DIWANI WA THEMI KUCHANGIA MAJI SHULE YA MSINGI ENGIRA

DIWANI wa Kata ya Themi, Milance Kinabo, (CHADEMA), ameahidi kutoa sh 50,000 kila mwezi kwa ajili ya kuchangia gharama za ankara ya maji kwenye shule ya Msingi Engira, jijini hapa.
Aidha, amesaidia kukamilisha ujenzi wa mfumo wa maji taka kwenye choo cha matundu nane cha wanafunzi wa shule hiyo, hivyo kuanza kutumika baada ya kushindwa kutumika kwa zaidi ya miaka mitano.
Alitoa ahadi hiyo mwishoni mwa wiki wakati alipokuwa akikabidhi vifaa mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya usafi wa choo cha shule hiyo, zikiwemo ndoo za kuchotea
maji, brashi na sabuni.

Kinabo, alisema ameamua kuchangia kiwango hicho cha fedha ili kuwapunguzia mzigo wazazi wa shule hiyo ambao kwa sasa hulipa sh 80,000 kila mwezi.
“Nimesaidia kubadili mfumo wa maji taka, nimejenga chemba hivyo sasa choo hiki kitatumika ila kitahitaji maji mengi, hivyo kuanzia sasa nitakuwa nalipa kiasi cha fedha kitakachoongezeka kwenye hiyo 80,000,” alisema Kinabo.
Aliziomba taasisi, kampuni na jamii kwa ujumla kuona umuhimu wa kujitolea kwa kuchangia elimu katika shule za Kata, ambazo baadhi yake zinakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vifaa vya kufundishia na madawati.

Kinabo, alisema kuwa kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata, (WDC), hatakubali shule yoyote katika kata yake ikabiliwe na changamoto itakayosababisha wanafunzi kukwama kimasomo, ambako aliahidi ikibidi atatumia rasilimali zake kumaliza kero
zitakazojitokeza.

Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Simon Siara, alimshukuru diwani huyo kwa misaada yake ya mara kwa mara, ingawa alilalamikia mwamko mdogo wa
wazazi kuchangia malipo ya mlinzi wa shule, mpishi na ankara za maji

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post