BREAKING NEWS

Tuesday, March 15, 2022

BARAZA LA UONGOZI CHUO CHA UHASIBU ARUSHA WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA KUFUATA SHERIA SERA NA KANUNI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Emmanuel Tutuba (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kushoto kwake Dkt. Mwamini Tulli na kulia kwake ni Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Cairo Mwaitete



Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Emmanuel Tutuba akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) jijini Arusha. Katikati ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Dkt. Mwamini Tulli na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Cairo Mwaitete






Kushoto meneja wa maktaba ya chuo Cha uhasibu Arusha Joseph Daudi akiwaeleza katibu mkuu wa wizara ya fedha na mipango na mlipaji mkuu wa serikali Emmanuel Tutuba pamoja na bodi ya chuo hicho namna maktaba hiyo inavyofanya kazi ambapo alisema maktaba hiyo inauwezo wa kuubeba watu 600 Kwa wakati mmoja na wamekuwa wakinunua vitabu vipya Kila mwaka





Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Emmanuel Tutuba amelitaka Baraza la Uongozi la Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) wakati wa utekelezaji wa majukumu yake, kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Sera, Kanuni na Miongozo mbalimbali ya Serikali kwa maslahi mapana ya Taifa.

Bw. Emmanuel Tutuba alitoa wito huo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), uliofanyika katika ukumbi wa Chuo hicho jijini Arusha.

“Tuna imani na ninyi na nimatumaini yetu kwamba mtatumia weledi wenu kwa uadilifu katika kutekeleza majukumu mliyopewa ili kuhakikisha kwamba, Chuo chetu kinakua na kinakidhi matarajio tuliyojiwekea” alisema Bw. Tutuba”.

Alilitaka Baraza hilo kuhakikisha wanashirikiana na Menejimenti ya Chuo kusimamia matumizi ya fedha za Serikali ikiwa ni pamoja na mali za Chuo zinazo hamishika na zisizohamishika, ili kufikia malengo makubwa waliojiwekea.

Sambasamba na uzinduzi wa Baraza hilo Bw. Tutuba alitembelea maeneo ya Chuo hicho ambapo alijonea miundombinu mbalimbali chuoni hapo na kusikiliza changamoto mbalimbali zinazokikabili Chuo hicho ikiwemo uhaba wa makazi kwa wanafunzi.

Bw. Tutuba aliahidi kufanyia kazi changamoto ya makazi kwa wanafunzi ambao asilimia 90 wanakaa nje ya maeneo ya Chuo ili kuhakikisha wanafunzi hao wanaishi chuoni ili wawe karibu na mazingira ya chuoni.

“Nimetembea na nimeona ujenzi unaoendelea hivyo, naahidi kulifanyia kazi ombi lenu la kupata fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa makazi ya wanafunzi wetu alisema Bw. Tutuba”.

Alitoa wito kwa Mwenyekiti pamoja na Wajumbe wote wa Baraza la Uongozi kwa kuteuliwa kwao kuwa wasimamizi wa shughuli za Chuo, aliwataka wakawe chachu ya kuchochea uzalendo na utumishi wa umma kwa Chuo hicho.

“Nitumie nafasi hii pia kuwakaribisha kwenye familia ya Wizara ya Fedha na Mipango. na matarajio yangu mtatekeleza majukumu yenu kwa ushirikiano wa karibu na Wizara pamoja na Taasisi nyingine ili kuhakikisha mipango tuliyojiwekea inafikiwa”, alisema Bw. Tutuba”.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Dkt. Mwamini Tulli, aliwataka wajumbe wa Baraza hilo kushirikiana katika kutimiza majukumu waliyopewa kwa mujibu wa sheria katika kipindi chote cha miaka mitatu watakayokuwa wakitekeleza majukumu yao.

Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Cairo Mwaitete amesema kuwa Chuo kimeendelea kuhakikisha kina miundombinu wezeshi ili vijana wasome katika mazingira bora na salama chuoni pamoja na kuhakikisha IAA inaendelea kutoa elimu bora.
 

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates