Mkuu wa Wilaya ya
Arusha John Mongela akiongea jambo wakati akifungua rasmi mafunzo ya siku mbili kuhusu masuala ya
jotoardhi kwa washirki kutoka nchi
zilizo katika bonde la Ufa . Mafunzo hayo yanatangulia kabla ya ufunguzi rasmi
wa Kongamano la Tano la Kimataifa la Jotoardhi litakalofunguliwa tarehe 29
Oktoba, 2014 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
Mohamed Gharib Bilal.
Baadhi ya washiriki
wanaohudhuria mafunzo kuhusu masuala la jotoardhi wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya
ya Arusha John Mongela hayupo pichani wakati akifungua rasmi mafunzo hayo.
Imeelezwa
kuwa, nguvu ya nishati mchanganyiko ikiwemo jotoardhi ni kichocheo na kipimo
cha maendeleo kwa nchi yoyote kutokana na umuhimu wa nishati hiyo kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za uchumi na viwanda.
Hayo
yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya
Arusha John Mongela wakati akifungua mafunzo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa
Arusha Magesa Mulongo, kuhusu masuala yanayohusu jotoardhi yaliyoanza leo katika Ukumbi wa Mikutano
wa Kimataifa wa Arusha (AICC).
Mafunzo
hayo yanashirikisha washiriki takriban 150 kutoka nchi mbalimbali za Afrika zilizo
katika bonde la ufa na nchi nyingine
duniani.
Aidha,
ameongeza kuwa, mafunzo hayo ni muafaka kwa Tanzania kutokana na uzoefu ambao
washiriki wataupata kutoka nchi nyingine ambazo zimepiga hatua katika masuala
ya jotoardhi kama Kenya na Ethiopia ambazo
zimechangia katika gridi ya Taifa ya nchi zao kiasi cha megawati 500 za nishati
ya umeme unaotokana na jotoardhi.
Kwa
upande wake, Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia nishati jadidifu,
Wizara ya Nishati na Edward Ishengoma, ameeleza kuwa, mafunzo hayo na uwepo wa
kongamano hilo kwa Tanzania kuna manufaa makubwa.
Ishengoma
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano la tano la
Kimataifa la Jotoardhi alitaja manufaa hayo kama kutangaza hazina kubwa ya
jotoardhii iliyopo Tanzania, jambo ambalo litasaidia kuvutia wawekezaji na
taasisi zinazofanya utafiti wa masuala ya jotoardhi.
Ameongeza
kuwa, nishati ya jotoardhi ni nishati isiyokwisha hivyo uwepo na matumizi yake
yatasaidia katika ukuaji wa viwanda ikiwemo kuchangia katika sekta za kilimo na
manufaa yake ni makubwa kimaendeleo.
“Jotoardhi
ni chazo ambacho hakiishi. Uzalishaji wake hauna mwisho na una manufaa makubwa.
Tanzania tunataka kukiendeleza chanzo hiki kama wenzetu Kenya na
Ethiopia”amesisitiza Ishangoma.
Aidha,
mafunzo hayo ni mwendelezo wa shughuli mbalimbali zitakazofanyika katika
kongamano la tano la Kimataifa la Jotoardhi litakalofunguliwa rasmi tarehe 29
Oktoba, 2014, na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Mohamed Gharib Bilal.
Washiriki
wa kongamano hilo pia watapata fursa ya kutembelea katika maeneo yenye dalili
za jotoardhi ikiwemo Ngorongoro na Manyara lakini pia watapata nafasi ya
kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini.