KAMPUNI
ya Bia Tanzania (TBL), imetumia sh milioni 80 kufanikisha shughuli
mbalimbali wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama barabarani
nchini.
Hayo
yalisemwa na Ofisa Uhusiano wa TBL, Dorris Malulu, wakati wa zoezi la
upimaji afya kwa madereva wa mabasi na magari ya mizigo lililofanyika
kituo cha kupimia uzito magari Makuyuni wilayani Monduli mkoani Arusha.
Malulu,
alisema wameamua kufadhili madhimisho hayo kutokana na ukweli kwamba,
TBL ni wadau wakubwa wa usalama barabarani, ukizingatia kwamba bidhaa
zao zinasafirishwa kwa njia ya barabara hadi kuwafikia wateja wao.
Katika
fedha hizo, alisema zimetumika katika upimaji wa afya, kugawa
vipeperushi, stika, fulana, kofia na shughuli nyinginezo huku
akibainisha mwaka huu walilenga kuwafikia madereva 2,000 katika vituo
vya Mikese, Msata na Makuyuni.
Kwa
upande wake, Mganga Mkuu wa Jeshi la Polisi kutoka Makao Makuu, Dk.
Charles Msenga, alisema katika kituo cha Mikese walifanikiwa kuwapima
afya madereva 800, wakati Msata walikuwa 600 na Makuyuni 800.
Akizungumzia
hali waliyoikuta wakati wa zoezi hilo, Dk. Msenga, alisema wamewakuta
baadhi ya madereva wakiendesha magari huku Shinikizo la Moyo (BP),
likiwa juu kwa kiwango cha 217 kwa 125 na dereva huyo alikuwa amebeba
abiria 60, hivyo kulazimika kumpumzisha kwa muda na kumpatia dawa.
“Pia
madereva wengi tumekuta macho yao yana uono hafifu ama kwa macho yote
au jicho moja, ambapo hawa tumewapa ushauri na kuwataka waendelee na
matibabu ama kwa kupewa miwani itakayowasaidia kuona vizuri,” alisema
Dk. Msenga.
Naye
Mratibu wa Huduma za Macho Jiji la Arusha, Dk. Juraj Msuya, alisema
dereva wa gari anatakiwa kila baada ya miezi mitatu awe anapima macho
yake ili kujua yana kiwango gani cha kuona wakati akiwa anaendesha
chombo cha usafiri.
Awali,
Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Jowika Kasunga, aliyekuwa mgeni rasmi katika
zoezi hilo, aliwashukuru TBL kwa kufanikisha upimaji wa afya za
madereva kwa madai kuwa, zoezi hilo lina gharimu kiasi kikubwa cha
fedha.
Naye
Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani nchini, Mohamed Mpinga, alitoa
wito kwa madereva kote nchini kujenga tabia ya kupima afya zao pindi
wanapopata nafasi.