ANTI Ezekiel
waziri nyalandu
Mwigizaji wa filamu nchini, Aunty Ezekiel amekanusha uvumi
ulioenea kuwa alikwenda nchini Marekani akifuatana na Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu .
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Aunty
alisema hadi sasa haelewi nia ya wanaovumisha habari hiyo isiyokuwa na
chembe ya ukweli wowote.
“Mashabiki wangu wajue nilikwenda Marekani kwa
mwaliko wa Blogu ya Vijimambo, ambao walitaka nikashiriki katika sherehe
yao ya kutimiza miaka minne, wakati wote nilikuwa na mwenyeji wangu,
Lukasi Mkami,” alisema.
Mwigizaji huyo alisema akiwa Marekani alipigiwa
simu na waandishi wengi wakimuuliza kuhusu ziara yake na aliwaeleza
ukweli ulivyo, lakini anashangaa kibao kimemgeukia.
“Sijakaa Marekani siku 14 kama inavyoelezwa, nimekaa kule siku 10 tu, nimeenda tarehe 13 (Septemba) na kurudi 24.
Nilikutana na Nyalandu tarehe 13, Waziri alikuwa
mgeni rasmi, tangu usiku huo wa hafla sikumwona tena na sijui kama
aliendelea kuwapo Marekani au aliondoka.”
Alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo, Waziri Nyalandu
alijibu kwa kifupi bila kufafanua alichomaanisha akisema, “Waongo wote,
sehemu yao ni katika ziwa liwakalo moto.”
Aunty ni mmoja kati ya wasanii wa kike nchini
wanaofanya vizuri katika tasnia ya filamu, ambayo imekuwa ikizidi
kuitambulisha Tanzania nje ya mipaka yake kwa filamu zao tangu
walipofanya mapinduzi miaka ya 2000.