Chama
Kikuu cha Wakulima wa Kahawa Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU), kimemjia juu
mrajisi wa vyama hivyo nchini kwa kile ilichodai kukwamisha ustawi na
maendeleo yake.
Kauli
hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na mwenyekiti wa KNCU, Maynard Swai
wakati akisoma hotuba yake katika mkutano mkuu maalumu ulioitishwa kwa
shinikizo la mrajisi huyo, Dk Audax Rutabanzibwa.
Licha
ya kupokea lawama hizo, Dk Rutabanzibwa aliyekuwa mwenyekiti katika
mkutano huo hakuweza kujibu malalamiko yaliyoelekezwa kwake na
mwenyekiti huyo.
Mwenyekiti
huyo aliwaachia wajumbe wa mkutano huo kufanya uamuzi kwa njia ya kura
kama bodi ya uongozi iendelee au ing’oke ambapo kura 83 zilikataa na 68
zikitaka ing’oke.
Swai alisema ofisi ya mrajisi huyo imekuwa kikwazo cha maendeleo kwa KNCU .
“Mfano,
shamba la Garagagua lilitakiwa kuuzwa Mei 2014, wajumbe mlisharidhia
lakini kutokana na ukiritimba wa ofisi ya mrajisi imekwama,” alisema
Swai. Swai aliitaja mipango mingine kuwa ni ujenzi wa hosteli ya kisasa
na hoteli kwenye eneo la makao makuu ya KNCU.
“Sina
nia ya kuifundisha au kuikumbusha ofisi ya Mrajisi wajibu wake
kiutendaji lakini ina wajibu wa kushauri na kusimamia ushirika ili
uendelee kushamiri nchini kwa manufaa ya wanachama,”alisema.
Lakini
Swai alisema hata tume mbalimbali za uchunguzi zilizotumwa KNCU katika
kipindi kifupi cha miaka miwili na Mrajisi, hazijawahi kutoa mrejesho wa
matokeo ya uchunguzi huo.
“Kifungu
57(1) cha sheria namba 6 ya Ushirika ya mwaka 2013 imeweka bayana kuwa
ikiwa kuna uchunguzi au ukaguzi umefanywa dhidi ya chama cha Ushirika,
Mrajisi atapaswa kutoa matokeo ya uchunguzi huo,”alisema Swai.
KNCU
kimeshangazwa pia na hatua ya Mrajisi kutoamini ukaguzi uliofanywa na
COASCO ambacho ni chombo cha Serikali kuhusu kiasi cha hasara ambayo
KNCU ilipata wakati wa mdororo wa uchumi duniani mwaka 2008.
Katika
hesabu hizo, KNCU ilionyesha kupata hasara ya zaidi ya Sh765 milioni
wakati uhakiki uliofanywa na hazina ulionyesha KNCU kilipata hasara ya
Sh250 milioni.
“Mrajisi
aliagiza kufuatiliwa kwa tofauti hii huku akionesha kutokuwa na imani
na hesabu zilizokaguliwa na COASCO jambo ambalo linashangaza kama
Serikali haiwezi kuamini kazi iliyofanywa na chombo chake,” alisisitiza
Swai.