HIKI NDICHO KILICHOMFANYA SIPORA KUGOMBANA NA MKUU WA MKOA WA ARUSHA

Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora, Sipora Liana (pichani) , amesema mwaka jana alivyokuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha aliingia katika mgogoro mkali na Mkuu wa Mkoa baada ya kugoma kutoa milioni 100.
Mkurugenzi aliyasema hayo jana wakati akijitetea mbele ya Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, dhidi ya madai ya matumizi mabaya ya madaraka kwa kumsimamisha kazi aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Kilimo na Mifugo na Ushirika, Dk. Francis Mallya, wa Halmashauri ya Mkuranga.
Liana alitoa madai hayo bila kutaja jina la Mkuu wa Mkoa aliyeomba fedha hizo wala hakufafanua kwa undani kuhusiana na jinsi alivyoombwa fedha hizo wala lengo lake.
Mkurugenzi huyo alikuwa akihojiwa na Mwanasheria wa mlalamikaji, Getrude Cyricus, ambaye alitaka aeleze kitu gani kilimfanya akaingia kwenye mgogoro alivyokuwa Mkurugenzi wa Jiji.
Mbele ya Mwenyektii wa Baraza hilo, Jaji Hamis Msumi, alidai kuwa “RC Arusha alitaka nitoe Sh milioni 100 nilivyokataa ndiyo chanzo cha mgogoro,” alidai Liana.
“Watumishi ambao hawanipendi ni wale ambao wanataka kutafuna fedha za umma au kujichotea watakavyo, nimesimamia hilo na ndiyo msimamo wangu na sitayumba,” alisisitiza.
Alidai ulaji ndani ya Halmashauri una mtandao mrefu sana na unahusisha watu wengi na kwamba daima hakubaliani na watu wanaochota fedha ya umma kwa manufaa yao wenyewe.
“Kila Halmashauri niliyopita nimeziba mianya ya ‘ulaji’ wa fedha za umma, niliingia Mkuranga kukiwa na mapato ya milioni tatu kwa mwezi, lakini ndani ya muda mfupi nilipandisha hadi kufikia milioni 71, Jiji la Arusha niliweza kufikisha hadi zaidi ya bilioni moja, sikubaliani na ulaji, wizi na hapo ndipo napigwa vita sana kila ninapohamishiwa,” alidai.
Awali, Dk. Mallya alilieleza Baraza hilo kuwa kusimamishwa kazi kwa kipindi cha wiki 17 na wiki tatu kumemuathiri kisaikolojia, kiuchumi na hakutendewa haki kwa kuwa kanuni, sheria na taratibu hazikufuatwa na hivyo jamii kumuona asiyefaa.
Alidai katika kumsimamisha kazi Liana alitumia ubabe kwa kuwa kwa kipindi chote aliwekewa zuio la kutotoka nje ya wilaya bila kibali na bila kamati ya uchunguzi ikikutana kwa siku moja kwa saa moja na kutoa uamuzi.
Alidai kwa wakati huo mama yake alikuwa mgonjwa alihitaji kupelekwa India kwa matibabu, alikosa ruhusa kwa madai kuwa ni mtuhumiwa huku akikataa asipandishwe daraja, hivyo kuathirika kiuchumi kwa kubaki kwenye daraja la mshahara wa TGSD J huku waliokuwa naye kazini wakiwa mbali. Akijibu madai hayo, Liana alisema Dk. Mallya alisimamishwa majukumu yake kutokana na mwenendo wa utendaji kazi zake na wizi wa fedha za umma kwa kushirikiana na Mkaguzi wa Ndani, Mwenyekiti wa halmashauri, Afisa Utumishi na watumishi wengine.
“Baada ya kuhamishiwa pale Agosti 2008, Septemba kulikuwa na ukaguzi maalum wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), iliyotaja watumishi 68 na Mwenyekiti wa Halmashauri kuhusika kwenye ubadhilifu na kutakiwa kurudisha fedha hizo…niliwaandikia barua wote akiwemo Mwenyekiti,” alidai.
Alidai ndani ya muda huo alipata safari ya kikazi na kumkabidhi ofisi Dk. Mallya, ambaye hakuwa na maelekezo ya kushughulikia ripoti ya CAG, lakini kwa kipindi kifupi aliitisha Bazara la Madiwani kwa ajili ya kuazimia kumfukuza kazi (Liana).
Alidai katika ripoti hiyo Mwenyekiti wa halmashauri alikuwa anawekewa mafuta na halmashauri kila siku kwenye magari yake mawili na teksi yake na kutokana na urafiki wa Dk. Mallya na Mwenyekiti, walimuondoa na kumuweka yeye (Mallya) kama Kaimu DED.
Alisema Mkuu wa Wilaya, Clemence Urawia, alimtaka Dk. Mallya kuomuonyesha mashamba darasa yaliyotajwa kwenye ripoti ya CAG, lakini alimzungusha na yeye (Liana) aliomba ampeleke akampa msaidizi wake ambaye baada ya kusafiri kilomita tano alimueleza ukweli kuwa hakuna miradi kama hiyo.
Kulikuwa na miradi hewa kama ya barabara, joshu, na bwawa ikiwamo kuweka katika ripoti iliyokwenda kwenye Kamati ya CCM wilaya mazao ambayo hayalimwi kwenye eneo husika.
“RC na DC waliniagiza kumfukuza kazi, lakini nilimwandikia barua ajieleze, lakini hakufanya hivyo…Dk. Mallya kwa kushirikiana na wengine alikuwa anafanya hujuma nyingi, lakini nilimsamehe na wakati mwingine kumtaka ajieleze na kuomba ushauri kabla ya kumchukulia hatua,” alieleza.
Liana alieleza kuwa kuna wakati hakuwapo ofisini fedha za uwekezaji zilitolewa na kuelekezwa kwenye ujenzi wa ofisi ya Mallya huku akijua fedha hizo zinapaswa kutekeleza miradi pekee badala ya matumizi mengine na kwamba kuna wakati faili la barua lilitoweka katika mazingira tatanishi.
Alisema fedha za wakulima wa korosho Shilingi milioni 65 zilitaka kuliwa, lakini kutokana na jitihada zake zililipwa kwa wakulima baada ya suala hilo kufika mbele ya kamati ya ulinzi na usalama. Alidai kuwa Dk. Mallya alikuwa anashirikiana na baadhi ya viongozi wa mkoa kumkwamisha na kula fedha za halmashauri na hata alipounda kamati ya uchunguzi hakupata ushirikiano stahili badala yake alipigwa vita ili akate tamaa, lakini hakurudi nyuma katika kusimamia fedha ya umma.
“Baada ya Dk. Mallya kusimamishwa mambo yalianza kwenda kwa kuwa nina taaluma ya kilimo, nilisimamia uanzishwaji wa mashamba darasa matano na kupata fedha nyingine za utekelezaji wa miradi 44 ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), ambazo zililiwa,” alidai.
“Kwa ujumla mazingira ya utendaji kazi kwangu yalikuwa magumu sana kwa kuwa yalitengenezwa na Dk. Mallya na wenzake waliotaka kutafuna fedha,” alidai.
Shauri hilo linatarajiwa kuendelea kesho kwa DED kuleta mashahidi zaidi ambao ni Mwansheria wa Halmashauri, Mkuu wa wilaya na Mkuu wa mkoa wa Pwani.
DC GAMBO ATUHUMIWA TUHUMA NZITO
Wakati huo huo, Mkuu wa wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, Mrisho Gambo, alifika mbele ya Baraza hilo na Mkurugenzi wa Mji wa Korogwe kueleza jinsi anavyotukana na kudhalilisha watumishi wa halmashauri.
Mkurugenzi wa mji huo, Lewis Kalinjuna, akiongozwa na mwanasheria Hassani Mayunga, alidai amefanyakazi kwenye halmashauri kwa miaka 27 na wakuu wa wilaya 14, lakini hajawahi kukutana na kiongozi mwenye lugha chafu na za kudhalilisha kama Gambo.
Alidai kuwa mara kwa mara amekuwa akiwaita watumishi kwenye vikao vya kamati ya ulinzi na usalama na kuwadhalilisha.
Alidai DC Gambo amekuwa akitumia mikutano ya hadhara ya wananchi na watendaji kudhalilisha watendaji, ikiwa ni pamoja na kumtaka DED kutohudhuria vikao vya kamati ya ulinzi na usalama ambavyo yeye (DC) ni Mwenyekiti.
Mkurugenzi huyo aliweka hadharani majina ya watumishi waliowahi kutukanwa na kudhalilishwa na kudai kuwa ana mashahidi juu ya malalamiko hayo.
Alidai DC huyo amekuwa akilazimisha halmashauri kukiuka sheria za manunuzi, kuweka shinikizo watumishi kuchukuliwa hatua kinyume cha sheria.
Kalinjuna alidai kuwa DC huyo alilazimisha kutumika kwa mafundi wa kawaida kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa huku fedha zilizotolewa zikiwa na masharti ya kutumia wakandarasi.
Shauri hilo litaendelea kesho kwa mashahidi zaidi kutoa ushahidi wao.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post