Mheshimiwa Dkt.
Fenella Mukangara (MB), Waziri wa Habari,
Vijana, Michezo, Utamaduni na Michezo;
Mheshimiwa Zainabu
Omar Mohamedi, Waziri wa Uwezeshaji,
Ustawi wa Jamii, Vijana Wanawake na
Watoto – Zanzibar;
Mheshimiwa Fatuma A.
Mwasa, Mkuu wa Mkoa wa Tabora;
Mheshimiwa Samwel
Sitta, Waziri wa Afrika Mashariki, Spika Mstaafu na Aliyekuwa Mwenyekiti wa
Bunge Maalum la Katiba;
Waheshimiwa Mawaziri
na Naibu Mawaziri;
Waheshimiwa Wabunge
na Wajumbe wa
Baraza la Wawakilishi;
Ndugu Mwenyekiti
wa CCM Mkoa wa Tabora;
Waheshimiwa Wakuu wa
Mikoa kutoka Tanzania
Bara na Zanzibar;
Makatibu Wakuu kutoka
Wizara Mbalimbli Tanzania
Bara na Zanzibar;
Waheshimiwa Mabalozi
na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Waheshimiwa viongozi
wa vyama mbalimbali vya Siasa;
Viongozi wetu wa
Kiroho kutoka katika Madhebu mbalimbali;
Vijana Wetu;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Nawashukuru
Mawaziri
wetu Mheshimiwa Fenella Mukangara wa Serikali ya Muungano na Mheshimiwa
Zainabu
Omari Mohamed wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kunialika kuja
kushiriki
katika sherehe za mwaka huu za kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Napenda pia kutumia nafasi hii kumpongeza na
kumshukuru Mkuu wa Mkoa wa Tabora na viongozi wenzake na wananchi wote
wa Tabora
kwa kukubali kuwa mwenyeji wa sherehe hizi na kwa maandalizi mazuri.
Hakika sherehe zimefana sana. Tunawashukuru kwa mapokezi mazuri na kwa
ukarimu wenu.
Pongezi kwa
Wizara na Wananchi
Aidha, nawapongeza
Makatibu Wakuu, viongozi waandamizi na maafisa wa ngazi mbalimbali wa Wizara zetu
mbili husika kwa kazi kubwa na nzuri ya kuandaa na kusimamia utekelezaji wa
programu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2014.
Matunda yake mema sote tunayashuhudia na kujivunia. Pamoja na hao napenda kuwatambua, kuwashukuru
na kuwapongeza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Watendaji wa
Halmashauri na viongozi wa Shehiya, Majimbo, Kata, Vijiji na Mitaa kote nchini
kwa kuziwezesha Mbio za Mwenge mwaka huu kupita kwa usalama katika maeneo yao.
Mwisho, lakini siyo
mwisho kwa umuhimu, nawapongeza na kuwashukuru wananchi wote kwa jinsi
walivyoupokea na kuukimbiza Mwenge katika maeneo yao. Kama tulivyosikia Mwenge umekagua, kuzindua
na kuweka mawe ya msingi kwa miradi 1,451 yenye thamani ya shilingi bilioni
361.3. Hii ni miradi mingi yenye
manufaa makubwa na kufanya mbio hizi kuwa chachu kubwa ya maendeleo hapa
nchini. Hongereni sana.
Pongezi kwa
Wakimbiza Mwenge
Nawapongeza sana
vijana wetu waliokimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa chini ya uongozi wa Ndugu
Rachel Kasanda kwa kazi kubwa na nzuri ya kukimbiza Mwenge kwa siku 165
kupitia Mikoa yote, Wilaya zote, vijiji vingi na mitaa mingi kote nchini. Poleni kwa yote yaliyowakuta lakini uvumilivu
wenu na moyo wenu wa upendo na uzalendo kwa nchi yenu ndivyo vilivyotuwezesha
kufikia kuiona siku ya leo. Mwenge mmeufikisha
salama Tabora ukiwa unang’ara kama ilivyo kawaida yake. Nawashukuru kwa Risala yenu na kwa kunikabidhi
Kitabu kikubwa chenye Risala za Utii za wananchi wa Tanzania. Kama ilivyo ada tutazisoma zote na mambo
yanayostahili kufanyiwa kazi tutachukua hatua stahiki.
Ndugu Wananchi;
Kama mjuavyo, katika sherehe hizi pia tunakumbuka
tarehe na siku kama ya leo mwaka 1999 ambapo mpendwa wetu Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere alitutoka hapa duniani. Ilikuwa siku ya majonzi na simanzi
kubwa. Leo, hata hivyo, siyo siku ya kuomboleza,
bali ni siku ya kusherehekea maisha ya kiongozi wetu mpendwa asiyekuwa na mfano
wake na muasisi wa taifa letu lililo huru la Tanganyika, Desemba, 1961 na wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 26, 1964 kwa kushirikiana na Mzee Abeid
Amani Karume.
Katika kipindi cha
uongozi wake na uhai wake Mwalimu aliifanyia nchi yetu mema mengi ambayo daima
hayatasahaulika. Hivyo basi, siku kama ya
leo ni ya kukumbuka kazi zake nzuri pamoja na mambo mengi mazuri aliyotuachia
kama urithi. Ni siku ya kutafakari na kuona
namna gani tutayadumisha na
kuyaendeleza.
Sherehe za mwaka huu
ni spesheli kweli kweli, kwani zinafanyika siku chache tu baada ya Bunge Maalum
la Katiba kukamilisha kazi yake na kukabidhi Katiba Inayopendekezwa. Katiba hiyo ambayo imepatikana chini ya
uongozi wa mwana Tabora, mashuhuri, Mheshimiwa Samwel Sitta imesisitiza ubora
na kuendelea kwa Muungano wa Serikali Mbili alizoasisi Mwalimu Julius Nyerere akiwa
na Mzee Abeid Amani Karume. Bila ya
shaka mtakumbuka jinsi Mwalimu alivyoupigania muundo huo kwa nguvu zake zote
wakati wa uhai wake. Hatuna budi
kulipongeza Bunge Maalum la Katiba kwa uamuzi wake wa busara ambao unamuenzi kwa
dhati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kudumisha urithi wake mkuu kwetu
ambayo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sijui tungesema nini katika Sherehe za mwaka huu kama ndiyo tungekuwa na
Katiba Inayopendekezwa yenye muundo wa Serikali Tatu?
Mwenge
na Taifa Letu
Ndugu
Wananchi;
Mwenge
wa Uhuru ni moja ya alama muhimu ya umoja wa nchi yetu na utaifa wetu. Mwenge umebeba falsafa kubwa ndani yake
kuhusu nchi yetu na uhusiano wake na watu wengine duniani hasa wanyonge wenye
dhiki wasiokuwa na amani. Wakati wa
harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza Mwalimu
Julius Nyerere aliwahi kusema “Sisi tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu
ya mlima Kilimanjaro, umulike hata nje
ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali
palipo na chuki na heshima palipojaa dharau”. Dhamira hii ilitimizwa tarehe 9 Desemba, 1961
siku Tanganyika ilipopata Uhuru. Pamoja
na kupandisha bendera ya taifa huru la
Tanganyika kwenye Kilele cha Mlima Kilimanjaro na Mwenge wa Uhuru uliwashwa.
Miaka
michache baadaye utaratibu wa kukimbiza Mwenge ulianza na kuendelea mpaka sasa. Mwenge
wa Uhuru umeendelea kumulika nchi nzima ukipita katika mitaa, vijiji, shehia na
majimbo, wilaya na mikoa ukieneza ujumbe wa udugu, umoja, upendo, amani na
mshikamano miongoni mwa Watanzania. Aidha,
Mwenge umeendelea kuwakumbusha Watanzania wajibu wa kufanya kazi kwa bidii na
maarifa ili kujiletea maendeleo yao na ya nchi yetu. Pia wapige vita maovu nchini.
Kwa kuzingatia dhima
nyingine ya Mwenge wa Uhuru, nchi yetu na sisi Watanzania tumejitolea kwa hali
na mali kusaidia ndugu zetu Barani Afrika waliokuwa wanatawaliwa kujikomboa
kutoka kwenye makucha ya wakoloni na wabaguzi wa rangi. Ni fahari kwetu kwamba wananchi wa Msumbiji,
Zimbabwe, Angola, Namibia na Afrika Kusini wamepata ukombozi na uhuru wao na
sisi tumetoa mchango muhimu. Ni jambo la
faraja kubwa kwamba nchi yetu imeweza kuwapatia hifadhi ndugu zetu wa nchi
jirani na hata mbali wakati maisha yao yalipokuwa hatarini kwa sababu ya kukosekana
kwa amani au kwa kukimbia mateso ya uongozi wa kikatili na kidikteta. Ndugu zetu wa Kongo, Burundi, Rwanda, Uganda,
Kenya na Comoro wanajua ukweli huo. Na,
kwa Uganda tuliwasaidia kuling’oa dikteta Idd Amin na Comoro tumewasaidia
kuunganisha tena nchi yao. Hivi karibuni
ndugu zetu wa Sudani Kusini waliniomba tuwasaidie kupatanisha makundi makuu
yanayohasimiana katika Chama chao kikuu cha SPLM. Nimekubali, hivyo tutaanzisha mchakato huo
tuone tutafika nao wapi.
Ujumbe
wa Mbio za Mwenge
Ndugu Wananchi;
Nimefurahishwa sana na
kuafiki ujumbe wa mwaka huu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru unaosomeka “Katiba ni Sheria Kuu ya Nchi: Jitokeze kupiga kura ya Maoni Tupate katiba
Mpya”. Ujumbe huu ni mwafaka kabisa
kwa kipindi hiki cha mchakato wa kupata Katiba Mpya nchini. Pamoja na ujumbe huu
mahususi wa kila mwaka, Mwenge wa Uhuru umeendelea kuelimisha jamii na kutoa
msukumo kuhusu vita dhidi ya UKIMWI, malaria, dawa za kulevya na rushwa. Nawapongeza sana Wakimbiza Mwenge kitaifa kwa
kuwasilisha ujumbe wa mambo yote manne vizuri.
Ndugu Wananchi:
Kama
mnavyofahamu
nchi yetu iko katika mchakato wa kuandaa Katiba Mpya. Mchakato huu sasa
umeingia hatua ya juu kabisa baada ya kumalizika kwa Bunge Maalum la
Katiba kwa
kutunga Katiba Inayopendekezwa. Baada ya
Katiba Inayopendekezwa kukabidhiwa kwangu na kwa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti
wa Bunge Maalum la Katiba tarehe 8 Oktoba, 2014 mjini Dodoma, kazi
inayofuata
ni Kura ya Maoni ya wananchi kuamua ili nchi yetu ipate Katiba Mpya.
Hatua husika kuhusu matayarisho ya kutekeleza
masharti ya Kura ya Maoni zimeshaanza kuchukuliwa. Nawaomba Watanzania
wenzangu muwe na subira. Mtaelezwa na kuelekezwa ipasavyo.
Ndugu Wananchi;
Nimebahatika
kuisoma
Katiba Inayopendekezwa na naendelea kuisoma.
Kwa kweli ni Katiba bora, kuliko hii tuliyonayo sasa yaani Katiba ya
mwaka 1977. Ni Katiba inayotambua na kuimarisha
tunu za taifa letu na mambo mazuri ya huko tulikotoka na hapa tulipo.
Ni Katiba inayorekebisha upungufu uliopo sasa
na kuweka mifumo mizuri inayoendana na wakati tulionao sasa na huko
mbele tuendako. Kwa lugha nyepesi ni Katiba inayotoa majawabu
sahihi kwa changamoto zetu za leo na kesho.
Katiba
Inayopendekezwa inatokana na ushirikishwaji mpana wa wananchi wa Tanzania
walioko ndani na hata wale walio nje ya nchi. Ndiyo maana haki na maslahi ya makundi yote
zimetambuliwa na kupewa nafasi yake stahiki.
Kama mjuavyo, leo pia ni kilele cha Wiki ya Vijana. Napenda mjue kuwa Katiba Inayopendekezwa
imetambua haki za vijana na kuelekeza kuundwa kwa Baraza la Vijana la Taifa. Kuundwa kwa Baraza hilo kutawaongezea vijana
sauti katika kushiriki kwenye utungaji wa sera na uamuzi unaohusu maendeleo ya
vijana na nchi yenu (ambayo ndiyo yetu sote).
Kitakuwa chombo huru cha kuunganisha vijana wote nchini bila kubagua kwa
jinsia, rangi, kabila, dini, ufuasi wa vyama vya siasa na maeneo watokako
katika kutafuta majawabu ya changamoto zinazowakabili ikiwemo tatizo kubwa la ajira.
Hii ni fursa ambayo vijana wamekuwa wakiililia
tangu kutungwa kwa Sera ya Vijana ya mwaka 1996. Hatimaye kilio hiki kimepatiwa kitambaa cha
kufutia machozi na Katiba Inayopendekezwa.
Shime vijana mjitokeze kwa wingi wakati utakapofika, mpige kura ya kuunga
mkono Katiba Inayopendekezwa ili mjitengenezee hatma njema ninyi na vizazi
vyenu. Mnayo nafasi sasa ya kihistoria ya kushika hatamu ya maendeleo
yenu. Katiba Inayopendekezwa ni fursa
hiyo, hakikisheni haiwaponyoki.
Ndugu Watanzania Wenzangu;
Naomba muisome kwa
makini Katiba Inayopendekezwa ili muielewe na kuona jinsi masuala muhimu kuhusu
vijana na wananchi wengine yalivyozingatiwa.
Epukeni kuondolewa kwenye mambo yenye maslahi ya moja kwa moja na ustawi
wenu na kubeba agenda hasi za watu wengine.
Kamwe msikubali kutumika na kutumiwa na wanasiasa au wanaharakati kwa mambo
ambayo hayana tija kwenu na nchi yetu. Nawaomba
vijana mtambue kuwa kwa sababu ya umri wenu, ninyi ndiyo mtakaoishi na kufaidi
matunda ya Katiba Inayopendekezwa kwa miaka mingi ijayo. Kwa sababu hiyo, itumieni fursa hii vizuri,
kutengeneza mustakabali mwema kwenu na kwa vizazi vyenu. Hatima ya nchi yetu iko mikononi mwenu.
Ndugu Wananchi;
Bila ya shaka mnajua
kuwa mwezi Desemba, 2014 kwa upande wa Tanzania Bara kutafanyika Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa. Napenda kutumia fursa
hii kuwashauri vijana na wananchi wote wenye sifa stahiki na kujitokeza
kugombea uongozi. Pia nawaomba mjitokeze
kwa wingi na kushiriki kwa ukamilifu katika kupiga Kura siku ya uchaguzi. Kufanya hivyo ndiko kutakakotupatia viongozi wazuri
wanaoweza kutuvusha na kutupeleka huko mbele kuzuri tunakokutaka. Tushirikiane ili tupate viongozi wanaoendana
na mahitaji ya sasa na ya miaka ijayo mbele.
Ngazi za kitongoji, mitaa na kijiji ndizo ngazi za msingi za kuanzia za kuleta
maendeleo na mabadiliko katika nchi yetu.
Shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma za
jamii hasa zinafanyika katika vijiji, vitongoji na mitaa tunayoishi. Hivyo, mabadiliko mnayoyataka hamna budi
yaanzie katika mitaa au kitongoji unachoishi. Hii ndiyo ngazi inayotugusa moja
kwa moja kila mmoja wetu katika maisha yetu ya kila siku. Hivyo basi, vijana
mjitokeze kugombea uongozi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Vile vile, mwakani kwenye Udiwani, Ubunge na
Uwakilishi, msibaki nyuma. Ni haki yenu
na ni wakati wenu. Gombeeni hata kwa
nafasi ya Urais, na iwapo kuna mtu anayefanana na ujana na atakuwa ametimiza
masharti ya Katiba, asiogope, ajitokeze.
Watu wataamua. Shime jitokezeni
mkawe chachu ya mabadiliko katika maeneo mnayoishi na nchi nzima.
Wiki ya Vijana
Ndugu Wananchi;
Kama
sehemu ya sherehe hizi, jana nilitembelea Kijiji cha Mfano cha Vijana katika wilaya
ya Sikonge. Nimefurahishwa sana na
juhudi zifanywazo na vijana za kujiletea maendeleo. Nimevutiwa na miradi mbalimbali
wanayoitekeleza pale ikiwemo ya kufuga nyuki na kuvuna mazao yatokanayo na
nyuki, ufugaji wa kuku na ng’ombe wa maziwa, ushonaji nguo na viatu. Halikadhalika, shughuli za kilimo na ujenzi
wa nyumba bora. Nimewashauri viongozi wa
Wilaya, Mkoa na Wizara waangalie uwezekano wa kuwafanya vijana hao kuwa wakaazi
na wamiliki wa eneo hilo la miradi ili kiwe kweli kijiji cha mfano badala ya
kuwa mahali pa kupita mithili ya chuo cha mafunzo ya amali.
Baadae nitapata nafasi
ya kutembelea mabanda ya maonesho ya kazi wafanyazo vijana na wadau wengine hapa
uwanjani. Maonyesho haya yanathibitisha kwa
uwazi fursa zilizopo za kuwaendeleza vijana.
Lililo muhimu kufanya, ni kwa vijana kuwa na upeo mzuri wa ufahamu wa
mambo, ubunifu, moyo wa kujituma na kufanya kazi kwa bidii. Mkifanya hivyo tutaondokana na tatizo la
ukosefu wa ajira na umaskini kwa vijana na taifa kwa ujumla.
Ndugu Wananchi;
Kwa kutambua ukweli
huu, ndiyo maana Serikali zetu zimeongeza bajeti katika Mifuko ya Maendeleo ya
Vijana kupitia Wizara zetu mbili zinazosimamia na kuratibu maendeleo ya vijana. Shabaha yetu ni kuwawezesha vijana wengi
zaidi kupata mikopo na kuwa na mitaji ya kutekeleza miradi yao itakayowawezesha
kujiajiri wenyewe na kujipatia kipato. Naikumbusha Wizara inayosimamia na
kuratibu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kuhakikisha kwamba fedha za Mfuko huo
zinawafikia walengwa na, kwa wakati muafaka.
Kwa upande mwingine
nazikumbusha Halmashauri zote za Wilaya na Miji kutekeleza kwa ukamilifu agizo
la kutenga asilimia 10 ya mapato yao kwa mwaka kwa ajili ya shughuli za
maendeleo ya Vijana na Wanawake. Ninazo
taarifa kuwa baadhi ya Halmashauri zinalitekeleza vizuri agizo hili lakini zipo
nyingine ambazo zinasuasua. Nataka
isiwepo hata Halmashauri moja ya kunyooshewa kidole kwa kutokufanya vizuri kwa jambo
lenye manufaa kwa vijana wetu kama hili.
Naomba nitumie nafasi hii leo kuzitaka Halmashauri zote kutoa taarifa za
mara kwa mara za utekelezaji wa agizo hili.
Taarifa ya kwanza kwa ajili hiyo itolewe mwisho wa mwezi Desemba, 2014,
ifuatayo iwe miezi minne baadae na kila baada ya miezi minne.
Mapambano
Dhidi ya UKIMWI
Ndugu
Wananchi;
Janga
la UKIMWI bado ni tatizo kubwa nchini hivyo ni sahihi kabisa kwa Mwenge
kuendelea kulisemea. Inakadiriwa kuwa
tunao wagonjwa wa UKIMWI milioni 1.4.
Bahati mbaya waathirika wengi
zaidi ni vijana. Takwimu za maambukizi
zinaonyesha pia kuwa wasichana wa umri wa miaka 20 – 24 wako katika
hatari ya kuambukizwa karibu mara tatu ikilinganishwa na wavulana wa umri huo
huo.
Ni jambo la kutia
moyo kwamba kiwango cha maambukizi kinashuka mwaka hadi mwaka kutokana na
shughuli za uhamasishaji ambazo na Mwenge nao una mchango wake. Kwa mfano, kiwango cha maambukizi kimeshuka
kutoka asilimia 5.7 mwaka 2010 hadi asilimia 5.1 mwaka 2012. Kiwango cha maambukizi ya UKIMWI hapa mkoani
Tabora ni wastani wa asilimia 5.1 ambayo ni sawa na kiwango cha kitaifa. Mwelekeo huu kwa taifa na Tabora ni mzuri
lakini tusibweteke bali tuongeze bidii katika mapambano. Watu watano katika kila 100
kuwa wameambukizwa ni wengi mno.
Isitoshe maambukizi mapya 78,843 ni makubwa mno, tunataka
maambukizi mapya yawe sifuri.
Tumeendelea
kupata mafanikio ya kutia moyo katika vita dhidi ya UKIMWI. Idadi ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI
wanaopata tiba imeongezeka kutoka 201,181 (2005) hadi 512,555
mwaka 2013. Hali kadhalika tumewezesha
huduma za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kutolewa karibu
katika Kliniki zote nchini (aslimia 97).
Vilevile, idadi ya waliopima afya zao imeongezeka kutoka watu 365,189
mwaka 2005 hadi 20,469,241 mwaka 2013.
Katika mwaka 2013 peke yake, watu 2,793,636 walipima afya
zao. Yote hayo ndiyo yanayochangia
kupungua kwa maambukizi.
Ndugu Wananchi;
Ili
kushinda vita hii hatuna budi kukumbushana kuachana na tabia na mienendo inayowaweka
wanaadamu katika hatari ya maambukizi.
Mimi naamini Watanzania tunaweza kabisa kushinda vita dhidi ya UKIMWI. Kinachotakiwa ni kuamua kukataa kupata
maradhi haya. Inawezekana, timiza wajibu
wako.
Mapambano Dhidi ya Rushwa
Ndugu Wananchi;
Tumeendelea na mapambano dhidi ya rushwa na
mafanikio yanaendelea kupatikana. Watu
wengi zaidi hivi sasa wakiwemo vijana, wamefikiwa na kampeni ya kuwafanya watambue
madhila yake, waichukie rushwa na wawe tayari kujitokeza kupambana na uovu
huu. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) imeongeza kasi ya kupambana na rushwa. Katika kipindi cha Julai 2013 hadi Juni, 2014
imefanikiwa kufungua kesi mpya 327, kati ya hizo kesi tatu ni za rushwa kubwa. Aidha, shilingi bilioni
38.96 zimeokolewa. TAKUKURU sasa imekwenda mbali zaidi na
kuanzisha ofisi za Waratibu wa Kanda (Public Expenditure Tracking System – PETS
Coordinators) wenye jukumu la kufuatilia matumizi ya fedha kwenye shughuli za ununuzi
hasa kwenye miradi ya maendeleo.
Tumefanya hivyo kwa kutambua kuwa shughuli
za ununuzi kwenye Halmashauri na Serikali Kuu kwa jumla ndiko waliko mchwa
wengi, wakubwa na wanene. Katika kipindi
cha 2013/14 pekee, miradi 215 yenye thamani ya shilingi bilioni 20.594 imekaguliwa.
Kati ya miradi hiyo, miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 9.59 ilionekana kuwa na mazingira ya mashaka na
uchunguzi wa kina unaendelea hivi sasa.
Itakapothibitika kuwepo kwa dalili za rushwa, hatua zipasazo za kisheria
zitachukuliwa bila ya ajizi.
Ndugu
Wananchi;
Tunaweza kupata ushindi mkubwa zaidi katika vita dhidi ya
rushwa na mafanikio tunayoendelea kupata ni ushahidi wa ukweli wa kihistoria. Sisi katika Serikali tutaendelea kutekeleza
wajibu wetu kwa kuiwezesha TAKUKURU kwa rasilimali watu, vitendea kazi na
majengo. Mwaka huu pekee tumeiwezesha
Taasisi kuajiri Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi 304 ili kuimarisha utendaji katika taasisi yetu hii
muhimu. Tunachohitaji ni ushirikiano wa
karibu wa wananchi katika kuwafichua wale wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.
Ukweli ni kwamba watu hao tunaishi nao katika maeneo yetu. Tuache kuwatukuza na kuwalinda kwani kwa
kufanya hivyo tunawaimarisha, na kuwakatisha tamaa watu waadilifu na wale walio
mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa. Tuyachukue mapambano dhidi ya rushwa kuwa ni yetu
sote na siyo ya TAKUKURU au viongozi peke yao.
Ushindi dhidi ya rushwa ni ushindi wetu sote. Hali kadhalika, kushindwa
vita dhidi ya rushwa ni kushindwa kwetu sote.
Ni hasara kwako na taifa kwa jumla.
Vita
Dhidi ya Dawa za Kulevya
Ndugu Wananchi;
Tunaendelea na mapambano dhidi ya matumizi na biashara
haramu ya dawa za kulevya. Tunaendelea
kupata mafanikio pamoja na ugumu uliokuwepo katika mapambano hayo. Wahalifu wamekuwa wakibadili mbinu na
kuongeza nguvu kila kukicha. Hata hivyo,
na sisi tumekuwa na unyumbufu wa kutosha. Ukweli ni kwamba kadri wahalifu hao wanavyoongezeka
na ndivyo wanavyoongezeka kukamatwa. Wakati
katika kipindi cha Januari hadi Septemba
mwaka 2013 walikamatwa watuhumiwa 2,000, mwaka huu tangu Januari, hadi kufikia Oktoba, (2014)
watuhumiwa 6,875 wameshakamatwa
na kesi zao ziko katika hatua mbalimbali. Takwimu hizi zinaonyesha namna tulivyoongeza
nguvu na tunavyofanikiwa katika juhudi zetu.
Katika Mkoa wa Tabora peke yake, washitakiwa 177 wamefikishwa Mahakamani.
Kilichonisikitisha zaidi ni taarifa kuwa sasa kilimo cha bangi kinaongezeka
kwa kasi mkoani Tabora. Nawaomba
muendelee kuwa wakulima hodari wa tumbaku pekee na siyo kilimo cha bangi.
Ndugu
Wananchi;
Tumeendelea
kuchukua hatua nyingi madhubuti kukabiliana na mtandao wa
uuzaji na usafirishaji wa dawa za kulevya, ndiyo maana taarifa za
matukio ya
kukamatwa watu katika viwanja vyetu vya ndege zimepungua sana tofauti na
mwanzo
mwa mwaka huu. Hii inaashiria kuwa mambo
yamekuwa magumu kwenye njia hiyo, lakini tunajua wanatafuta au
watatafuta njia nyingine. Kwa yote mawili hawatafika mbali, mkono mrefu
wa sheria utawafikia.
Tumeendelea
kutoa huduma za kuwasaidia waathirika wa dawa za kulevya
kuacha kutumia dawa hizo na kurejea katika maisha ya kawaida. Vituo
vyetu vya majaribio katika hospitali za
Muhimbili, Mwananyamala na Temeke sasa vinahudumia waathirika wapatao
1,835 kwa
kutumia dawa ya Methadone. Tanzania ni
moja kati ya nchi chache sana Afrika ambazo zimepiga hatua kubwa katika
kutibu
waathirika wake na wenzetu sasa wanakuja kujifunza kwetu. Tutafanya
zaidi ya tufanyavyo sasa. Nia yetu ni kueneza huduma hiyo nchi nzima
ili kunufaisha vijana wetu wengi.
Ndugu
Wananchi;
Tunayo kila sababu ya kushinda vita hii. Hatamu ya ushindi wetu iko mikononi mwa wananchi
wa Tanzania na vijana ambao ndiyo waathirika na wateja wakubwa wa dawa
hizo. Kataeni kuwa mawakala wa biashara
hii haramu na ya maangamizi. Pia kataeni
kuwa watumiaji wa dawa za kulevya.
Biashara hii haiwezi kushamiri iwapo hapatakuwepo na mawakala na wateja
wa uhakika. Sisi Serikalini tunaendelea
kuchukua hatua stahiki. Sasa tunapitia upya sheria ili tuweze kuanzisha taasisi
mpya yenye mamlaka makubwa ya kupambana na dawa za kulevya kuliko Tume ya
Kudhibiti Dawa za Kulevya iliyoko sasa.
Maandalizi yamefikia pazuri.
Tutakamilisha jambo hili mapema iwezekanavyo.
Maji na Barabara
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza
naomba niwathibitishie wananchi wa Mkoa wa Tabora kwamba ahadi yangu ya kuleta
maji mjini Tabora, Nzega na Igunga kutoka Ziwa Victoria iko palepale. Tumechelewa kuanza kutokana na kuendelea
kutafuta fedha za kutekeleza dhamira yetu hiyo.
Nafurahi kusema kuwa Mungu ni mwema tumefanikiwa. Serikali ya India imekubali maombi yangu na
watatukopesha kiasi cha dola za Marekani milioni 264 kwa ajili ya
kutekeleza mradi huu. Wataalamu
wanamalizia michoro ya mradi ili baada ya hapo ujenzi uanze. Subira yavuta heri, wote tuwe wavumilivu.
Tunaendelea na
jitihada za kujenga barabara mbalimbali kwa kiwango cha lami hapa Mkoani
Tabora. Barabara zinazoendelea kujengwa
zitakamilishwa na zile zinazoendelea na maandalizi zitaanza pindi tutakapopata
fedha. Lengo letu ni kuunganisha Mkoa
huu na Mkoa wa Katavi, Kigoma na Singida kupitia Itigi hadi Manyoni. Tumezungumza na Kuwait Fund ili watusaidie
kujenga barabara ya Nyahua – Chaya wamekubali. Hali kadhalika, Benki ya Maendeleo ya Afrika
wanaelekea kuwa tayari kutupatia mkopo wa ujenzi wa barabara ya Tabora - Sikonge – Koga - Mpanda.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Narudia tena
kuwashukuru wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine kufanikisha sherehe
hizi ambazo zimefana mno. Baada ya
kusema hayo natamka rasmi kwamba shughuli za Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka
huu zimefikia kilele chake leo.
Nawatakia kila la
kheri katika shughuli zenu za kila siku.
Mungu
Ibariki Tanzania!
Mungu
Ibariki Afrika!
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia