu wa RIWADE
mkoa wa Singida na Afisa kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ayub Sengo
Dc Mtaturu akisisitiza jambo wakati wa kufunga mafunzo hayo
Na Mathias Canal, Singida
Uongozi wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida umeahidi kuvisaidia vikundi
mbalimbali ambavyo vitakubali kujihusisha na kilimo cha mbogamboga na
matunda (Perishable Crops) sambamba na kilimo hicho kwa kutumia Kitalu
Nyumba (Green House).
Kauli ya serikali imetolewa na Mkuu wa
Wilaya hiyo Mhe Miraji Jumanne Mtaturu wakati akifunga mafunzo kwa
wajasiriamali, wakulima na wafugaji yaliyoendeshwa na Asasi isiyo ya
kiserikali ya Right Way For Development (RIWADE) kwenye ukumbi wa
Mikutano katika Shule ya Sekondari Ikungi na kuhudhuriwa na watu 115
ambao wanatokea katika Kata 24 kati ya Kata 28 zilizopo Wilayani humo.
Katika Mafunzo hayo jumla ya Vikundi 39 vimehudhuria ambavyo vimetakiwa
kujishughulisha zaidi kukimbia kilimo cha mazoea ambacho wakulima
hulima msimu mmoja hadi mwingine na hatimaye kujihusisha na kilimo cha
umwagiliaji ambacho kinatumia muda mchache kukamilika na kuanza kwa
mavuno.
DC Mtaturu amevitaka vikundi hivyo kwa pamoja kutumia
vyema fursa ya Makao makuu ya serikali kuhamia Mjini Dodoma kwani
itakuwa taswira chanya katika kukuza soko la mazao yao pasina kupata
ugumu wa uuzaji.
Amesema kuwa Mkoa wa Singida mara nyingi umekuwa
ukitajwa kama mkoa masikini nchini Tanzania kati ya mikoa 10 ambayo ipo
mkiani katika maendeleo ya kiuchumi kwa sababu ya wananchi wenyewe
kutofanya ubunifu katika kilimo chao jambo ambalo linasababisha
uzalishaji mdogo na kupelekea kipato kuendelea kuwa duni ilihali
maandalizi ya mashamba ni makubwa.
Mtaturu amesema kuwa wananchi
wanapaswa kutoa ushirikiano kwa serikali katika kukamilisha adhma yake
katika uwekezaji na Tanzania ya viwanda kwani endapo watakubali kulima
kilimo cha kisasa na kuwa na uzalishaji mkubwa itakuwa rahisi kwa
serikali kuanzisha viwanda vya kusindika mazao.
Kwa upande wake
muwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Asasi isiyo ya
kiserikali ya RIWADE ambayo imesajili kwa lengo la kiwasaidia vijana
wasio na ajira waweze kufanya kilimo, Ufugaji, Uvuvi na Mazingira
Mhandisi Ayubu Massau alisema kuwa wananchi wanapaswa kufikia kilimo cha
kuachana na kuuza mazao yao kwa madalali badala yake kuuza moja kwa
moja kwa mtumiaji jambo ambalo litatoa fursa chanya ya mafanikio makubwa
katika pato la mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Hata
hivyo amepigia chepuo zaidi kilimo cha Kitalu Nyumba (Green House) na
kusema kuwa ndicho kilimo pekee chenye uwezo wa kuwatoa wananchi kwenye
kadhia ya umasikini kwani kilimo hichp kupitia umwagiliaji wa kisasa
unatumia maji machache na matokeo yake ni makubwa kama wakulima
watafuata taratibu zote za utunzaji wa shamba.
Massau alisema
kuwa umefika wakati wa wananchi kuachana na vyama vya kufa na kuzikana
badala yake kujihusisha zaidi na vyama vya kujikwamua kiuchumi kupitia
vikundi mbalimbali.
Naye Moses Msai ambaye ni Mratibu wa RIWADE
mkoa wa Singida alisema kuwa wakulima wanapaswa kutambua kuwa sekta
pekee yenye uwezo wa kuajiri watu wengi na kuwatoa kwenye lindi la
umasikini ni Sekta ya Kilimo hivyo ni vyema kufanya kilimo cha kisasa
kwani ndicho kitakacho wanufaisha wananchi.
Ametoa fursa kwa
wananchi kujiunga na RIWADE kwani watapata fursa ya kuunganishwa na
wataalamu ili kuelekezwa namna bora ya kulima kilimo cha umwagiliaji.
Hata hivyo Mjasiriamali na mkulima aliyeshika nafasi ya Kwanza kanda ya
kati katika sekta ya kilimo Hassan Tati aliwasihi wakulima hao
waliopatiwa mafunzo kuwa mafanikio kwenye kilimo ni makubwa endapo
wakulima watafuata taratibu za kilimo na kuwasikiliza wataalamu.
Tati amesema kuwa hakuna ajira nzuri duniani kama kuwekeza kwenye kilimo
lakini amewasihi wananchi kuing'ang'ania Asasi ya RIWADE kwani ni
taasisi muhimu kwa kila mmoja kwa kujitolea kutoa mafunzo ya kilimo na
ufugaji.
Asasi isiyo ya kiserikali ya Right Way For Development
(RIWADE) ilianzishwa Mwezi June 2016, ikiwa ni dhima ya kutengeneza na
kutoa fursa kwa watanzania wote ili waweze kupata elimu ya ujasiriamali
na namna ya kutengeneza mitaji kwa ajili ya ukuaji endelevu wa kijamii
na kiuchumi.