
Mkuu wa Polisi wilayani Masasi, Ndagile
Makubi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa
watuhumiwa hao walikamatwa juzi jioni katika eneo la Masasi mbovu
watuhumiwa kutokana na kucheza wakiwa watupu kunakokiuka maadili ya
Kitanzania.
Alisema walipata taarifa za kuwepo kwa
tukio hilo la kiudhalilishaji kutoka kwa wasamaria wema waliokuwepo
kwenye sherehe hizo na kwamba Polisi walifika na kufanikiwa kuwatia
mbaroni watuhumiwa hao waliokutwa wakiwa wanaendelea kutoa burudani hiyo
kwa mamia ya watu waliojitokeza kwenye sherehe hizo wakiwamo watoto.
Makubi aliwataja wanaoshikiliwa na jeshi
hilo kuwa ni pamoja na Anna Yohana (25), Jemima Jordan (22), Aziza
Chukachuka (20) na mtoto wa miaka 17 (jina linahifadhiwa) wote wakiwa ni
wakazi wa mjini Masasi mkoani Mtwara.
Alisema uchunguzi unaendelea na kwamba
watakapobainika kuhusika na tukio hilo la udhalilishaji hasa kwa jinsia
ya kike watafikishwa mahakamani kwa taratibu zingine za kisheria.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Tiba
Matwani na Fatuma Hamisi wamepongeza Polisi wilayani Masasi kwa kuanza
operesheni hiyo na kwamba vitendo hivyo vinavyofanywa na wanawake wenzao
havistahili kuachiwa vikiendelea kwa kuwa vinadhalilisha utu wao.
Aidha, Kamanda Makubi alizungumzia
mikakati iliyowekwa na jeshi hilo mjini humo, ikiwa ni pamoja na
kuendesha operesheni maalumu kwenye maeneo yote ya burudani na sherehe
mbalimbali ili kuwabaini watu wote wanaokwenda kinyume na maadili ya
Kitanzania.