Wananchi wa
Kitongoji cha Saitabau, Kata ya Tarakwa wilaya ya Arumeru,Mkoa wa Arusha,
wamegoma kujiunga na Mamlaka ya mji mdogo wa Ngaramtoni na kuruhusu mradi wa
maji katika kijiji chao kuwa chini ya Mamlaka hiyo.
Kutokana na
mgomo huo, Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameamua kuunda kamati ya
wataalam kutoka ofisini kwake ili kuchunguza mgogoro huo. Wakizungumza
na Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo aliyefika katika kitongoji hicho,
kukagua mradi wa maji wa Olosaita uliokwama, ikiwa ni sehemu ya ziara
yake ya siku tano katika halmashauri ya Arusha vijijini, wananchi hao walisema
hawataki kujiunga na Mamlaka hiyo kwani hawajuwi faida zake.
Mwenyekiti
wa kitongoji hicho,Lucas Lukumai alisema wananchi wanapinga kujiunga na Mamlaka
hiyo, kutokana na kutopatiwa elimu na pia mamlaka kutaka kuchukuwa mradi wao wa
maji ambao waliuchangia na kusaidia na shirika la Oxfam.
"Mimi
nilikamatwa na kuwekwa rumande na polisi kwa agizo la Mkurugenzi wa
halmashauri kwa tuhuma za kukataa mamlaka jambo ambalo sio kweli wanaokataa ni
wananchi wenyewe kwani hawajapewa elimu"alisema Alisema
viongozi wa Mamlaka walipewa fursa ya kukutana na wananchi na kutoa elimu
lakini wameshindwa kufanya hivyo, badala yake wanawatuhumu viongozi.
Akijibu
tuhuma hizo, Mtendaji mkuu wa Mamlaka ya mji mdogo, Sophia Shoko alisema
wananchi wanagomea kujiunga na mamlaka kwa lengo la kuzuia mradi wa maji usiwe
chini ya Mamlaka yao.
"hapa
kuna mradi wa maji, wenyewe hawataki uwe chini ya Mamlaka ili maji yasambazwe
maeneo mengine na wanataka kuendelea na malipo ya sh 500 kwa mwezi jambo ambalo
sio sahihi"alisema.
Hata hivyo,
Diwani wa kata hiyo, Elihuruma Laizer alimuomba Mkuu wa mkoa kuunda kamati
maalum ya kuchunguza suala hilo na atafute fursa ya kukaa na wananchi
kuwasikiliza kwani jambo hilo lina mgogoro mkubwa.
Akizungumza
baada ya majadiliano hayo, Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alisema
anakubaliana na ushauri wa Diwani wa kata hiyo, kuunda kamati maalum ya
kuchunguza mgogoro huo kabla ya kuchukuwa hatua.
"nitaunda
kamati ya wataalam kutoka ofisini kwangu watakuja hapa na kuzungumza na
wananchi , viongozi wa Mamlaka ya mji mdogo na viongozi wa kitongoji na
baadaye watanipa ushauri kufikia maamuzi"alisema.
Mamlaka ya
mji mdogo wa Ngaramtoni, iliundwa mwaka jana na halmashauri ya Arusha vijijini
ili kupeleka huduma za kiserikali karibu zaidi na wananchi .
0 Comments
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia