MWENYEKITI wa Baraza la Wanawake Chadema Taifa
(Bawacha),Halima Mdee ameitaka jamii kupaza sauti pale inapobaini kuwepo
kwa unyanyasaji dhidi ya mtoto na kupigania haki ya mtoto wa kike
kupata uongozi .
Akizungumza katika kituo cha watoto yatima cha Samaritan
Village kilichopo Moshoni,jijini hapa katika maadhimisho ya jubilei ya
miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Chama cha demokrasia na Maendeleo
(Chadema) alisema kuwa lazima jamii ipaze sauti zao ili watoto wabaki
salama pale inapoonekana kuna dalili za unyanyasaji.
Aidha alisema kuwa pamoja na chamgamoto nyingi anazozipata
kama mbunge, kamwe hatanyamaza na ataendelea kumtetea mtoto na kuitaka
jamii iwe mstari wa mbele kupinga ndoa za utotoni kwa mtoto wakike.
Alisema watoto katika jamii wanafanyiwa ukatili mwingi,
hivyo mtu yoyote anayejitokeza kulea watoto yatima anapaswa kupongezwa
na kuungwa mkono kwani hilo ni taifa la kesho.
Katika maadhimisho hayo bawacha mkoa wa Arusha imetoa
msaada wa vitu mbalimbali pamoja na kupanda mti wa kumbukumbu katika
kituo hicho cha watoto yatima Kama Sehemu ya maadhimisho .
Kwa upande wake mwenyekiti wa Bawacha mkoa wa Arusha,Cesy
Ndosi alisema kuwa wameamua kuungana na watoto yatima katika
kusherehekea maadhimisho ya miaka 25 ya chama hicho kama kutambua
mchango wa watoto kwa taifa na kuitaka jamii kuyakumbuka makundi
yaliyosahaulika kama watoto na wazee .
Naye Mratibu wa kituo cha yatima Samaritan Village,
Josephat Mmanyi alishukuru kwa msaada huo na kusema kituo lina watoto 50
wenye umri wa miaka 21 hadi mwaka mmoja na wapo ngazi mbalimbali za
shule.Hata hivyo alisema kituo bado kinachangamoto ya gharama za
uendeshaji.
Alitumia fursa hiyo kimwomba Halima Mdee kupanda mti
kituoni hapo ili kuamsha ari ya watoto wake wanaotamani kuwa wanasheria
kama yeye.