BREAKING NEWS

Saturday, September 30, 2017

CHINA YAIPATIA TANZANIA MSAADA WA SH. BILIONI 29.4 KWA AJILI YA MIRADI YA MAENDELEO


 Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (wa pili kulia)
na Kaimu Balozi wa China Nchini Tanzania, Mhe. Gou Haodong (wa tatu
kushoto) wakisaini makubaliano ya msaada wa Sh. bilioni 29.4 kwa ajili ya
miradi ya Ujenzi wa Chuo cha VETA Mkoani Kagera, Utalii wa Kijilojia na
Ukarabati wa Uwanja wa Taifa, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango
Jijini Dar es Salaam.

Kaimu Balozi wa China Nchini Tanzania, Mhe. Gou Haodong (kushoto) na Katibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (kulia) wakibadilishana
hati ya makubaliano ya msaada wa Sh. bilioni 29.4 kwa ajili ya miradi ya
Ujenzi wa Chuo cha Ufundi (VETA), Mkoani Kagera, Utalii wa Kijiolojia na
Ukarabati wa Uwanja wa Taifa, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango
Jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi Amina Khamis Shaaban
(kushoto) na Kamishna wa Fedha za Nje wa Wizara hiyo Bw. John Rubuga
(kulia) wakishuhudia utiliwaji saini makubaliano ya msaada wa Sh. bilioni
29.4 uliotolewa na China kwa ajili ya miradi ya Ujenzi wa Chuo cha Ufundi
(VETA) Mkoani Kagera, Utalii wa Miamba na Ukarabati wa Uwanja wa Taifa,
katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam


Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (katikati), Kaimu
Balozi wa China Nchini Tanzania, Mhe. Gou Haodong (wa pili kulia) na
Maafisa waandamizi kutoka Tanzania na China wakiwa katika picha ya pamoja
baada ya kusainiwa makubaliano ya msaada wa Sh. bilioni 29.4 uliotolewa na
Serikali ya China kwa ajili ya miradi mbalimbali katika ukumbi wa Wizara ya
Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam



SERIKALI ya China imeipatia Tanzania msaada wa Shilingi bilioni 29.4 kwa
ajili ya kusaidia sekta ya elimu ya ufundi stadi, utalii wa kijiolojia na
kukarabati wa Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.



Makubaliano ya msaada huo yametiwa saini Jijini Dar es Salaam na Katibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, kwa niaba ya Serikali,
na Kaimu Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Gou Haodong.



Bw. Doto James alisema kuwa kiasi cha Shilingi bilioni 22.4 cha msaada huo
kitatumika kujenga Chuo cha Ufundi Stadi-VETA wilayani Ngara mkoani Kagera,
ambacho kitakapo kamilika kitadahili zaidi ya wanafunzi 400.



“Fedha hizo zitatumika kujenga vyumba 19 vya madarasa, ujenzi wa karakana 9
za kutolea mafunzo ya elektroniki, ufundi bomba, useremala, ufundi uashi na
upakaji rangi” alisema Bw. James



Alieleza kuwa kiasi hicho pia kitatumika kujenga majengo ya utawala,
mabweni, nyumba za walimu na miundombinu mingine itakayosaidia kuboresha
mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwenye chuo hicho.



“Tunaamini kwamba msaada huo utakuwa sehemu ya kusaidia jitihada za
Serikali za kujenga uwezo wa wataalamu wake watakaochangia kukuza sekta ya
uzalishaji na hatimaye kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana
nchini” alisema Bw. James



Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James alibainisha
kuwa katika makubaliano ya msaada huo, Jamhuri ya watu wa China, itatoa
kiasi cha shilingi bilioni 6.7 kwa ajili ya kuukarabati Uwanja wa Taifa wa
Michezo wa Dar es Salaam.



“Katika makubaliano yetu ya msaada wa kuendeleza Uwanja wa Taifa wenye
uwezo wa kuingiza watu 60,000, China itatoa msaada wa kiufundi na vifaa vya
kisasa vya michezo na utaalamu katika usimamizi na ukarabati wa uwanja”
Alifafanua Bw. James



Bw. Doto James alisema kuwa kiasi kingine cha shilingi  milioni 300
kitatumika kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa kuanzishwa kwa aina
mpya ya utalii ujulikanao kama utalii wa kijiolojia “Geopark Project”
katika Hifadhi ya Taifa Ngorongoro, mkoani Arusha.



Alisema lengo la utafiti huo ni kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika na
maajabu mbalimbali ya kitalii yaliyopo nchini ambayo hayajatumika
kikamilifu kuvutia watalii watakaoongeza pato la Taifa



“Tanzania ina kila sababu ya kujifunza kutoka katika Hifadhi ya Kimataifa
ya Jiolojia ya Jiaozuo ya Yuntaishan ya China, iliyoanzishwa mwaka 2000
ambayo inaongeza asilimia 37.2 ya watalii kila mwaka na huchangia asilimia
12 ya pato la Taifa la nchi hiyo” aliongeza Bw. Doto James.



Aliishukuru China kwa ushirikiano wake wa dhati na Tanzania tangu miaka ya
1960 na kwamba mpaka sasa nchi hiyo imeendelea kuipiga jeki Serikali katika
ujenzi wa miradi mbalimbali ukiwemo upanuzi wa Chuo cha Polisi Moshi,
Ujenzi wa Maktaba mpya katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na ujenzi wa
Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.



Kwa upande wake Kaimu Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Gou Haodong,
amesema kuwa nchi yake inatarajia kwamba ujenzi wa Chuo Cha Ufundi VETA
huko Ngara mkoani Kagera utaanza haraka kama ilivyopangwa.



Kuhusu masauala ya utalii wa kijiolojia katika Hifadhi ya Taifa Ngorongoro,
alisema Tanzania ina bahati ya kuwa na vivutio vingi vya utalii lakini
haijavutia idadi kubwa ya watalii kutoka China kuja kuvitembelea.



“Zaidi ya watalii milioni moja kutoka China wanatembelea nchi mbalimbali
dunia lakini kati ya hao, Tanzania inapokea watalii elfu 20 tu kila mwaka
kutoka China, lakini kwa kuanzisha mradi huu, watalii wengi kutoka China
watavutiwa kuja nchini kufurahia utalii wa miamba, mandhari nzuri, urithi
wa dunia, na kutembelea hifadhi za Taifa” aliongeza Mhe. Haodong



Akizungumzia masuala ya uchumi, Balozi huyo alisema kuwa hivi sasa China
imekuwa mwekezaji mkubwa zaidi nchini Tanzania kwa kuwekeza kiasi cha Dola
za Marekani bilioni 1.77 na kukuza ajira nchini.



Ameitaja baadhi ya miradi mikubwa iliyowekezwa kuwa ni pamoja na mradi wa
miundombinu ya mtandao (*Tanzania ICT Broadband backbone),* Bomba la gesi
la kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, mradi wa kuboresha miundombinu ya
Bandari, barabara na madaraja.



Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo, ambaye alisema kuwa msaada wa ujenzi wa
Chuo cha Ufundi VETA mkoani Kagera kitaongeza watalaamu watakaosaidia
kuendeleza sekta ya viwanda nchini.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates