Umoja wa Vijana wa CCM, UVCCM Wilaya ya Hanang' Mkoani Manyara, umepinga
uteuzi wa
Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye, kuwa Kamanda mpya wa UVCCM wa
wilaya hiyo, badala yake wanataka Mbunge wa Jimbo hilo Dk Mary Nagu
aendelee na ukamanda wake.
Wakizungumza juzi vijana hao walisema viongozi wa UVCCM
wilaya hiyo walifanya kosa kwa kupeleka jina moja la Sumaye badala ya majina matatu
ya mbunge wa jimbo hilo Dk Mary Nagu na Charles Gapchojiga.
Vijana
hao walidai kuwa kupitia kikao chao cha Baraza la UVCCM wilaya wanapinga uteuzi
huo wa Sumaye kuwa kamanda wa UVCCM wilaya kwani utaratibu haukufuatwa kwa
kupendekezwa jina moja badala ya majina matatu.
Baadhi
ya wajumbe, Katibu wa UVCCM kata ya Masqaroda Shamimu Ally, Katibu UVCCM kata ya Gidahababieg Theresia
Mahuka na Mwenyekiti UVCCM kata ya Masakta Emmanuel Manase walidai kuwa uteuzi huo siyo halali kwani
haukufuata utaratibu.
Katibu wa UVCCM kata ya Measkron Faustin Anselim, alisema wajumbe
wanne kati ya sita wa Baraza la utekelezaji UVCCM wilaya, walipitisha jina la
Sumaye peke yake na kuacha majina mengine ya Gapchojiga na Dk Nagu.
"Hata Mwenyekiti wa Chipukizi wa wilaya, ambaye ni mjumbe wa Baraza hilo
hakuwepo kupitisha jina hilo, hivyo sisi bado tunamtambua kamanda wa sasa Dk
Nagu, kuwa bado ni kamanda wa UVCCM wilayani humu," alisema Anselim.
Alisema wao hawamtambui Sumaye kuwa ni kamanda wao kwani taratibu za kupitisha jina lake hazikufuatwa hivyo wanamtambua Dk Nagu, ambaye bado hajamaliza muda wake, ndiye kamanda wa UVCCM wilaya ya Hanang’.
Kwa upande wake, Sumaye alisema alishapatiwa barua ya kuteuliwa
kwake kuwa kamanda wa UVCCM wilayani humo na anachosubiri hivi sasa ni
kuapishwa kwenye nafasi hiyo ya ulezi wa vijana Octoba 18 mwaka huu.
"Mchakato huo ulifanyika kwa njia ya halali kwani ulianza ngazi ya
wilaya kwa UVCCM wilaya ya Hanang’ kupendekeza jina langu lililopelekwa UVCCM
mkoa, ambao nao walilipeleka UVCCM Taifa, nao waliopitisha jina hilo," alisema Sumaye.
Alisema endapo kuna mtu ana wasiwasi kuhusu hilo waulizwe
viongozi wa CCM mkoa au UVCCM mkoa wanaweza kujibu
kwani akizungumza yeye ataonekana kwamba anajitetea mwenyewe.
Hata hivyo, Katibu wa UVCCM mkoa wa
Manyara, Ezekiel Mollel alisema mchakato wa kupitisha jina la Sumaye kuwa
Kamanda wa UVCCM wilayani Hanang' ulifuata utaratibu wote hivyo
amepatikana kihalali.
Mollel alisema walipata majina matano ya watu ambao walipendekezwa na UVCCM Hanang' kuteuliwa kuwa Kamanda na wao wa tukapitisha majina matatu kwenda Taifa, ambao wamepitisha jina moja la Sumaye kuwa Kamanda.
Mollel alisema walipata majina matano ya watu ambao walipendekezwa na UVCCM Hanang' kuteuliwa kuwa Kamanda na wao wa tukapitisha majina matatu kwenda Taifa, ambao wamepitisha jina moja la Sumaye kuwa Kamanda.