Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Onorius Njole (kushoto), akitoa ufafanuzi mbalimbali kwenye semina ya siku moja ya wanahabari kuhusu mifuko ya jamii Dar es Salaam leo. Kulia ni Mkuu wa Idara ya Uhusiano na Uhamasishaji, SSRA, Sarah Kibonde.
Mkurugenzi wa Tafiti, Sera na Tathmini wa SSRA, Ansgar Mushi akitoa mada katika warsha hiyo.
Waandishi wa habari wakiwa katika semina hiyo.
Waandishi wakiwa kwenye semina hiyo
Semina ikiendelea.
Waandishi wa habari wakichukua mambo kadhaa kwenye semina hiyo.
Wanahabari wakiwa makini katika semina hiyo.
Maswali yakiulizwa.
Taswira meza kuu katika semina hiyo.
Picha ya pamoja waandishi wa habari na maofisa wa SSRA.
Na Dotto Mwaibale
MAMLAKA ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii nchini (SSRA), imewataka Watanzania kuondoa hofu iliyojengeka kwenye jamii kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii ina hali mbaya kifedha.
Akizungumza katika warsha maalum ya siku moja ya waandishi wa habari, iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa SSRA, Ansgar Mushi alisema kuwa mifuko hiyo haina hali mbaya kama wanavyodhani watu katika jamii kwani ina fedha za kutosha.
“Watanzania wamekuwa wakiambizana kuwa mifuko hii ina hali mbaya kifedha, napenda kuwahakikishia kuwa ina fedha za kutosha kwani tumekuwa tukifanya ukaguzi wa mara kwa mara. Katika kaguzi zetu za mara kwa mara hakuna mfuko tuliobaini kuwa una kasoro au upungufu wowote,” alisema Mushi.
Aidha, Mushi alisema kwa mwaka mifuko hiyo ya pensheni imekuwa ikikusanya jumla ya sh trilioni 1.692 wakati mfuko wa bima ya afya (NHIF) unakusanya sh bilioni 88.5 ambapo jumla ya makusanyo yote ni sh trilioni 1.78.
Kwa upande wa fao la kujitoa, Mushi alisema licha ya kutawaliwa na sintofahamu, fao hilo lilifutwa na Serikali kuanzia mwaka 2012 na kwa sasa SSRA imeanzisha mchakato wa kuratibu uanzishwaji wa fao la upotevu wa ajira.
Mushi alisema kuwa fao hilo lilipofutwa, bado kulikuwa na mifuko iliyoendelea kuruhusu kujitoa lakini kwa sasa wameamua waanzishe mchakato wa fao la kupoteza ajira, ambalo ni mahususi kwa ajili ya kuwanufaisha waathirika.
“Fao la Upotevu wa ajira litakuwa mahsusi kwa ajili ya wale waliopoteza ajira zao, huku wakiwa wamechangia mifuko ya hifadhi kwa kipindi cha miezi zaidi ya 18. Hawa watalipwa asilimia 33 ya mshahara wa mwisho kwa kipindi cha miezi 6,”
“Kipindi hicho cha miezi 6 kikiisha, mtu huyo kama hajapata ajira atawekwa katika hatua nyingine ambapo ataruhusiwa kuchukua nusu ya fedha alizochangia katika kipindi chake cha ajira,” alisema Mushi.
Akizungumzia wale waliopoteza ajira zao wakiwa hawajafikisha kipindi cha miezi 18, Mushi alisema kuwa wataruhusiwa kuchukua asilimia 100 ya fedha walizochangia kipindi chote walipokuwa kwenye ajira.
“Watu hao wataruhusiwa kuchukua fedha zao kwa asilimia 100 ambazo walichangia kipindi wakiwa waajiriwa. Hata hivyo, napenda kuwaambia Watanzania kuendelea kuichangia mifuko hiyo kwani ina manufaa zaidi nyakati za uzeeni baada ya kustaafu,” alisema Mushi.