BREAKING NEWS

Thursday, October 9, 2014

RUFAA BARABARA YA SERENGETI YAANZA

 
Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), imeziagiza pande zinazohusika kwenye rufaa ya kupinga hukumu ya kuzuia ujenzi wa barabara ya lami kupitia katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuwasilisha hoja zao ifikapo Desemba 5, mwaka huu.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania, ambaye ndiye mrufani ametakiwa kuwasilisha kwa maandishi hoja zake ifikapo Oktoba 22 na asasi isiyo ya kiserikali ya Africa Network For Animal Welfare (ANAW) ya Nairobi, Kenya ikitakiwa kujibu Novemba 21, mwaka huu.
Jopo la majaji watatu wa Kitengo cha Rufaa cha EACJ, Loboire Nkurunziza, James Ogola na Edward Rutakangwa wanaosikiliza rufaa hiyo namba 3 ya mwaka 2014, wamemwagiza mrufani kutoa majibu ya ziada ili Mahakama ipange siku ya kusikiliza rufaa hiyo.
Pande zote zimekubaliana kushughulikia hoja zote nne za rufaa zilizowasilishwa na Mwanasheria Mkuu, kupitia kwa Wakili wa Serikali, Gabriel Malata.
Katika hoja zake, Serikali inadai Mahakama ya Awali ya EACJ ilikosea kisheria kukubali kupokea, kusikiliza na kuamua shauri namba 9 la mwaka 2010 lililofunguliwa na ANAW kupinga wazo la ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 239, ikidai itaathiri mazingira, uhai wa wanyama na baionuai.
Serikali pia inakiomba Kitengo cha Rufaa kubatilisha hukumu ya mahakama ya awali, kuamuru ilipwe fidia na gharama za kesi na amri nyingine kama mahakama itakavyoamua.
Katika shauri la msingi, ANAW inayowakilishwa na wakili Kanchori Saitabau ilitaja madhara kumi ya ujenzi wa barabara hiyo ikiwamo, kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu, kusumbua wanyamapori katika maeneo yao ya asili, ongezeko la magari na uchafuzi wa hewa kutokana na moshi wa magari.
Walidai utekelezaji wa mradi huo unakiuka ibara za 5(3), 8(1), 111(2) na 114 (1) ya mkataba wa EAC unaelekeza wajibu kwa nchi za EAC kupanga na kutekeleza sera na miradi yote iliyo chini ya mamlaka na wajibu wao kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates