SERIKALI mkoa wa Kilimanjaro imeahidi kuwakamata na kuwachukulia
hatua za kisheria wazazi na walezi ambao watoto wao watapewa ujauzito
huku wao wakishindwa kuonesha juhudi za kuwasaka wahusika.
Mkuu wa Mkoa huo, Said Mecky Sadiki amesema hayo wakati akikagua
ujenzi wa madarasa katika shule ya sekondari Mpirani, kata ya Mabogini
wilayani Moshi Vijijini ili kuona matatizo yake.
Kauli ya Mkuu wa Mkoa inatokana na taarifa ya Mkuu wa shule hiyo, Ali
Mhando kwamba kwa kipindi cha miezi minane sasa jumla ya wanafunzi
wanne wamepewa ujauzito na kuacha shule huku mmoja akiwa tayari
amejifungua.
A,esema haiwezekani mwanafunzi akapewa ujauzito huku mzazi ama mlezi
wake akikaa kimya bila jitihada za kukemea na kuchukua hatua za kisheria
kwa wahusika kama njia mojawapo ya kukomesha vitendo hivyo.
Sadiki alisema serikali haiwezi kuvumilia kuona wanafunzi
wanakatishwa masomo na baadhi ya watu wenye nia ovu kwani kwa mujibu wa
takwimu mkoa huo kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu,
wanafunzi 238 wamepewa ujauzito.
Akikagua vyumba vya madarasa pamoja na matundu 12 ya vyoo
vilivyogharimu zaidi ya Sh milioni 88, Sadiki alitaka wananchi kuchangia
ujenzi wa vyumba vya madarasa na chakula shuleni badala ya mzigo huo
kuwaachia wazazi pekee.
Mkuu wa shule hiyo, Mhando amesema wamebaini watuhumiwa wakuu wa
kuwapa wanafunzi ujauzito ni waendesha bodaboda na madereva wa daladala.
Amesema wanafunzi wa shule hiyo wanatoka katika vijiji vya Mvuleni,
Mtakuja na Mabogini ambapo baadhi yao wanatembea umbali wa zaidi ya
kilometa 10 kwenda shule na kurudi, jambo ambalo huwapa vichocheo vya
kupata lifti za pikipiki na daladala na kuwapa vishawishi vya mahusiano
ya kimapenzi.