WANANCHI WAHIMIZWA KUJIUNGA NA MFUKO WA AFYA YA JAMII


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizugumza na wananchi wa Kata ya Ngulyati wilayani Bariadi katika Mkutano wa hadhara wakati wa ziara yake yenye lengo la kusikiliza kero mbalimbali za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.
Mchungaji Nicholuos Chimbu mkazi wa Kijiji cha Ngulyati(kulia) wilayani Bariadi akiwasilisha kero yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) alipofanya ziara wilayani humo kwa lengo la kuzikiliza kero za wananchi na kuzitafuatia ufumbuzi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga wakiteta jambo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa katika Kata ya Ngulyati aliyofanya kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Minza Maduhu mkazi wa Kijiji cha Ngulyati wilayani Bariadi akiwasilisha kero yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) alipofanya ziara wilayani humo kwa lengo la kuzikiliza kero za wananchi na kuzitafuatia ufumbuzi
Eliasi Hopi mkazi wa Kijiji cha Nyasosi Kata ya Ngulyati wilayani Bariadi aliwasilisha kero kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) alipofanya ziara wilayani humo kwa lengo la kuzikiliza kero za wananchi na kuzitafuatia ufumbuzi.
Afisa Uhusiano wa TANESCO Mkoa wa Simiyu akitolea ufafanuzi suala la utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini REA Awamu ya III ambalo liliulizwa na wananchi wa Kata ya Ngulyati wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka aliyoifanya kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Kikundi cha Burudani cha Msanii Polepole kutoka Ngulyati kikitoa burudani ka wananchi na viongozi katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) aliyoifanya katika kata ya Ngulyati wilayani Bariadi kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.


Na Stella Kalinga, Simiyu

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka ametoa wito kwa wananchi Wilayani Bariadi mkoani humo kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii(CHF).

Mtaka ametoa wito huo wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Ngulyati wilayani Bariadi wakati wa ziara yake yenye lengo la kusikiliza kero mbalimbali za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.

Amesema azma ya Serikali ni kuwa ifikapo mwaka 2020 Watanzania wote wawe wamejiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii(CHF) au Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), hivyo akawahamasisha wananchi ambao bado hawajajiunga na CHF kujiunga kwa kuwa gharama yake ni nafuu.

“Watu wa Ngulyati ni wafanyabiashara wazuri, wafanyakazi wazuri, wakulima wazuri ningetamani kuwaona wote hapa mnakuwa na kadi za Mfuko wa Afya ya Jamii ambazo zinapatikana kwa gharama ya shilingi 10,000, hii ni sawa na kuku mmoja tu mnapata matibabu watu sita kwa maana ya baba, mama na watoto wa nne” amesema.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha vituo vya kutolea huduma za afya ili wananchi waweze kupata huduma bora, ambapo Serikali kupitia Mradi wa RBF(Result Based Financing/Kulipa kulingana na Matokeo) imetoa fedha kwa ajili ya kuboresha huduma.

Akitoa ufafanuzi wa fedha hizo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Bariadi, Ndg.Abdallah Malela amesema, kupitia mradi wa RBF Halmashauri hiyo imepokea shilingi milioni 260, zilizogawanywa katika vituo vilivyopo 26 vya kutolea huduma za afya ambapo kila kituo kimepokea shilingi Milioni 10 ili kuboresha utoaji wa huduma za Afya.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga kufuatilia na kuhakikisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi anawasilisha kwake taarifa ya fedha za Mradi wa RBF alizopokea na kazi zilizofanyika katika vituo vya kutolea huduma.

“Mhe. DC umesikia hapa hawa watu wamepokea fedha toka mwezi saba mwaka huu na leo ndio wamekaa kikao cha mpango, maana yake ni kwamba mwezi wa nane wananchi hawajapata huduma zilizokusudiwa na Wizara ya Afya, na naamini yanayofanyika kwenye kituo hiki yapo katika vituo vyako vyote, sasa nimuombe Mkurugenzi wa Mji Jumatatu atuletee taarifa ya mpango uliotekelezeka” amesema Mtaka.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga amemhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kuwa atalifuatilia suala hilo pamoja na kutekeleza maelekezo yote aliyoyatoa katika ziara hiyo na ameahidi kuwachukulia hatua watumishi watakaoshindwa kutimiza wajibu wao katika kuwahudumia wananchi.

Kuhusu suala la taratibu za uwekaji wa umeme wa REA awamu ya III kwa wananchi na Taasisi za Umma ambalo liliwasilishwa na wananchi akiwemo Mwl. Daudi Jackson, Mkuu wa Mkoa, Mhe.Anthony Mtaka amesema atakutana na Meneja wa TANESCO Mkoa siku ya Jumatatu Septemba 04, ili wajadili namna na kushughulikia suala hilo.

Katika hatua nyingine Mtaka amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi kuhakikisha Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri anafika eneo la ujenzi wa Soko la Ngulyati Jumatatu tarehe 04 Septemba kukutana na viongozi wa Kijiji na Kata, kwa ajili ya kuanza mpango wa ujenzi wa soko hilo ili kutatua kero ya ukosefu wa soko na kuwawezesha wananchi kupata sehemu ya kuuzia bidhaa zao.

Wakati huo huo Mtaka amewataka wananchi kutumia vizuri msimu wa kilimo, kulima mazao yanayostahimili ukame na akawasisitiza kutunza chakula walichokipata katika msimu uliopita kwasababu Serikali haitakuwa na chakula cha msaada.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post