KILIMANJARO waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu,
ameagiza kufanyika uchunguzi wa haraka juu ya tuhuma za ubakaji unaodaiwa
kufanywa na askari wa hifadhi ya
Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) dhidi ya wanawake waliokuwa wakikata
majani ndani ya hifadhi hiyo kwa nyakati tofauti.
Nyalandu ametoa
agizo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mbahe wilaya
ya Moshi mkoani Kilimanjaro, kufuatia malalamiko yaliyotolewa na Mbunge wa Jimbo
la Vunjo (TLP), Augustino Mrema juu ya
vitendo vya askari hao kuendesha vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Kabla ya
agizo hilo, wananchi wa kijiji hicho ambacho ni moja ya vijiji vinavyozunguka
hifadhi hiyo, walimweleza waziri huyo kuwepo kwa baadhi ya askari hao, kuwabaka
pindi wanapoingia katika hifadhi hiyo kwa lengo la kukata majani ya ng’ombe.
Alisema
askari yeyote wa wanyamapori haruhusiwa kuwapiga, kuwatesa wala kuwafanyia
vitendo vya udhalilishaji, na kwamba
hayo siyo sehemu ya majukumu yao na kuongeza kuwa askari anapomkamata mharifu sharti amfikishe kwenye vyombo vya sheria.
Waziri Nyalandu
alisema askari yeyote atakaye bainika kuhusika na matukio hayo atafikishwa katika
vyombo vya maamuzi na sehemu yake ya ajira
katika wizara ya maliasili
haitakuwepo akatafute kazi kwingine.
Amefafanua kuwa
wapo baadhi ya askari wamekuwa wakitumia vyeo vyao vibaya, jambo ambalo
limepelekea kuwepo kwa mahusiano mabaya baina ya wahifadhi na wananchi wa
kawaida.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti katika mkutano huo, wananchi hao walisema askari hao
wamekuwa wakiwachapa viboko, na vitendo
vya udhalilishaji pindi wanapoingia ndani ya hifadhi hiyo.
Mmoja wa
waathirika wa matukio hayo ya ubakaji aliyejitambulisha kwa jina la Therecia Minja mkazi wa Kijiji hicho cha Mbahe,
alimweleza waziri Nyalandu kuwa alikumbwa na mkasa huo Septemba 17 mwaka huu wakati akikata majani
ambako alilazimishwa na askari hao kuvua nguo zake zote na kisha kubakwa.
Kwa upande
wake Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Dkt Agustino Lyatonga Mrema, alisema kumekuwepo
na matukio ya ubakaji na udhalilishaji wa wananchi yanayofanywa na askari wa
KINAPA.
Alisema
mahusiano ya askari wa hifadhi ya mlima Kilimanjaro, KINAPA na wananchi sio
mazuri kwani wananchi hao wamekuwa wakibambikiziwa kesi huku wanawake
wakifanyiwa vitendo vya kinyama ndani ya hifadhi hiyo.