MBUNGE
wa Monduli, Edward Lowassa, (CCM), amekemea tabia ya baadhi ya viongozi
wa serikali na mila wanaochukua rushwa na kuuza ardhi za wananchi
wakiwemo wajane kinyume cha utaratibu.
Aidha,
ameitaka jamii ya wafugaji kuelewa kuwa ardhi ni utajiri mkubwa, hivyo
wailinde kwani wanavyoiuza ndiyo tatizo la ukosefu wa maeneo ya malisho
ya mifugo yao linavyozidi kukua.
Lowassa,
aliyasema hayo jana wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa kujadili
changamoto za ardhi na mazingira wilayani Monduli uliowashirikisha
wajumbe zaidi ya 400 wakiwemo viongozi wa mila (malaigwanani), viongozi
mbalimbali wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi, (CCM) kuanzia ngazi za
Vijiji, Kata na Wilaya.
Alisema
kuwa tatizo la ardhi wilayani hapa ni kubwa lakini limekuwa likizidi
kuongezeka kutokana na wafugaji kuuza ardhi waliyokuwa wakiitumia kwa
ufugaji kwa watu wengine ambao huibadilisha matumizi na kuitumia kwa
kilimo na kuendeleza makazi.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu huyo aliyejiuzulu, alisema kuwa sehemu kubwa ya
ardhi ya jimbo hilo imetengwa kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori na
jeshi, huku eneo dogo likibaki kwa ajili ya matumizi ya wananchi ambao
idadi yao imekuwa ikiongezeka, hivyo akawataka washiriki wa
mkutano huo wajadili matumizi bora na endelevu ya ardhi hiyo.
“Tumewaita
hapa tujadiliane tuone tatizo liko wapi kisha tushauriane tufanye nini
kulimaliza, ndiyo maana tumewaalika wataalam wa ardhi wa halmashauri na
Kamaishna msaidizi wa ardhi (Kanda ya Kaskazini),
Doroth Wazala watusaidie,” alisema Lowassa.
Kwa
upande wake, Mbunge wa viti maalum, Namelok Sokoine (CCM), alisema kuwa
wilayani hapa kuna migogoro mingi ya ardhi kuanzia ngazi za familia
na koo, jambo linaloibua uhasama miongoni mwa jamii kutokana na wengine kuamua kupelekana mahakamani.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia