Mbowe akabithi vifaa vya michezo vyenye thamani ya shs 10 milioni.


MBUNGE wa  jimbo la Hai ,Freeman Mbowe amekabithi jezi na vifaa vya michezo vyenye thamani ya shs 10 milioni kwa timu 16 za michezo zitakazoshiriki mashindano ya Mbowe Cup yatakayofanyika mkoani Kilimanjaro.

Akikabithi vifaa hivyo wilayani Hai ,jana Katibu wa Mbunge , Ndonde Totinan alisema kuwa, vifaa hivyo ni kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya Mbowe Cup yatakayoanza rasmi oktoba 18 mwaka huu.

Ndonde alisema kuwa, mchakato wa kupatikana kwa timu hizo ni baada ya kuwepo kwa mashindano katika timu za kata ambapo timu 18 zilishiriki na hatimaye kuweza kupatikana timu16 zilizoshinda na kuingia kwenye mashindano  hayo ngazi ya  wilaya.

Alisema kuwa, timu hizo zitakuwa zinacheza mchezo wa mtoano hadi kuweza kupata timu bora tatu ambazo zitaweza kupata zawadi huku mshindi wa kwanza akipatiwa kiasi cha shs 500,000,mshindi wa pili akipatiwa shs 300,000 na mshindi wa tatu akipatiwa shs 150,000.

Ndonde alifafanua kuwa, ofisi ya mbunge imefikia hatua ya kutekeleza wajibu huo kwa kutambua mchango mkubwa wa vijana katika kupenda michezo na kuweza kuinua vipaji vya vijana hao na hatimaye kuweza kupata timu zilizo bora.

Alifafanua kuwa, ofisi hiyo imeahidi kuendelea kusaidia timu hizo katika kuhakikisha kuwa zinafanya vizuri na hatimaye kufikia malengo yao waliyojiwekea.

Naye Mwenyekiti wa chadema wilaya ya Hai,James Mushi aliwataka vijana hao kuonyesha nidhamu ya hali ya juu katika mashindano hayo ili kufanikisha mchezo huo.

Mushi aliwataka wananchi na wachezaji hao kutohusisha  mashindano hayo ya Mbowe Cup na siasa , ambapo alisema kuwa mashindano hayo hayahusiana kabisa na maswala ya kisiasa .

‘nawaombeni sana msichanganye maswala ya siasa kwenye michezo kwani swala hilo limekuwa likichangia kwa kiasi kikubwa sana kuporomoka kwa michezo hapa nchini,hivyo aliwataka kutoleta siasa kwenye michezo’.alisema Mushi.

Aidha aliwataka wadau mbalimbali kuanzisha programu za michezo ngazi za  shule za msingi ili kuwawezesha kupenda na kujifunza michezo wakiwa tangu wadogo na hatimaye kuweza kupata timu zilizo bora zaidi.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post