
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Kamishina Msaidizi wa
Polisi (ACP) Barnabas Mwakalukwa amewataka wananchi kwa ujumla
wanaofanyiwa vitendo vya uhalifu mitandaoni wasiende TCRA bali wanapaswa
kutoa taarifa katika jeshi la polisi.ACP Mwakalukwa amebainisha hayo
wakati alipokuwa anazungumza katika mkutano wa pamoja na Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhusu suala zima la uhalifu wa makosa ya
mitandao ambapo kwa sasa limeshika kasi kubwa
"Chochote kinachofanyika ambacho ni kosa jinai
nawaomba msiende Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kwa watoa
huduma wa mitandao ya simu mbalimbali wala katika vyombo vya kutolea
habari bali unapaswa uje katika kituo cha polisi utoe taarifa zako kama
ni kosa la jinai kwa sababu mkienda huko uchunguzi utakuwa shida kwa
maana wewe mwenyewe utaweza kusababisha hata yule aliyekutendea uhalifu
atoroke", amesema ACP Mwakalukwa
Pamoja na hayo, ACP Mwakalukwa ameendelea kwa kusema "Kutokana
na kukua kwa teknolojia vitu vingi vimekuwa vikifanyika 'online' kwa
hiyo hii mitandao ya kijamii imeonekana ni muhimu sana kwenye maendeleo,
lakini pia imebadilisha mbinu ya kufanya uhalifu katika mitandao ya
kijamii kwa kutumiwa na baadhi ya watu kutapeli, hata kutishia kuua,
hivyo jeshi la polisi limejipanga kwa ajili ya kushughulikia makosa
ambayo yanatokana na mtandao", amesema Mwakalukwa.
Kwa upande wake,Kaimu Mkurugenzi wa TCRA, Thadayo Ringo
amesema analishukuru jeshi la polisi kwa kuweza kuwasaidia katika
kuwatatulia changamoto mbalimbali hasa za kiusalama huku akiwataka
wananchi watakaopata matatizo katika mtandao kwenda kutoa taarifa polisi
ili waweze kuwasaidia kabla ya kufika kwao.