Ticker

6/recent/ticker-posts

VURUGU ZAIBUKA UVCCM ARUSHA,POLISI WAINGILIA KATI


baadhi ya wanachama Wa UVCCM mkoa Wa Arusha wakiwa  wanaminyana na askari Wa chama cha mapinduzi  kuzuia kufunga ofisi hiyo kutokana na mgogoro uliopo Wa kutaka Katibu Wa zamani Ezekiel Molel alieamishwa kukabidhi ofisi kwa Katibu mpya 
Na Woinde Shizza,Arusha

Baadhi ya vijana wa  chama cha mapinduzi mkoa wa Arusha (UVCCM) leo wamefanya Vurugu  katika jengo la makao makuu ya ofisi za  jumuiya ya umoja wa vijana wa chama cha Mapinduzi (Uvccm) mkoani Arusha baada ya baadhi ya vijana wa umoja huo kufunga  ofisi hizo



Tukio hilo lilitokea  majira ya asubuhi  ambapo baadhi ya vijana hao walijitokeza katika ofisi hizo na kufunga ofisi hizo na mara baada ya kufunga wakati walipoondoka ndipo mwenyekiti wa UVCCM  Lengai Ole Sabaya akiwa na baadhi ya viongozi wa chama na vijana wa chama hicho kujitokeza na kisha kuzifungua  kabla ya jeshi la polisi kuingilia kati.



Katika vurugu hizo jeshi la polisi mkoani Arusha linamshikilia mwenyekiti wa miradi ya jumuiya hiyo,Phillemon Amo ambapo alikamatwa na kisha kufikishwa mbele ya kituo kikuu cha polisi cha kati mkoani hapa.



Hatua hiyo ilifuatia baada ya ofisi hizo kufungwa kwa  minyororo jana majira ya saa 8;00 asubuhi na baadhi ya wanachama wa umoja huo wakipinga kitendo cha katibu aliyehamishwa,Ezekiel Mollel kuendelea kushikilia ofisi.



Hatahivyo,majira ya saa 11;30 kundi linguine la baadhi ya   wanachama  wa umoja huo likiongozwa na mwenyekiti wa jumuiya hiyo mkoani Arusha,Lengai Ole Sabaya lilifika na kisha kufungua tena ofisi hizo .



Mara baada ya tukio hilo ndipo jeshi la polisi mkoani hapa majira ya saa 11;00 asubuhi liliwasili katika ofisi hizo na  kumshikilia mwenyekiti huyo na kisha kumfikisha  mbele ya kituo kikuu cha polisi cha kati.



Akizungumzia tukio hilo kamanda wa jeshi la polisi mkoani Arusha,Charles Mkumbo alithibitisha kushikiliwa kwa kiongozi huyo huku akisema kwamba atatoa taarifa kamili mara baada ya kumaliza mapokezi ya ugeni wa serikali mkoani hapa.



“Ni kweli tumemkamata lakini nina ugeni wa serikali naomba nitoe taarifa baadae”alisema Mkumbo  lakini alipotafutwa baadae simu yake iliita bila kupokelewa



Awali baadhi ya wanachama wa umoja huo waliwasili  majira ya asubuhi  na kisha kufunga kwa minyororo ofisi hizo kwa madai ya kupinga kitendo cha katibu aliyehamishwa,Ezekiel Mollel kushindwa kukabidhi ofisi na kumpisha katibu mteule,Said Goha.



Wanachama hao waliwasili katika eneo hilo na kisha kufunga ofisi hizo  huku wakimtaka Mollel akabidhi ofisi hiyo haraka  kwa madai uhamisho wake ni utaratibu wa kawaida ndani ya jumuiya hiyo na unapaswa kuheshimiwa.



Hatahivyo,mara baada ya muda mchache kundi jingine la wafuasi wa umoja huo likiongozwa na Ole Sabaya liliwasili katika ofisi hizo wakiwa na nyundo,vyuma na mawe na kisha kuanza kukata minyororo iliyokuwepo na kufungua ofisi hizo.



Akizungumza mara baada ya kufungua ofisi hizo Ole Sabaya alisema kwamba yeye kama mwenyekiti anapinga vikali na kulaani kitendo cha baadhi ya wanachama wa umoja huo kufunga ofisi hizo kinyume na taratibu.



Mwenyekiti huyo alisema kwamba tayari wamevitaarifu vyombo vya dola kuchukua hatua na kuchunguza kwa kina tukio hilo kwa kuwa kufungwa kwa ofisi hizo anahisi ni njama za kutaka kuhujumu taasisi yao.







“Ofisi ni lazima zifunguliwe ili kazi za vijana ziendelee lakini tumevitaarifu vyombo vya dola kuanza kuchunguza kwa kina tukio hili kwa kuwa tunahisi hizi ni njama za kutaka kutuhujumu”alisema Ole Sabaya



Akizungumzia suala la Mollel kushindwa kukabidhi ofisi Ole Sabaya alisema kwamba katibu huyo hatakwenda popote kwa kuwa kuna njama zinasukwa kwa lengo la kupoteza ushahidi wa baadhi ya tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya fedha ndani ya umoja wao kwa kumwondoa katibu huyo.




Post a Comment

0 Comments