WASHINDI 10 WA SHINDANO LA KUINGIZA SAUTI KWENYE FILAMU KUPATA FURSA YA KUFANYA KAZI NA STARTIMES NCHINI CHINA


Na Dotto Mwaibale 

 WASHINDI 10 kumi watakaopatikana kwenye shindano la kuingiza sauti kwenye filamu na tamthiliya za Kichina kwenda lugha ya Kiswahili liloendeshwa na StarTimes Tanzania watapata fursa ya kwenda kufanya kazi katika makao makuu yake yaliyopo jijini Beijing, China.

Akizungumzia juu ya taarifa hiyo Makamu wa Rais wa StarTimes Tanzania, Zuhura Hanif amebainisha kuwa katika jitihada za kuboresha maudhui ya vipindi mbalimbali vinavyopatikana kwa lugha za kigeni kama vile Kichina yaweze kueleweka na kufurahiwa na wateja wao, kampuni hiyo inatoa fursa kwa watanzania kumi kwenda kufanya kazi ya kuingiza sauti za lugha ya Kiswahili jijini Beijing, China yalipo makao makuu ya kampuni hiyo.

“Mpaka hivi sasa tayari wamekwishapatikana washindani watano kwenye usaili uliofanyika Arusha na Zanzibar, watano kwa kila mkoa. Kwa upande wa mkoa wa Dar es Salaam pia tunatarajia kuwapata watano siku ya Jumamosi ya Septemba 10 katika ukumbi wa Coco beach kuanzia saa 2 asubuhi mpaka 12 jioni. Washindani hao ambao jumla yao itakuwa ni 15 watashindanishwa katika fainali, ambapo washindi kumi watapatikana na kujipatia fursa ya mkataba wa miaka miwili wa kwenda kufanya kazi katika ofisi za makao makuu ya StarTimes yaliyopo jijini Beijing, China.” Alisema Hanif

Hanif ameendelea kwa kufafanua kuwa dhumuni kubwa la kufanya hivyo ni kuwawezesha wateja wa StarTimes kuelewa na kufurahia maudhui yaliyopo kwenye lugha za mataifa mengine kama vile Kichina.

“Tunafahamu kuwa wateja wetu ni wapenzi na watazamaji wakubwa wa filamu na mfululizo wa tamthiliya kadha wa kadha za Kichina lakini wanashindwa kuelewa lugha inayozungumzwa. Hilo tumeliona baada ya kuonyesa tamthiliya kadhaa za Kichina zilizotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili kupendwa sana na kupendekezwa na wateja. Hivyo basi tumeona kuwa hatuna budi kuongeza nguvu katika rasilimali watu kwa ajili ya kuingiza sauti za lugha ya Kiswahili katika tamthiliya na filamu hizo.” Alifafanua zaidi Hanif

StarTimes kupitia matangazo ya runinga wamekuwa wakifanya jitihada za kutosha katika kukuza lugha ya Kiswahili kwani ndio lugha inayozungumzwa sana katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati.

Kupitia visimbuzi vyake StraTimes inayo chaneli mahususi kwa ajili ya vipindi vyenye maudhui kwa lugha ya Kiswahili ijulikanayo kama StarTimes Kiswahili. Chaneli hii inaonekana katika nchi za Tanzania na Kenya na kutoa uwanja mpana kwa kazi za sanaa kwa lugha hiyo kuonekana.

“Hivyo basi ningependa kuchukua fursa hii kuwataka watanzania kutembelea ofisi zetu ili kujaza fomu za kushiriki katika shindano hili. Hakuna gharama zozote za kujaza fomu hizo na kwa hapa Dar es Salaam maduka yetu yapo sehemu za Bamaga Mikocheni, Buguruni, Posta mtaa wa Samora, Kariakoo mtaa wa msimbazi, Makumbusho, Vingunguti na Mkuki Mall. StarTimes inaamini kuwa kuna watanzania wengi wenye vipaji vya kuingiza sauti kwa lugha fasaha ya Kiswahili na huu ndio wakati wao.” Alihitimisha Makamu huyo wa Rais wa StarTimes nchini

Katika shindano hili la aina yake na kipekee kuwahi kufanyika nchini Tanzania litakalofanyika jijini Dar es Salaam wikiendi hii, washiriki watakuwa wakiingia kwenye chumba maalumu cha kuingizia sauti baada ya kupewa sehemu fupi ya filamu au tamthiliya ya Kichina. Mshirikia mwenye sauti nzuri na kufanikiwa kuingiza sauti kwa ufasaha ndiye atakayechaguliwa kuwa mshindi.

Katika kichumba hicho si majaji wala hadhira watakaoshuhudia ni nini kinafanyika isipokuwa mshiriki pekee akiingiza sauti tu. Mshiriki atajajiwa kutokana na ubora wa sauti yake tu, hivyo washiriki kumi wenye sauti bora kabisa ndio watakaofanikiwa kuwa washindi na kujipatia fursa ya kufanya kazi nchini China yalipo makao makuu ya kampuni ya StarTimes.


Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post