Kamati Kuu ya Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imekutana katika kikao chake cha kawaida
na kujadili, pamoja na mambo mengine, mchakato wa Katiba Mpya. Kamati Kuu
imepata taarifa ya kina juu ya mchakato ulivyoendeshwa katika hatua mbali mbali
wakati wa kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na marekebisho yake na,
baadaye, Sheria ya Kura ya Maoni.
Aidha, Kamati Kuu imepata taarifa ya mchakato
ulivyokuwa katika hatua ya kuundwa kwa Tume ya Mabadiliko, kukusanya maoni ya
wananchi na kuandaliwa kwa Rasimu ya Kwanza na ya Pili ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Vile vile, Kamati
Kuu imepata na kujadili taarifa ya kina juu ya mchakato wa Katiba katika hatua
ya uteuzi wa Bunge Maalum na baadaye ndani ya Bunge hilo. Mwisho Kamati Kuu
imepata uchambuzi wa kina wa Katiba Inayopendekezwa iliyopitishwa na Bunge
Maalum tarehe 2 Oktoba, 2014.
Uchambuzi
huo utatolewa kwa vyombo vyote vya habari na kwa wananchi wa Tanzania kama
taarifa hapo baadae.
Baada ya mjadala
mrefu na wa kina, Kamati Kuu imeridhika kwamba mchakato wa Katiba katika hatua
zake zote ulitawaliwa na nia mbaya iliyokuwa na lengo kuu la kuhakikisha kwamba
hakuna mabadiliko yoyote ya maana yatakayofanyika kwenye mfumo wa kikatiba na
kiutawala ambao umekuwepo katika nchi yetu kwa zaidi ya miaka hamsini.
Ø Mchakato
wa kutunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ulitawaliwa na ubabe na usiri
uliohakikisha kwamba mchakato wa Katiba unadhibitiwa na Serikali na Chama cha
Mapinduzi;
Ø Uteuzi
wa wajumbe wa Bunge Maalum kutoka ‘Kundi la 201’ ulifanywa na Rais Jakaya
Kikwete kwa lengo la kuhakikisha wajumbe wengi zaidi wa Kundi hilo wanatoka CCM
na washirika wake. Kwa sababu hiyo, zaidi ya asilimia 82 ya wajumbe wa Bunge
Maalum kutoka Kundi la 201 walikuwa wanachama wa CCM waliochomekwa katika
makundi na taasisi mbali mbali;
Ø Sambamba
na idadi hiyo ya wajumbe wa Kundi la 201, asilimia 72 ya wajumbe wa Bunge
Maalum waliotokana na Kundi la Wabunge na Wawakilishi wa Zanzibar walikuwa
wanachama wa CCM;
Katika hatua ya
mjadala ndani ya Bunge Maalum, Kamati Kuu imeridhika kwamba mjadala huo
ulitawaliwa na ukiukwaji wa wazi wazi wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na
Kanuni za Kudumu za Bunge Maalum.
Ø Bunge
Maalum lilijigeuza ‘Tume’ na kuanza kukusanya upya maoni ya wananchi kuhusu
Katiba Mpya, wakati kazi ilikwisha kufanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba;
Ø Muda
wa kuwasilisha taarifa za Kamati mbali mbali ulifupishwa kutoka dakika sitini
hadi dakika ishirini na ule wa kuwasilisha maoni tofauti ulifupishwa kutoka
dakika thelathini hadi dakika kumi;
Ø Utaratibu
wa kupiga kura juu ya Katiba Inayopendekezwa kwa njia ya kifungu kwa kifungu uliondolewa
na badala yake kura zilipigwa kwa ujumla ya Sura za Rasimu, yaani kura
zilipigwa kwa Sura kumi za mwanzo na baadae kwa Sura tisa mwisho;
Ø Wajumbe
waliokuwa nje ya Ukumbi wa Bunge, au nje ya Dodoma na hata waliokuwa nje ya nchi
kwa sababu mbali mbali kama vile mahujaji na wagonjwa waliruhusiwa kupiga kura
ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa;
Ø Kura
za wajumbe waliopinga baadhi ya vifungu vya Katiba Inayopendekezwa na kukubali vifungu
vingine zilihesabiwa kuwa kura za kukubali Katiba Inayopendekezwa;
Katika
mazingira haya, mambo ya ajabu na yenye kuifedhehesha nchi yetu yaliyotokea ndani
ya Bunge Maalum yasingeacha kutokea.
Ø Wajumbe
Waislamu waliokwenda Makkah kuhiji na ambao uongozi wa Bunge Maalum ulieleza
mwanzoni kwamba wangepiga kura kwenye Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia
hawakupiga kura Ubalozini na haijulikani walipigia wapi kura zao. Aidha, sasa
inajulikana kwamba Mahujaji hao – kama ni kweli walifanya hivyo - walipiga kura
siku moja kabla ya siku rasmi ya upigaji kura kwenye Bunge Maalum;
Ø Licha
ya Waheshimiwa Mohamed Raza na Salim Turky – wote wa kutoka Zanzibar - kuharibu
kura zao, kura hizo zilizoharibika zilihesabiwa kuwa kura halali za ‘Ndiyo’;
Ø Kura
za wajumbe waliokufa kama vile Marehemu Shida Salum zilihesabiwa kuwa kura halali
za ‘Ndiyo’;
Ø ‘Kura
za Maruhani’, yaani wajumbe wa UKAWA kutoka Zanzibar na za Wazanzibari wengine
waliojitoa na ambao hawajulikani majina yao hadi sasa zilihesabiwa kuwa kura halali
za ‘Ndiyo’;
Ø Mheshimiwa
Maulida Komu wa UKAWA ambaye alitajwa kwenye Gazeti la Serikali lililotangaza
majina ya wajumbe wa Bunge Maalum kuwa anatoka Zanzibar aligeuzwa na kuhesabika
kuwa anatoka Tanzania Bara, wakati Mheshimiwa Zakia Meghji wa CCM aliyetangazwa
kwenye Gazeti la Serikali kuwa anatokea Tanzania Bara alihesabika kuwa anatoka Zanzibar
na hivyo kupiga kura ya ‘Ndiyo’ kama Mzanzibari;
Ø Kura
za partly ‘Hapana’ na partly ‘Ndiyo’ zilizopigwa na wajumbe
wanne wa kutoka Zanzibar zilihesabika kuwa ni kura za ‘Ndiyo.’
Kamati Kuu
imeridhika kwamba, katika mazingira haya, theluthi mbili ya kura za Zanzibar
isingeacha kupatikana. Katika mazingira haya, na kwa kipimo chochote, Kamati
Kuu imeridhika kwamba upigaji kura ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa ulikuwa
batili - na matokeo ya upigaji kura huo - yaani Katiba inayopendekezwa haiwezi
kuwa halali.
Na katika mazingira
haya, ujasiri unaostahili kupongezwa wa Mwanasheria wa Zanzibar, Othman Masoud
Othman, na wajumbe wengine nane wa Zanzibar waliopiga kura ya wazi ya ‘Hapana’
kuikataa Katiba Inayopendekezwa licha ya shinikizo kubwa, matusi na vitisho vya
kila aina, usingeweza kuzuia uharamia huu wa CCM.
Kwa hali hii,
Kamati Kuu inaungana na vyama vingine vya siasa vya UKAWA, taasisi kuu za
kidini nchini kama vile Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), Baraza la Kikristo
Tanzania (CCT), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT), Shura ya
Maimamu, Baraza Kuu la Taasisi za Kiislamu, n.k. kulaani matukio yote
yaliyotokea wakati wa mchakato wa Katiba katika hatua zake zote hadi sasa. Kamati
Kuu inapondeza na kuunga mkono taasisi, mashirika na vyama vya siasa pamoja na
wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba waliosusia tukio la Rais Kikwete
kukabidhiwa Katiba Inayopendekezwa siku ya tarehe 8 Oktoba, 2014.
Aidha, Kamati Kuu
inatoa rai kwa taasisi na mashirika yasiyokuwa ya kiraia ambayo tayari
yameshaonyesha msimamo wa kuiunga mkono Katiba Inayopendekezwa kujifikiria upya
na kujiridhisha kama mashirika yao hayatumiki kuhalalisha mambo haramu ambayo
yamefanywa na CCM na washirika wao katika mchakato huu.
Kamati Kuu
imeazimia kwamba CHADEMA itaungana na vyama na taasisi zilizotajwa hapa pamoja
na umma wa Watanzania wenye nia njema na taifa kuhakikisha kwamba wanashiriki
katika kampeni kubwa na ya nchini ili kuhakikisha kwamba Katiba Inayopendekezwa
inapigiwa kura ya ‘Hapana’ katika kura ya maoni, ambayo ni hatua ya mwisho ya
mchakato wa Katiba.
Katika hili, Kamati
Kuu inatoa rai kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhakikisha kwamba inatekeleza
ahadi yake kwa Watanzania kwamba Daftari la Kudumu la Wapiga Kura litaboreshwa
kabla ya kufanyika kwa kura ya maoni ili kuhakikisha kwamba kila Mtanzania
mwenye haki ya kupiga kura anajiandikisha kwenye Daftari hilo na anapata haki
ya kushiriki katika maamuzi ya jambo hili muhimu kwa taifa letu.
Kamati Kuu
inawakumbusha Watanzania kujiandaa kutimiza wajibu wao wa kihistoria wa kukataa
uchakachuaji wa maoni yao uliofanywa na CCM na washirika wake katika Bunge
Maalum. Kukataa uchakachuaji huu kitakuwa ni kitendo cha kizalendo cha kila
Mtanzania. Kunyamazia au kuunga mkono uchakachuaji huu itakuwa ni kuisaliti
nchi yetu na kuendeleza utawala wa kikandamizaji na wa kifisadi ambao umekuwa
janga la taifa letu kwa miaka mingi.
-------------------------------------------------------
Dr.
Willibrod P. Slaa
KATIBU MKUU